Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi
na Umeme – TEMESA Dkt. Mussa Mgwatu (aliyesimama) akifungua mafunzo
elekezi kwa watumishi wa karakana za TEMESA juu ya mfumo wa utozaji
gharama katika karakana za TEMESA pamoja na mfumo wa utoaji taarifa za
kila mwezi, yanayofanyika katika ukumbi wa Karakana ya MT. Depot Dar es
Salaam. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Uendeshaji Bw. Hans
Lyimo na kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Uzalishaji na Matengenezo Mhandisi
Sylivester Simfukwe.
Watumishi kutoka Karakana za
Wakala wa Ufundi na Umeme – TEMESA wakimsikiliza Mtendaji Mkuu Dkt.
Mussa Mgwatu (hayupo pichani) katika ufunguzi wa mafunzo elekezi juu ya
mfumo wa utozaji gharama katika karakana za TEMESA pamoja na mfumo wa
utoaji taarifa za kila mwezi, yanayofanyika katika ukumbi wa Karakana ya
MT. Depot Dar es Salaam.
Watumishi kutoka Karakana za
Wakala wa Ufundi na Umeme – TEMESA wakimsikiliza Mhandisi Sylivester
Simfukwe (aliyesimama) katika mafunzo elekezi juu ya mfumo wa utozaji
gharama katika karakana za TEMESA pamoja na mfumo wa utoaji taarifa za
kila mwezi, yanayofanyika katika ukumbi wa Karakana ya MT. Depot Dar es
Salaam.
Wawakilishi kutoka Karakana ya
TEMESA Pwani wakifuatilia kwa makini mada mbali mbali katika mafunzo
elekezi juu ya mfumo wa utozaji gharama katika karakana za TEMESA pamoja
na mfumo wa utoaji taarifa za kila mwezi, yanayofanyika katika ukumbi
wa Karakana ya MT. Depot Dar es Salaam.
Picha zote na TEMESA.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi
na Umeme – TEMESA Dkt. Mussa Mgwatu leo amefungua mafunzo elekezi kwa
watumishi wa karakana juu ya mfumo wa utozaji gharama za matengenezo ya
magari katika karakana za TEMESA pamoja na mfumo wa utoaji taarifa za
uzalishaji na matengenezo za kila mwezi.
Dkt. Mgwatu amesema kuwa mafunzo
hayo yamelenga kuleta uwiano sawa katika gharama za matengenezo ya
magari kwa karakana zote za TEMESA bila kujali mikoa zilipo karakana
hizo. Aliongeza kuwa utaratibu utakaoelekezwa katika mafunzo hayo
utasaidia kupunguza gharama za matengenezo ya magari ya serikali, suala
linalolalamikiwa na wateja wa TEMESA kwa muda mrefu sasa.
“Nataka sasa tuanze kutoza gharama
za matengenezo ya magari kulingana na muda unaotumika kutengeneza gari
husika (man hour), badala ya kutumia kigezo cha asilimia ya fedha
iliyotumika kununulia vipuri kwa ajili ya matengenezo ya magari, kwani
baadhi ya vipuri ni ghali sana lakini hutumia muda mchache sana
kuvifunga,” alisema Dkt. Mgwatu.
Dkt. Mgwatu aliongeza kuwa,
kumekuwa na changamoto ya uwasilishaji wa taarifa za utendaji kutoka
katika mikoa/vituo vya TEMESA, mara nyingi taarifa hizi hazifiki kwa
wakati. Huku akisisitiza kuwa ni matumaini yake baada ya mafunzo hayo
taarifa hizo zitakuwa zikifika kwa wakati tena zikiwa sahihi.
Katika hatua nyingine, Kaimu
Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji na Matengenezo, Mhandisi Sylivester
Simfukwe alisema idara yake imejipanga kutoa huduma bora zinazokidhi
viwango hasa katika matengenezo ya magari ya serikali, ili kuhakikisha
kuwa uzalishaji unaongezeka na kero za wateja zinakwisha. Aliongeza kuwa
mafunzo kama hayo yatatolewa kwa wawakilishi wa karakana zote za TEMESA
nchi nzima.
Mafunzo hayo elekezi juu ya Mfumo
wa utozaji gharama katika karakana za TEMESA pamoja na mfumo wa utoaji
taarifa za kila mwezi, yanafanyika kwa siku 5 katika ukumbi wa MT.
Depot, Dar es salaam na yamehusisha watendaji wa TEMESA kutoka mikoa ya
Tanga, Morogoro, Pwani, Dar es Salaam, Lindi na Mtwara, pamoja na vituo
vya MT. Depot na Kikosi cha Umeme.
Imetolewa na Kitengo cha habari na Mawasiliano
TEMESA
No comments:
Post a Comment