Wednesday 28 December 2016

Polisi wazingira bunge la seneti Kenya wakati kikao kikiendelea


Maseneta nchini Kenya wamelalamikia kutishiwa na polisi waliozingira majengo ya bunge la seneti.
Aidha, polisi waliweka vizuizi mbalimbali katika barabara ya kuingia bunge.
Bunge la maseneta nchini Kenya
Maseneta hao waliokongamano kwa ajili ya kikao maalum cha kujadili sheria ya uchaguzi, wameeleza kughadhabishwa na hatua ya polisi kuwadhalilisha bungeni.
Wamejitetea kuwa polisi waliojihami walimiminika katika sehemu mbalimbali ya bunge, jambo lisilokuwa la kawaida.
"Tunalaani vikali hatua ya polisi kuzingira bunge la Seneti na yeyote aliyehusika kuwapa mamlaka ya kuzingira bunge siku hii, anastahili kuchukuliwa hatua". Alisema kiongozi wa waliowengi katika Seneti, Kithure Kindiki.
Hata hivyo wabunge hao walitofautiana huku wengine wakiunga mkono kuwepo kwa polisi.
Seneta kutoka mrengo wa serikali, Kipchumba Murkomen, alisifu hatua ya kuwepo kwa polisi hao. 
"Tujilaumu wenyewe kwa mienendo yetu, tunaingia bunge tukibeba visu, pilipili na hata firimbi,". "Wabunge wenzetu wanamtusi rais. Ni aibu".
Kauli yake ilipokea upinzani kutoka Seneta Profesa Anyang' Nyong'o. "Tunamuomba Seneta Murkomen asitufananishe wabunge,".
Seneta Hassan Omar alipendekeza kikao hicho kivunjwe hadi polisi watoke bungeni.
Siku kadhaa zilizopita, bunge la taifa hilo lilishuhudia vurugu baada ya wabunge wa upinzani kujaribu kumzuia spika Justin Muturi kuingia bungeni wakipinga mjadala wa kubadilisha sheria za uchaguzi.

No comments:

Post a Comment