S.NKINGA: MPANGO KAZI WA TAIFA WA KUTOKOMEZA UKATILI DHIDI YA WANAWAKE NA WATOTO KUZINDULIWA TAREHE 13/12/2016
Na erasto ching’oro– Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano, Wizara ya Afya, Maendeleo ya jmaii, jinsia, wazee, na Watoto
Tarehe 13, Desemba 2106 Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan,
atazindua Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake
na Watoto, shughuli itakayofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Julius
Nyerere, Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wazee na Watoto Sihaba Nkinga, ambaye Wizara
yake ndio inyoratibu Uzinduzi huu anabainisha kuwa, Mpango Kazi wa
Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto unalenga kushirikisha
Serikali na wadau wengine katika jitihada jumuishi za kuzuia ukatili
dhidi ya wanawake na watoto na hivyo kusaidia wahanga wa ukatili kupata
huduma stahiki ili kudhibiti ukatili nchini.
Kumekuwepo na matukio mengi ya
ukatili yanayosababishwa na mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na umaskini
katika familia, mila na desturi potofu zenye athari katika jamii,
malezi na makuzi mabovu na sheria kandamizi. Katibu Mkuu S. Nkinga
anatanabaisha kwamba, kabla ya kuandaliwa kwa Mpango Kazi huu, Tanzania
ilikuwa na mipango kazi minane (8) ya kuzuia ukatili dhidi ya wanawake
na watoto. Mipango hiyo ilikosa uratibu wa pamoja na hivyo kushindwa
kuleta matokeo makubwa katika kutokomeza ukatili.
Aidha, ameongza kuwa mipango hiyo
haikuwa na mfumo wa pamoja wa kufuatilia na kutathmini ufanisi
unaopatikana. Vilevile, kutokana na madhara ya ukatili dhidi ya wanawake
na watoto katika maendeleo ya nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, wakuu
wa nchi wanachama waliazimia kwa pamoja kutokomeza ukatili huo kupitia
utekelezaji wa lengo Na. 5 na 6 ya Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo
2030.
Itakumbukwa kuwa, Tanzania ni kati
ya nchi nne (4) za kwanza duniani na nchi pekee katika Afrika
iliyowezeshwa kupitia jukumu lilioanzishwa la kusaidia nchi wanachama wa
Umoja wa Mataifa kuandaa mpango wa kuzuia na kuitikia afua za kudhibiti
ukatili ili kuwa na mipango thabiti ya upatikanaji wa haki, usawa na
maendeleo kwa wote.
Akieleza katika kikao na
waandishi wa Habari mapema wiki hii, Katibu Mkuu Nkinga aliseama kuwa
Mpango kazi huo wa aina yake una maeneo makuu manane (8)
yatakayotekelezwa na wadau wa maendeleo ya wanawake na watoto. Meneo
hayo ni Uimarisha wa uchumi wa kaya; Uzuiaji wa mila na desturi zenye
madhara; na Uboreshaji wa mazingira salama katika jamii.
Maeneo mengine ni Kuendeleza
mazingira salama ya mafunzo shuleni na stadi za maisha na kuhuisha
mahusiano, malezi na makuzi katika familia; Utekelezaji na usimamizi wa
sheria; Utoaji huduma kwa wahanga na mwisho, ni sehemu ya Uratibu,
ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa mpango kazi wa miaka mitano
kuanzia mwaka 2017/2018 hadi 20121/21022.
Mpango Kazi huu mahususi
unatarajiwa kuwa na matokeo makubwa baada ya miaka mitano ya utekelezaji
kwani utawezesha kuondoa ukatili dhidi ya wanawake kwa asilimia 50
kufikia mwaka 2021/2022; na Kuondoa ukatili dhidi ya watoto kwa asilimia
50 kufikia mwaka 2021/2022, na hivyo kuleta mabadiliko makubwa kwa
kuwa na familia salama, na jamii yenye utulivu.
Mwisho, Katibu Mkuu Nkinga,
anaeleza kuwa, Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya
Wanawake na Watoto nchini Tanzania utakuwa ndiyo dira kwa wadau wote wa
masuala ya maendeleo ya wanawake na watoto hapa nchini. Mpango
unabainisha kazi zitakazotekelezwa na kila mdau kuanzia familia, jamii,
halmashauri, mikoa, wizara za sekta, sekta binafsi, asasi za Kiraia na
wabia wa maendeleo. Mpango umeweka mfumo fungamanishi wa uratibu,
ufuatiliaji na tathmini. Aidha, mpango utaratibiwa katika ngazi ya Taifa
na Ofisi ya Waziri Mkuu, ngazi ya mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa, na
ngazi ya halmashauri na Wakurugenzi Watendaji.
Mwisho, Wizara inawahimiza
washiriki wote waliopata mwaliko kuhakiksha kuwa wanafika mapema katika
mkutano huu muhimu. Vile vile, Wizara inatoa rai kwa vyombo vya Habari
kutoa ushirikiano katika kutangaza tukio hili la uzinduzi wa Mpango Kazi
wa Kutokomeza Ukatili, na pia kuwaelimisha wananchi waweze kuuelewa
mpango huu ili kuongeza uelewa wa wadau na jamii na kuwa tayari kuzuia
ukatili wa kijinsia na kutoa huduma kwa wahanga.
No comments:
Post a Comment