Saturday 31 December 2016

Ngasa kuanza ligi leo, Mbeya City ikiivaa Mbao

Image result for mrisho wa ngasa
Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inatarajiwa kuendelea leo kwa mechi mbili kwenye viwanja tofauti.
Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga wenyeji Mwadui wataikaribisha Kagera Sugar ya Bukoba, wakati Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, wenyeji Mbeya City watawakaribisha Mbao FC.
Mchezo kati ya Mwadui na Kagera unatarajiwa kuwa mkali na wa kusisimua ukikutanisha timu jirani kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa zinazoundwa na wachezaji wanaofahamiana vizuri.
Mjini Mbeya, wenyeji wanatarajiwa kumtumia kwa mara ya kwanza mchezaji wao mpya, Mrisho Ngassa waliyemsajili mwezi huu katika dirisha dogo la usajili kutoka Fanja ya Oman.
Ngassa, kiungo wa zamani wa Azam, Simba na Yanga alishindwa kucheza mechi mbili za awali za Mbeya katika mzunguko wa pili kutokana na kuchelewa kwa Hati yake ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC).

Aidha, Mbeya City pia inatarajiwa kumtumia kwa mara ya kwanza mshambuliaji wake, Zahoro Pazi ambaye pia alikwama kucheza kutokana na kuchelewa kwa ITC yake.

Ligi Kuu itaendelea kesho kwa michezo miwili, Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza Toto Africans wataikaribisha Stand United na Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, African Lyon wataikaribisha JKT Ruvu.

No comments:

Post a Comment