Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya maendeleo ya Kilimo nchini Francis
Assenga amewashauri vijana kujikita katika masuala ya kilimo badala ya
kuchagua kazi.
Akizungumza katika kilele cha kongamano la fursa lililoandaliwa na Umoja
wa Mataifa, Assenga alisema benki hiyo imewekwa madhubuti kwa ajili ya
kutoa mikopo kwa vijana walio na ari na moyo wa kuleta mabadiliko
katika jamii.
"Wengi wamekua wakichagua kazi na wengi wao hawapendi kufanya mambo ya
kilimo lakini ni ukweli usiopingika kuwa kilimo ndio sekta ilio na fursa
nyingi" ,alisema.
Alisema kuwa kijana akiwa na mawazo makini yenye tija ni rahisi kupata fedha.
"Tatizo wengi wamejikita kulalamikia mambo ya mitaji wewe andaa wazo kwanza," alisema.
Pia katika kongamano hilo Mkuu wa mkoa wa Iringa Richard Kasesela
aliwataka vijana kupangilia matumizi yao ya fedha na kuacha tabia ya
kutumia fedha kwa matumizi yasiyo na manufaa.
"Ili ufanikiwe ni muhimu kuhakikisha fedha yako unaitumia vizuri sio unahonga tu bila sababu" alisema na kuongeza:
“Kijana ni muhimu kuwa mthubutu na kuhakikisha haukati tamaa katika mambo unayoyafanya.”
Kwa upande wake Mzungumzaji Nickson Simon (Nick wa pili) amesema dhana
ya kuamini kuwa ujana ni umri imepitwa na wakati badala yake watu
watambue kuwa kijana ni uwezo mzuri wa kufikiri bila kujali umri.
"Kijana ni uwezo wa akili kimaarifa ambayo huwezesha kutafutia ufumbuzi
mbalimbali unaweza kujihisi kijana lakini kulala kwa akili yako ukawa
mzee" alisema.
No comments:
Post a Comment