Thursday 29 December 2016

Taarifa ya Jeshi la Polisi Mkoani Mbeya

unnamedm
 Jeshi la Polisi mkoa wa Mbeya limeendelea kufanya misako, operesheni na doria zenye tija katika maeneo mbalimbali ili kudhibiti uhalifu na wahalifu na limekuwa likishirikiana na wananchi na wadau wengine katika jitihada hizo za kukabiliana na uhalifu na wahalifu na kupata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kupungua kwa matukio makubwa ya uhalifu. Katika kuelekea sikukuu za mwisho wa Mwaka, Krismas na mwaka mpya 2017 Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limejipanga vizuri kwa kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo yote. Katika kuhakikisha wakazi wa Mkoa wa Mbeya wanasherehekea kwa amani na utulivu sikukuu ya mwaka mpya, tumeandaa mpango mkakati kama ifuatavyo:-
MPANGO MKAKATI WA JESHI LA POLISI MKOA WA MBEYA KUELEKEA SIKUKUU YA NA MWAKA MPYA:
  1. Ulinzi na usalama katika nyumba za ibada
Kwa makanisa ambayo yatakuwa na ibada za mkesha kwa siku ya tarehe 31.12.2016 kutakuwa na askari ambao wataimarisha ulinzi na usalama kwa kusaidiana na kamati ya ulinzi na usalama ya kanisa/msikiti husika. Kuhakikisha ulinzi ndani na nje ya kanisa/msikiti unakuwepo, ulinzi katika maeneo ya maegesho ya magari.
  1. Kumbi za starehe
Jeshi la Polisi linawataka wamiliki wa kumbi za starehe kufuata na kuzingatia taratibu za uendeshaji biashara zao hasa kwa kuzingatia muda wa kufungua na kufunga kumbi zao kulingana na vibali vya biashara zao, kuzingatia idadi ya watu wanaopaswa kuingia ukumbini kulingana na ukubwa wa ukumbi ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza. Pia tunawataka kuweka walinzi wa ndani ya ukumbi na nje hasa maeneo ya maegesho ya magari ili kudhibiti uhalifu na wahalifu.
  1. Waendesha vyombo vya moto na watumiaji wengine wa barabara.
Kutokana na kuwepo ongezeko la vyombo vya moto katika Mkoa wa Mbeya magari, pikipiki na bajaji kila mtumiaji wa vyombo hivi anatakiwa kuzingatia utimilifu wa afya yake, usalama wa chombo chake pamoja na kuheshimu, kufuata na kuzingatia sheria na alama za usalama barabarani. Aidha watembea kwa miguu kuhakikisha wanakuwa waangalifu wakati wa kuvuka barabara ili kuepuka ajali. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limejipanga vizuri kuhakikisha usalama kwa watumiaji wa vyombo vya moto na watumiaji wengine wa barabara unakuwepo, pia kwa wageni wanaoingia na kupita kuelekea nchi jirani na mikoa jirani wanapita bila usumbufu wowote.
  1. Uangalizi wa watoto katika kipindi chote cha sikukuu.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawataka wazazi na walezi kuhakikisha kila mmoja anakuwa makini na mtoto wake kwa kutoa uangalizi katika kipindi chote cha sikukuu ya mwaka mpya. Kuhakikisha watoto wanakuwa na waangalizi pindi wanapotoka kwenda maeneo ya mbali kama vile sehemu za kuabudu makanisani na misikitini, sehemu za michezo ya watoto ili kuepuka matukio ya kupotea kwa watoto na hata kuepuka vitendo vya uhalifu dhidi ya watoto. Aidha ni wito wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kila mzazi, mlezi na jamii kwa ujumla kuwa makini na kutoa taarifa kwa vyombo vya dola pindi wanapoona mtoto/watoto waliopotea.
  1. Ulinzi na usalama katika nyumba za kuishi/makazi yetu
Pia ulinzi na usalama ni muhimu katika makazi yetu, vikundi vya ulinzi shirikishi vilivyopo katika mitaa vina kazi ya kufanya katika kipindi hiki kutokana na ongezeko la watu. Aidha Jeshi la Polisi litakuwa pamoja na vikundi hivi kufanya doria ya pamoja katika maeneo tete na makazi. Pia ni rai yangu kwa kila mmoja kuhakikisha anapotoka anaacha mtu/muangalizi ili kuepuka vitendo vya uvamizi, uvunjaji.
WITO WA KAMANDA.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Naibu Kamishna wa Polisi DHAHIRI A. KIDAVASHARI anatoa wito kwa wakazi wa Mkoa wa Mbeya kwa ujumla kuwa watulivu, kusherehekea kwa utulivu na amani sikukuu ya mwaka mpya 2017. Aidha anatoa wito kwa wananchi kuacha kuzurura ovyo na pia kushirikiana na vikundi vya ulinzi shirikishi pamoja na kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu katika maeneo yao.
Imesainiwa na:
[DHAHIRI A. KIDAVASHARI – DCP]
KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA.

No comments:

Post a Comment