Saturday 31 December 2016

Kombe la Ligi ya Comoro.

como
Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Tanzania bara Yanga ina mataji mawili ya Ligi Kuu Bara na lile la FA kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini wapinzani wao Ngaya Club ya Comoro wikiendi iliyopita walitwaa taji la nne.
Ikicheza dhidi ya Ngazi Club ya Anjuani Jumapili iliyopita kwenye Uwanja wa Hombo uliopo Mutsamudu kisiwani Ngazija, Ngaya ilishinda mabao 2-1 na kutwaa ubingwa wa Kombe la Ligi ya Comoro.
Mataji mengine ambayo Ngaya imetwaa msimu huu ni Ligi Kuu ya Ngazija, Kombe la Ligi Ngazija na Ligi Kuu ya Comoro. Ngaya inafundishwa na Kocha Lucien Sylla Mchangama mwenye Leseni C ya ukocha ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf). 
Ngaya Club inapatikana katika mji mdogo wa Mde Bambao unaopatikana mita 400 kutoka Kusini mwa Mji Mkuu wa Comoro, Moroni. Mechi ya fainali ya Kombe la Ligi ilichezwa kwenye Uwanja wa Hombo uliopo Mutsamudu, Kisiwani Anjuani.
Comoro ni nchi inayoundwa na visiwa vinne ambavyo ni Ngazija, Anjuani, Moheli na Mayotte. Kila kisiwa hucheza ligi yake kisha mabingwa hukutana kucheza ligi ya kupata bingwa wa Comoro katika Ligi Kuu na Kombe la Ligi.
Febuari 11, mwakani Yanga inatarajiwa kucheza na Ngaya Club nchini Comoro mechi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kisha kurudiana Jumamosi ya Februari 18, mwakani jijini Dar es Salaam.
 
Hii ni mara ya tatu kwa Yanga kupangiwa timu ya Comoro, kwani mwaka 2009 ilicheza na Etoile d’or de Mirontsy na kuifunga jumla ya mabao 14-1 (8-1 na 6-0), mwaka 2010 ikaitoa Komorozine kwa mabao 12-2 (7-0 na 5-2).

No comments:

Post a Comment