Baada ya kutekeleza ahadi ya
mwanzo ya kuipeleka Madagascar kwa ajili ya kambi ya kuivaa Afrika
Kusini ‘Amajimbos’, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF),
Jamal Malinzi amepanga kutekeleza ahadi yake nyingine kwa kuipeleka
timu ya taifa ya Tanzania ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17
‘Serengeti Boys’ kwenye kambi tulivu, ikiwezekana nje ya nchi.
Rais Malinzi aliahidi na
kutekeleza ahadi yake kuipeleka Madagascar Serengeti Boys baada ya
kuitoa Shelisheli katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika
zitakazofanyika Madagascar, mwakani. Kadhalika aliahidi kuipeleka timu
hiyo nje ya nchi ambayo hata hivyo haijateuliwa baada ya kuindoa Afrika
Kusini. Ameahidi kambi hiyo itaanza Septemba mosi, mwaka huuu.
Serengeti Boys ilipiga kambi
Hosteli za TFF, zilizo Karume kwa wiki moja kabla ya kuhamia Hoteli ya
Urban Rose, katikati ya jiji la Dar es Salaam ambako ilivunjwa kwa muda
jana Agosti 22, 2016 ambako vijana wamekwenda makwao kusalimia ndugu zao
na itaitwa mwishoni mwa mwezi huu kwa ajili ya maandalizi ya kambi ya
nje ya nchi.
Serengeti Boys imebakiwa na
mtihani mmoja kufuzu kucheza fainali hizo kwa kucheza na Congo –
Brazaville na mchezo wa kwanza utafanyika Dar es Salaam, Septemba 18,
2016 kabla ya kurudiana Septemba 30, 2016, Oktoba 1 au Oktoba 2, 2016.
TFF imejipanga kwa ajili ya kambi
hiyo, na kinachosubiriwa kwa sasa ni mapendekezo ya makocha ili
shirikisho itekeleze hatua hiyo ya kambi ya utulivu.
Kocha Mkuu wa Serengeti Boys,
Bakari Shime maarufu kama Mchawi Mweusi amesema kwamba anaamini kuwa
mchezo ujao utakuwa mgumu kwa kuwa kila timu nitajipanga kuvuka ili
kucheza fainali hizo.
No comments:
Post a Comment