Wednesday 28 December 2016

Bossou kurejea kwao Togo

vincent001-tfff
Beki wa kati wa Yanga, Vincent Bossou leo Jumatano mara baada ya kumalizika kwa mchezo wa timu yake dhidi ya Ndanda, anatarajia kuchukua mabegi yake na kurejea kwao Togo kwa ajili ya kujiunga na kikosi cha timu ya taifa hilo ambacho kinajiwinda kushiriki Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon), ambayo itafanyika nchini Gabon.
Bossou ni mmoja kati ya wachezaji watatu watakaokwenda Gabon na timu zao kushiriki Afcon ambayo inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Januari 14. Wengine kutoka Tanzania ni Juuko Murshid wa Simba na Bruce Kangwa wa Azam.
Bossou ambaye anaunda ukuta imara wa timu hiyo akisaidiana na Kelvin Yondani, amesema kuwa anaenda kuungana na wenzake kwa ajili ya kuweka kambi na timu hiyo ambayo itakuwa Senegal.
“Kesho (leo) baada ya mechi na Ndanda naondoka na kurejea nyumbani kuungana na wenzangu kwenye timu ya taifa kuweka kambi ndogo kwa ajili ya kujiandaa kushiriki Afcon ambapo sisi ni moja ya timu shiriki.
 
“Baada ya kufika huko tunaenda Senegal ambapo ndipo kutakuwa na kambi rasmi na nitakosekana katika Kombe la Mapinduzi kwa sababu nipo huku lakini naamini kila kitu kitakuwa sawa kwani kuna watu wengi wanaoweza kucheza nafasi yangu,” alisema Bossou.

No comments:

Post a Comment