WINGA wa kushoto wa Klabu Bingwa
ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Farid Mussa, ameweka wazi kuwa
mabingwa hao hawajambania kwenda nchini Hispania kucheza soka la kulipwa
kama ilivyoripotiwa na vyombo mbalimbali vya habari.
Kwa kuudhihirishia umma, Mussa leo
amejitokeza hadharani na kupinga madai hayo akidai kuwa muda wowote
kuanzia sasa atakwenda nchini humo kujiunga na Club Deportivo Tenerife
inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza baada ya kupata ‘Visa’ maalumu ya
kuingia nchini akiwa kama mfanyakazi.
“Kwanza napenda kumshukuru Mungu
baada ya kupata visa, haikuwa kazi rahisi namshukuru Meneja Mkuu Abdul
(Mohamed) kapigania hadi suala hili limekamilika, cha kwanza nilikuwa
ninawaomba Watanzania wajue kuwa Azam haikuwa inanibania ni masuala tu
ya visa yalikuwa yakisumbua ubalozini.
“Mara baada ya kupata visa ya
kufanya kazi muda wowote ninaweza kuondoka kuanzia Januari,” alisema
Farid wakati akizungumza mbele ya waandishi wa habari leo wakati wa
zoezi la kutambulishwa wachezaji wapya waliosajiliwa na timu hiyo.
Taarifa hizo zilianza kutolewa
kwenye vyombo vya habari, kufuatia suala la Farid kwenda Hispania kuwa
kimya lakini ukweli wa mambo ni kuwa visa hiyo ndio iliyokuwa
ikikwamisha dili hilo.
Naye Ofisa Habari wa Azam FC,
Jaffar Idd, akitolea ufafanuzi suala hilo alisema kuwa lengo la uongozi
huo lilikuwa ni kinda huyo kuondoka mapema kuelekea nchini humo, lakini
suala kubwa lilikwamisha ni visa hiyo ya kufanya kazi nchini Hispania.
“Uongozi wa Azam FC ulikuwa
sambamba na Tenerife kuhakikisha Farid anaondoka, lakini tunashukuru
suala hilo limekamilika kwa asilimia 98, lakini ni kwamba Farid muda
wowote kuanzia sasa Mungu akijaalia ndani ya wiki mbili zijazo au wiki
moja anaweza kuondoka kutoka Tanzania kuelekea Hispania,” alisema.
Azam FC inaamini ya kuwa kuondoka
kwa nyota huyo wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kutafungua
milango kwa wachezaji wengine ndani ya timu hiyo na Taifa kwa ujumla
kuweza kupata nafasi ya kucheza soka la kulipwa barani Ulaya.
No comments:
Post a Comment