Thursday, 15 December 2016

Wadau wa sekta ya filamu Mkoani Mara wametakiwa kuzingatia weledi na ubora wakati wa kuandaa filamu.

mara Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Bibi. Joyce Fissoo (kushoto) akijibu swali wakati wa warsha ya mafunzo ya kuwajengea uwezo wadau wa sekta ya filamu na michezo ya kuigiza leo Mkoani Mara. Kulia ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bibi. Nuru Millao
mara-1
Mtendaji Mkuu kutoka Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) Dkt. Hubert Makoye akifundisha mada ya umuhimu wa weledi na taaluma katika filamu kwa washiriki wa warsha walioshiriki mafunzo ya kujengewa uwezo wadau wa sekta ya filamu leo Mkoani Mara.
mara-2
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bibi. Nuru Millao akizungumza na washiriki wa mafunzo ya kujengewa uwezo wadau wa sekta ya filamu (hawapo pichani) wakati wa warsha ya mafunzo hayo leo Mkoani Mara
mara-3
Mshiriki wa warsha ya mafunzo ya kuwajengea uwezo wadau wa sekta ya filamu Bw. Felix Mayoka akichangia wakati wa warsha hiyo leo Mkoani Mara
mara-4
Baadhi ya washiriki wa warsha ya mafunzo ya kujengewa uwezo wadau wa sekta ya filamu na michezo ya kuigiza wakifuatilia kwa makini mada zilizokua zikiendelea wakati wa warsha hiyo leo Mkoani Mara.
mara-5
Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Bibi. Joyce Fissoo akitoa ufafanuzi kwa wanakikundi alipokua akikagua majadiliano yaliyokua yakiendelea katika vikundi wakati wa warsha ya kuwajengea uwezo wadau wa sekta ya filamu leo Mkoani Mara.
mara-6
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bibi. Nuru Millao (mwenye koti la Blue) akichezo ngoma maarufu ya wakurya ijulikanayo kwa jina la litungi wakati wa warsha ya mafunzo ya kuwajengea uwezo wadau wa sekta ya filamu na michezo ya kuigiza leo Mkoani Mara. Kushoto ni Mtendaji Mkuu kutoka Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) Dkt. Hubert Makoye
Picha na: Genofeva Matemu – WHUSM.

Wadau wa sekta ya filamu Mkoani Mara wametakiwa kuzingatia weledi na ubora wakati wa kuandaa filamu.
Na: Genofeva Matemu – WHUSM
Tarehe: 15/12/2016
Wadau wa sekta ya filamu na michezo ya kuigiza Mkoani mara wametakiwa kushirikiana kwa pamoja kuwajibika na kukuza tasnia ya filamu nchini kwa kuzingatia weledi na ubora wakati wa kuandaa filamu kuanzia uandishi wa miswada ya filamu hadi pale filamu inapokamilika.
Hayo yamesemwa na Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Bibi. Joyce Fissoo wakati wa warsha ya mafunzo ya kuwajengea uwezo wadau wa sekta ya filamu na michezo ya kuigiza leo Mkoani Mara.
“Tumekua tukitoa filamu nyingi sana hadi kuifanya Tanzania kuwa nchi ya pili kwa bara la Afrika katika kuzalisha wingi wa filamu lakini filamu hizo hazizingatii weledi hivyo kuzifanya zisiweze kuvuka mipaka ya nchi yetu” amesema Bibi. Fissoo
Akizungumza wakati wa warsha hiyo Mtendaji Mkuu kutoka Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) Dkt. Hubert Makoye amesema kuwa warsha za kuwajengea uwezo wadau wa filamu ni njia mojawapo ya kuimarisha taaluma na kuinua vipaji hivyo ni vyema washiriki wakatumia warsha hizo kuvuka hatua na kuwa na vitu vipya vya kuendeleza tasnia ya filamu nchini.
Naye Rais wa shirikisho la filamu Tanzania Bw. Simon Mwakifwamba amesema kuwa Serikali imeona uhitaji wa kuwajengea uwezo wanatasnia wa filamu hivyo ni vyema mafunzo haya yakachukuliwa kwa mtazamo chanya kwani kumekuwa na changamoto kubwa ya masuala ya weledi kwa wanatasnia wa filamu nchini inayopelekea kuandaa filamu nyingi zisizokuwa na ubora hivyo warsha iliyotolewa na Bodi ya filamu Mkoani Mara imetoa fursa kwa wanatasnia kujengewa uwezo kwenye masuala ya elimu na weledi vitakaowawezesha kuendana na soko la ushindani  la kitaifa na kimataifa.
Aidha Bw. Mwakifwamba ameyataka makampuni mbalimbali nchini kujitokeza kuwekeza kwenye masuala ya filamu nchini kwani filamu ni kiwanda kinachokua kwa  kasi na kutoa ajira kwa vijana wengi nchini.
Kwa upande wake muigizaji kutoka Tanzania Drama and Film Arts Association (TDFAA) Bi. Jaqueline Frank amesema kuwa wadau wa sekta ya filamu na michezo ya kuigiza wa Mkoa wa Mara wamekua wakitumia vipaji vyao kuandaa filamu bila ya kuwa na weledi hivyo mafunzo waliyoyapata yatawasaidia kuboresha kazi zao kwa kuziandaa kwa weledi na ubora wa hali ya juu na kuziwezesha kuvuka mipaka ya Mkoa wa Mara na hata nchi za jirani.

No comments:

Post a Comment