Saturday 24 December 2016

Simba kumenyana na JKT Ruvu Stars kwenye uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam leo

wo
Na.Alex Mathias.
Baada ya African Lyon kuibeba Simba wekundu wa Msimbazi hao watashuka dimbani kucheza na timu ya JKT Ruvu Stars kwenye uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam.
Simba bado wanaongoza Ligi wakiwa na pointi 38 huku watani zao Yanga baada ya kukabwa koo na Lyon bado wanashika nafasi ya pili wakiwa na pointi 37 na kama Simba atashinda mchezo huo atakuwa ameongeza gape la pointi nne na kuendelea kukalia usukani.
Hata hivyo Simba itawakosa washambuliaji wake hatari Ibrahimu Ajibu aliyekwenda nchini Misri kufanya majaribio ya kucheza soka la kimataifa pamoja na Frederick Blagnon ambaye anasumbuliwa na majeraha aliyoyapata kwenye mchezo dhidi ya Ndanda FC ambapo waliibuka na ushindi wa magoli 2-0.
Kwa Upande wa matajiri wa jiji la Dar es salaam,Azam FC ipo nafasi ya tatu na ina tofauti ya pointi 12 na vinara Simba katika Ligi Kuu Bara, sasa imejigamba leo ni lazima iwafunge Majimaji ugenini ili kupunguza utofauti wa pointi hizo.
Azam ina pointi 26 katika mechi 16 ilizocheza ambapo kati ya hizo, imeshinda mechi saba, imefungwa mara nne na imetoka sare mara tano, imefunga mabao 21 na imefungwa mabao 14.
Mchezo wa Azam na Majimaji unachezwa kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea mkoani Ruvuma na Ofisa Habari wa Azam, Jaffar Idd amesema: “Lazima tushinde.”
 
Timu hizo zinakutana katika Uwanja wa Majimaji leo ambapo Azam ina historia ya kutofungwa katika uwanja huo na wapinzani wao hao.
Akizungumza, Idd alisema wamejiandaa vizuri kwa ajili ya mchezo huo na ametamba wataendeleza ushindi wao kwa wapinzani wao hao ili wachukue pointi tatu muhimu.
“Kocha ameyafanyia marekebisho makosa yaliyojitokeza katika mechi yetu na African Lyon na tuna imani tutafanya vizuri katika mchezo wetu wa kesho (leo) ili kuweza kuendeleza rekodi yetu kwani hatujafungwa na Majimaji katika uwanja wao.
“Kikosi kipo vizuri na wachezaji wamejiandaa vizuri kuelekea mchezo huo isipokuwa tutawakosa wachezaji watatu ambao ni Daniel Amoah, Mudathir Yahaya na Gadiel Michael ambao ni majeruhi,” alisema Idd.
Kwa upande wake Kocha wa Majimaji, Kali Ongalla, alisema: “Mechi hii ni ngumu, wenzetu wana wachezaji wengi wa kigeni, ila tutapambana ili tushinde.”
Michezo mengine:Mbeya City vs Toto African,Kagera Sugar vs Stand United,Mwadui FC vs Mbao FC,Ndanda FC vs Mtibwa Sugar na Ruvu Shooting vs Tanzania Prisons.

No comments:

Post a Comment