UKABILA NI DHAMBI YA UBINAFSI
NA UBAGUZI LAKINI INAYOLINDWA KWA NGUVU
NYINGI SANA
Siku moja nikiwa shuleni miaka ya mwanzoni mwa themanini
namkumbuka Mwalimu wangu mmoja Ndugu. Nsapaje aliyekuwa akitufundisha
somo la siasa alipomtandika bakora mwenzetu mmoja kwa kumuita mwenzie kwa
kabila lake. Nkana alimuita Mariam “we Mbungu unaitwa!” (wabungu ni moja kati
ya makabila zaidi ya nane yanayopatikana mkoani Mbeya katika Wilaya ya Chunya.
Pasipo kutambua kwamba nyuma yake alikuwa Mwalimu Nsapaje anajongea darasani.
Mwalimu Nsapaje alichukia sana watu kuitana, kuulizana wala kutambulishana kwa
kutumia makabila yao. Alisema hiyo ni dhambi mbaya sana na haipaswi kuvumiliwa.
Alimkamata Nkana na kuingia naye darasani huku akiwa amefura hasira.
Mbele ya darasa akamwita Mariam pia na kumwambia Nkana arudie alichomtamkia
mwenzie. Kwa kutambua kosa alilolifanya Nkana alisita sana kuirejea kauli yake.
Hata hivyo mwalimu hakumuacha mpaka alipotamka kauli ile na kukiri mbele ya
darasa.
Mariam alionekana amenyongea sana, amekosa raha kwa kile alichoambiwa
na Nkana. Alijiuliza maswali mengi sana kwamba pengine hastahili kuwapo
Tanzania, labda ni mkimbizi na mengine chungu mzima. Lakini alifarijika sana
kwa kuwa Mwalimu alisikia moja kwa moja ingawaje pia yalikuwa makusudi yake pia
aende kushtaki kwa Mwalimu wa Nidhamu yaani Mwalimu Nsapaje.
Baada ya Nkana kukiri mbele ya darasa, Mwalimu Nsapaje akaligeukia
darasa zima na kuuliza:-
Mwalimu: ni nini kosa
hapo?,
Wanafunzi: ametenda
dhambi ya Ubinafsi na Ubaguzi
Mwalimu: Adhabu yake nini?
Wanafunzi: Viboko kumi na viwili, kufyatua tofali na barua ya
onyo
Mwalimu: Akirudia tena adhabu gani?
Wanafunzi: Afukuzwe shule
Kwa wakati ule shule yetu ilikuwa na sheria kali sana dhidi ya
waliofanya dhambi ya ubaguzi kwa wenzao, waliogombana ama kutumia lugha chafu
dhidi ya wenzao na kadhalika. Walimu wote, Wazazi na wanafunzi walikuwa wasimamizi wa sheria
zilizowekwa. Tuliogopana kwa wema na hatukuaminiana kwa wema. Mambo yakawa safi.
Nilipoanza kuandaa CV kwa ajili ya kazi na hata sasa naogopa sana
kujitambulisha Kabila na Dini yangu nikiamini kwamba ni ubaguzi na ubinafsi wa
hali ya juu ambao pia haunisaidii chochote katika kupata kazi zaidi ya
kuchangia katika kufanikisha nia ovu ya ubinafsi na ubaguzi wa kiwango cha juu
sana katika ajira hasa pale muajiri anapokuwa hajitambui wala kutambua majukumu
yake sawasawa.
Kuanzia miaka ya mwanzoni mwa 2000 mpaka sasa nimekuwa katika nafasi
ya kusimamia raslimali watu sehemu mbalimbali katika sekta ya hoteli. Moja kati
ya miiko yangu mikubwa ni kutotoa ajira kwa misingi ya ukabila, udini na wala
aina yoyote yenye mlengo ama harufu ya rushwa. Ninashukuru nimefanikiwa katika hilo
kwa kiwango kikubwa. Miongoni mwa watakaoisoma makala hii ni watu niliofanya
nao ajira ama kuhusika katika zoezi lao la usaili na hapana shaka watakuwa
mashahidi wangu wazuri katika hili. Naogopa sana Ukabila na Udini kama
nilivyofundishwa na Mwalimu wangu Nsapaje.
Nikiwa mtu mzima nikaendelea kuuona ukweli wa Mwalimu Nsapaje ambaye
alipendelea kuingia shuleni akiwa na mavazi ya JKT wakati huo na kunifanya
niamini sana kwamba askari yoyote ndiyo kielelezo cha Uzalendo. Ninamkumbuka
Mwalimu wangu sana hasa alipoongelea suala la kutokuwa wabinafsi na wabaguzi, niliiona
kauli yake ikiwa imetoka moyoni haswa na wala haikuwa ya kinywani peke yake.
Wako wapi akina Mwalimu Nsapaje wengine leo?, waliishia wapi?, hawakuacha
urithi?. Najiuliza maswali haya lakini nakosa majibu sahihi.
Leo ninapoandika walaka huu ninaiona dhamira y dhati ya Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere, Baba wa Taifa la Tanzania kuamua kutuunganisha kwa lugha
moja tu yaani KISWAHILI. Najaribu kuitafakari Tanzania ya leo hii bila kuwapo
na lugha inayotuunganisha. Kila mtu katika makabila yetu zaidi ya mia moja na
ishirini angekuwa anatumia lugha yake katika mawasiliano sijui nini kingetokea.
Moja ya hotuba muhimu sana kwa Taifa la Tanzania zilizowahi kutolewa
na Baba wa Taifa ni ile aliyoitoa katika Mkutano Mkuu wa Chama cha Mapinduzi
1995 wakati wa mchakato wa kumpata mgombea urais wa serikali ya awamu ya tatu.
Mwalimu alitaja mambo manne kuwa yanahitaji rais atakayekuwa tayasimamia kwa
dhati ya moyo wake. Rushwa, Umaskini, Udini na Ukabila mwalimu aliona vimeanza
kuota mizizi hapa nchini wakati huo lakini kwa sasa sio tu vina mizizi bali
vimeanza kuzaa matunda. Kwa faida ya wasomaji wangu nitainukuu hotuba yote.
HOTUBA
YA MWALIMU JULIUS KAMBARAGE NYERERE ALIYOITOA KATIKA MKUTANO MKUU WA CCM MWAKA
1995 MJINI DODOMA
“Rais amewaambieni na mimi nasisitiza,
nitamalizia hapo sitaki kuchukueni muda
wenu mrefu. Teueni mgombea ambaye atakidhi matarajio ya Wananchi, acha
matarajio yako wewe mpiga kura. Tupeni mgombea ambaye atakidhi matarajio ya
Watanzania.
Watanzania wanataka mabadiliko,
wasipoyaona, wasipoyapata ndani ya CCM watayatafuta nje ya CCM. Watanzania kuna
mambo wanataka uongozi wa awamu ya tatu uyafanye, mengi tu mimi nitataja
machache. Mengi tu lakini nitataja machache, yatawatosheni.
La kwanza, nitataja manne, la kwanza;
Watanzania wamechoka na Rushwa. Wajumbe wa zamani wa Halmashauri kuu ya Taifa
watakumbuka nimelipigia kelele suala la Rushwa ningali Mwenyekiti wao hapahapa
Dodoma. Nilipiga kelele kiasi kwamba Waziri Mkuu wa wakati huo alikwenda kwa
Rais, alikuja kwako Ndugu Rais kuja kutoa hati yake ya kujiuzulu. Sasa hivi
hali ya Rushwa ni mbaya zaidi nchini, wasaidieni wananchi ku-deal nayo. Mgombea
mtakayemteua lazima tumtetee, wote tumtetee. Lakini inatakiwa ukiulizwa swali,
huyu atatusaidia kupiga rushwa vita?, jibu litoke ndani ya roho yako hapana
hapa tu (mdomoni) kwamba ndiyo anaweza. La kwanza.
La pili; nchi yetu masikini, nchi yetu hii
masikini. Wakulima wetu, wafanyakazi wetu masikini. Nchi hii bado ni nchi ya
wakulima na wafanyakazi ambao wote ni watu masikini. Nchi hii haijawa ya
matajiri, Chama hiki hakijawa chama cha matajiri!. Tunataka tuendelee
kushughulika na umasikini wa watu wetu,tushughulike kwa dhati na matatizo ya
wananchi ya uchumi wao, Hali yao ya uchumi, hali yao ya viwandani, hali yao ya
mashambani, hali yao ya shuleni, hali yao ya hospitalini. Tunataka kuwa na
hakika kwamba mtatuteulia mtu ambaye ukiulizwa swali huyu anajua?, kwamba nchi
hii ni nchi bado ni nchi ya masikini?, kwamba nchi hii bado ni nchi ya wakulima
na wafanyakazi, anajua hivyo?. Uweze kumjibu Yule anayekuuliza hivyo kwa moyo
wa dhati kwamba Naam!, huyu anatambua hivyo.
Sasa hivi katika nchi yetu, la tatu,
nataja la tatu, watu wameanza kutuzungumzia udini, tulikuwa hatuzungumzi mambo
ya udini udini katika nchi hii, hata kidogo. Tulikuwa hatujali dini ya mtu,
anaijua mwenyewe dini yake, basi. Ilikuwa haiji katika akili yetu kwamba
tunapompima mtu tumchague huyu tumfanye rais au tumfanye nani tunauliza dini
yake, hatuulizi hata kidogo, tulikuwa hatuulizi hata kidogo. Dini inatuhusu
nini sisi?. Zamani katika kuhesabu watu hapa Tanzania, katika kuhesabu watu
wakati wa mkoloni, siku ya sensa swali lilikuwa linauliza dini ya mtu. Tukasema
sisi hatujengi misikiti, hatujengi makanisa, hatujengi mahekalu hili swali la
udini ya mtu tunaliuliza kwa nini?. Linatuhusu nini?, tunataka kujua umri wa
watu, kwa sababu hiyo ina maana, tunataka kujua kama watu wanajua kusoma na
kuandika hiyo ina maana, tunataka kuuliza mambo ambayo serikali inayataka. Kama
maimamu wanataka kuuliza, wanataka kujua wana Waislamu wangapi watafute wao
sisi inatuhusu nini?, kama maaskofu wanataka kujua wana Wakristo wangapi
watafute wao si wanakuja makanisani kuungama?, wawaulize!. Sisi inatuhusu nini
jambo la dini hata tuulize watu wewe dini yako nani, inatuhusu nini sisi?. Hiyo
ndiyo ilikuwa Tanzania tunayojaribu kuijenga.Sasa watu wanazungumza dini, udini
bila haya, bila aibu. Wanajitapa kwa udini!. Tunataka mtuchagulie mgombea
ambaye atatusaidia kuondoa mawazo haya ya Kipumbavu katika nchi yetu. Na
ukiulizwa na wananchi wa Tanzania kwa dhati, mnadhani mgombea huyu analiona
hilo kwa uchungu kama mnavyoona nyinyi mseme ndiyo, uweze kujibu kwa dhati
kabisa kwamba Ndiyo.
La mwisho, nilisema nitataja manne tu.
Nilikuwa New York mwaka jana, yupo mwenzenu mmoja Getrude Mongela, sasa hivi ni
Katibu wa akina mama wa Mkutano wa akina mama utakaofanyika Beijing. Gaetrude
alinikaribisha chakula jioni katika flat yake hapo New York, akakaribisha jamaa
wengine nikaonana nao pale. Wakati tunakula, mama mmoja wa Kiganda ambaye anafanya
kazi hapo kanambia Mzee mimi nilikuwa nafanyakazi katika jumuiya ya Afrika ya
Mashariki. Wakati nafanya kazi katika jumuiya ya Afrika ya Mashariki, sisi watu
wa Uganda tulikuwa tunajuana kwa makabila yetu, na tunatajana kwa makabila
yetu. Watu wa Kenya walikuwa wanajuana kwa makabila yao, huyu Mkikuyu, huyu
Mjaluo, huyu Muruya na wanatajana kwa makabila yao. Watu wa Tanzania walikuwa
kabisa kabisa hatujui makabila yao. Nilimwambia Yule mama ni wakati huo mama!,
nilimwambia ni wakati huo sio sasa. Sasa Watanzania wanaanza kuulizana
makabila, wanafikiri ni jambo la maana sana kujua kabila la mtu, mnataka
Kutambika?. Maana faida ya makabila iliyobaki ni kutambika tu, basi!, lakini
hasa ina maana gani nyingine?. Katika nchi ya watu wazima, kabila lina maana
gani nyingine?. Tukifanya mitambiko pale Butiama pale tunafanya, mimi nipo
karibu pale na chaka letu ambapo ndipo
mungu wa Watiama wale anakaa. Lakini kabila hasa, Tanzania ya leo
inazungumza Kabila!!. Wazungu wale waliotutawala wana Mataifa makubwa makubwa,
yametawala dunia. Leo wanaviona vitaifa vyao vile ni vidogo mno wanaungana.
Waingereza na jeuri yao yote wametawala dunia, Wafaransa na jeuri yao yote
wametawala dunia, Wajerumani na jeuri
yao yote wameipiga Ulaya. Leo wanaungana kuwa Taifa moja. Nyinyi Waswahili,
vinchi vidogovidogo hivi, vya watu ishirini na saba milioni mnazungumza
makabila!!, mnazungumza lugha ya makabila!!, mtuingize katika karne ya ishirini
na moja mnapanda basi la makabila!!. Lakini tumeanza kuzungumza ukabila.
Tunataka mtuchagulie mtu ambaye anajua kwamba huko ni Upumbavu na ni hatari
huko.Hatuwezi, lugha ya ukabila hatuwezi kuzungumza. Wenzetu wanatushangaa,
wenzetu majirani sisi ndiyo ilikuwa mfano wao mbona Tanzania hawazungumzi
ukabila sisi tunazungumza ukabila, mfano wao ulikuwa ni Tanzania. Tunataka
kuwaiga majirani zetu katika hilo?. Tunataka kusema Kenya wanazungumza makabila
na sisi tusizungumze ukabila kwa nini?, Tunasema Uganda wanazungumza makabila
na sisi tusizungumze ukabila vilevile kwa nini?, Tunasema Rwanda na Burundi
wanazungumza makabila na sisi tuzungumze ukabila, tunasema hivyo
Watanzania??!!, bila haya?. Kabila si jambo la kuonea haya, kabila linakuwa ni
jambo leo unaweza kusema katika basi unajitapa ukabila!!?. Tunataka mtuteulie
kiongozi anayejua hiyo, atusaidie.
Ndugu Wananchi, Ndugu Mwenyekiti, Mimi
mliniomba nije kusaidia, nilikubali kuja kusaidia, kwa nini? Kwa sababu
hiyohiyo. Tunataka nchi yetu ipate Kiongozi safi, Kiongozi safi hawezi kutoka
nje ya CCM.
Nyinyi wapiga kura mnaweza kutupatia
kiongozi safi kwa kura zenu, basi tupatieni kiongozi safi kwa kura zenu.
Ahsanteni sana!”.
Pamoja na mengi ambayo Mwalimu Nyerere aliyasema kwa kuonya enzi za
uhai wake tukayapuuza leo hii tunaona madhara yake katika jamii zetu. Hata
hivyokatika waraka huu tutatazama zaidi suala la “UKABILA” jambo ambalo
aliliongelea kwa uchungu sana.
VIASHIRIA VYA UKABILA
Katika nchi yetu kwa sasa tunavyoviashiria vingi sana vya ukabila
lakini ninashawishika kuyaona mambo mawili katika uwepo wake na kuenea kwake
katika jamii kwa sasa.
a)
Wengine wanafanya kwa kuiga na huku wakidhani
ndiyo uzalendo kwa makabila yao
b)
Wengine wanafanya huku wakijua fika
kitakachovunwa hapo baadaye lakini wanaongozwa na Ubinafsi na Unafiki.
Kufanya Kwa
kuiga:
Yapo mengi sana tuliyoyaiga kwa kudhani ndiyo kwenda na wakati pasipo
kuchukua muda wa kutafakari kwa kina kujua upande hasi na upande chanya wa kile
tunachoiga. Hali hii mara nyingi imepelekea kumomonyoka kwa maadili na
kusababisha matatizo makubwa katika jamii zetu. Mbaya kuliko yote ni pale tunapoiga
mabaya mengi kuliko mazuri ambayo siku moja tungeweza kusimama hadharani na
kujivunia.
Vyama vya kikabila vya kufa na kuzikana vimeendelea kutamalaki sana
nchi kwetu na hasa kwa takribani miongo hii mitatu. Mlango huu wa ukabila
unainuka kwa kasi ya ajabu kwa tiketi ya kusaidiana wakati wa misiba. Swali la
msingi hapa ni kwamba kwa nini tunataka kusaidiana wakati wa kutoka kwa uhai wa
mtu?. Jibu rahisi ni Ubinafsi na Unafiki.
Pamekuwepo na mtindo wa watu kujipatia umaarufu kupitia shughuli kubwa
kubwa na hasa zinazogusa jamii kwa ukaribu sana kama misiba. Gharama kubwa sana
watu wamekuwa wakizitumia katika mazishi ya wapendwa wao kuliko zile ambazo
zingepaswa kutumika kwa mfano katika kumuuguza mgonjwa kabla ya kufa kwake.
Utafiti unaonyesha kwamba watu hutoa michango mikubwa mikubwa katika misiba
kuliko katika ugonjwa wa mtu. Unamsaidiaje mtu na inakusaidia nini wewe
unayetoa kwa sifa msibani lakini hukujali wakati pakihitajika gharama za matibabu.
Ili kudhirisha kwamba vyama vya ukabila katika suala la msiba havina maana
yoyote bado tumeendelea kuona ushiriki wa jumla wa wale wasiokuwa wa kabila
hilo kuliko hata kwa wenye kabila. Pia pameendelea kuwapo manung`uniko katika
sehemu nyingine kwamba vyama hivyo hivyo vya ukabila vimekuwa na ubaguzi wa
hali ya juu baina ya walionacho na wasionacho.
Watu wengi sana wamekuwa wakiiga mitindo hii ya vyama vya kikabila
hata pasipo kufanya uchunguzi wa kina kubaini faida na hasara zake. Kwa tafsiri
ndogo tuliyonayo tunadhani tunafanya kama mtindo madhubuti wa kujiimarisha
katika kabila letu. Lakini tujiulize, yote haya na kwa faida ya nani?. Kabila
lako liisha kuimarika lishindane na nani katika nini?.
” Nilimwambia Yule mama Ni wakati huo
mama!, nilimwambia ni wakati huo sio sasa. Sasa Watanzania wanaanza kuulizana
makabila, wanafikiri ni jambo la maana sana kujua kabila la mtu, mnataka
Kutambika?. Maana faida ya makabila iliyobaki ni kutambika tu, basi!, lakini
hasa ina maana gani nyingine?. Katika nchi ya watu wazima, kabila lina maana
gani nyingine?”.
Ingelikuwa jambo la maana sana kama Watanzania wangeamua kuanzisha
mshikamano wa kimitaa ambao baadaye unatengeneza nguvu kubwa ya Taifa. Hebu
tujiulize haya yafuatayo kasha tuweke kwenye mzani tuuone uzito uko wapi kati
ya mshikamano wa Kitaifa na mshikamano wa kikabila.
Mosi; a). Ni nani kati yetu
ambaye mtaani kwake pamekosekana maendeleo kwa sababu anaoishi nao sio wa kabila lake?.
b). Ingelikuwaje
kama wakazi wa mtaa Fulani wamkaamua kuweka makabila yao kando na badala yake waijenge jamii ya mtaa wao
kimaendeleo?
Pili; a). Ni nani ambaye akipatwa na tatizo
wanahusika watu wa kabila lake pekee kwa sababu ya chama cha kabila lake?
c)
Kama wakazi wote wanaweka kando makabila yao
wakati mwenzao akiwa na tatizo, ni wapi unaonekana umuhimu wa kuwa na chama cha
kikabila.
Ukabila hauna zaidi ya ubinafsi, ubaguzi na unafiki uliotukuka ambao
katu hauwezi kutetewa kwamba umewahi kuwa na tija ama manufaa yoyote zaidi ya
kila mtu kujipambanua kwamba wanalo kabila. Makabila yametutafuna hata katika
taasisi zetu za kidini. Watu wamepigana na kushutumiana kwa misingi ya ukabila
pasipo hata kuangalia kwamba dhehebu husika halihitaji uwepo wa kabila kwa kuwa
linahudumia watu wa makabila na rangi zote.
Dhambi ya ukabila ni kubwa sana kwani hata mifumo yetu ya kiutawala
katika nchi imeingiliwa na ubinafsi, ubaguzi na unafiki na hivyo kufanya ukabia
utamalaki. Vigezo vya msingi katika ajira vimewekwa kando na sasa watu
wanaajiriwa kwa makabila yao. Taifa linaangamia, hakuna uzalendo tena, hakuna
uwajibikaji tena, hakuna tija katika uzalishaji, hakuna uadilifu maofisini,
viwandani na mashambani. Migogoro ya wakulima na wafanyakazi ni ukabila tu,
ujinga unaoendelea kwenye siasa zetu ni ukabila tu, kukosekana kwa maamuzi
sahihi ni ukabila tu, kudorola kwa maendeleo ya kiuchumi ni ukabila tu.
Tamaa ikichukua mimba huzaa dhambi, dhambi ikiisha kukomaa huzaa
mauti. Watu wanayatamani makabila yao zaidi kuliko Taifa lao na sasa tama zao
zikazaa dhambi ya ubaguzi, ubinafsi na unafiki. Dhambi hiyo imeendelea kukomaa
na mpaka sasa zipo dalili za kutosha kabisa kwamba dhambi hizo zimekomaa kiasi
cha kuelekea kuzaa mauti.
Soma zilizopita
No comments:
Post a Comment