Ile ishu iliyomkuta mwamuzi, Martin Saanya kwa kuchezesha mchezo wa
Oktoba Mosi kati ya Simba na Yanga, umezua mapya, baada ya mechi ijayo
itakayopigwa Februari 18, mwakani kuachwa pengo katika ratiba ya waamuzi
kwa duru ya pili.
Ratiba hiyo ilipangwa tangu Desemba 5, mwaka huu na Chama cha Waamuzi
Tanzania (Frat), kabla ya Jumapili iliyopita kupitishwa rasmi na Kamati
ya Waamuzi, lakini mechi ya Simba na Yanga ikawekewa nyota kwa kile
kilichosemekana ni kutokana na mechi zao kugubikwa na utata mkubwa,
hivyo mwamuzi atatajwa baadaye.
Mmoja wa mabosi mhusika katika upangaji wa ratiba hiyo ya waamuzi,
amethibitisha na kutaja sababu kuu tatu ambazo zimewafanya waiweke
chemba kwanza.
“Kwanza ni presha, maana mara nyingi mechi zao huwapa presha kubwa
waamuzi, hasa wakijulikana mapema, pili tunataka tuwe makini zaidi
katika kumpangia mwamuzi mechi hii kutokana na malalamiko mengi ambayo
hutokea baada ya mchezo, hatutaki yaliyojitokeza Oktoba Mosi yajirudie.
“Pia tunataka kuanza tujiridhishe katika maamuzi ya mechi hizi nyingine,
tuone yupi anayeweza kusimama katikati siku hiyo, ndiyo maana ikawekewa
nyota,” alisema bosi huyo aliyeomba hifadhi ya jina na kusisitiza hata
kamisaa wa mchezo huo hajapangwa.
Akina Saanya wamefungiwa miaka miwili kwa kosa la kuvurunda kwenye
mchezo huo kwa kukataa bao halali la Ibrahim Ajibu wa Simba na kukubali
bao la mkono la Amissi Tambwe pamoja na kadi nyekundu aliyopewa Jonas
Mkude wa Simba iliyokuja kufutwa kwani haikuwa halali.
No comments:
Post a Comment