Friday 26 February 2016

Waziri Nape aahidi upatikanaji wa Sera ya Filamu nchini.

fiso1
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Nnauye (kulia) akiwasili eneo la tukio kushuhudia uchaguzi wa Rais, Makamu wa Rais pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF) uliofanyika 25 Februari, 2016 Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu, Bi. Joyce Fissoo.
fiso3
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Nnauye (mwenye suti nyeusi) akiwahutubia Wasanii pamoja na wageni waalikwa wakati wa siku ya uchaguzi wa Rais, Makamu wa Rais pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF) uliofanyika 25 Februari, 2016 Jijini Dar es Salaam.
fiso4
Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu, Bi. Joyce Fissoo (kushoto) akiwahutubia Wasanii pamoja na wageni waalikwa wakati wa siku ya uchaguzi wa Rais, Makamu wa Rais pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF) uliofanyika 25 Februari, 2016 Jijini Dar es Salaam.
fiso5
Viongozi wa Uchaguzi wakitoa maelekezo juu ya namna zoezi la upigaji kura kwa kiti cha Rais, Makamu wa Rais pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF).
fiso6
Viongozi wa Uchaguzi wakitoa maelekezo juu ya namna zoezi la upigaji kura kwa kiti cha Rais, Makamu wa Rais pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF).
fiso7
Baadhi ya Wasanii toka vikundi mbalimbali katika baadhi ya mikoa wakifuatilia kwa makini zoezi la upigaji kura pamoja na sera na vipaumbele vya Wagombea wa ngazi mbalimbali wakati wa uchaguzi wa Rais, Makamu wa Rais pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF) uliofanyika 25 Februari, 2016 Jijini Dar es Salaam.
fiso8
Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF), Simon Mwakifwamba (kulia) akihitimisha ukomo wa Serikali yake ya Shirikisho hilo kabla ya upigaji kura kuanza siku hiyo ya 25 Februari, 2016.

Na Tabu Mullah
Katika kuhakikisha kuwa Sekta ya Filamu nchini inakua kwa kasi na kuleta manufaa kwa wasanii, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Nape Nnauye amewahakikishia wasanii juu ya kupatikana kwa Sera ya filamu ili kuleta matokeo chanya ya katika kazi zao.

Mhe. Nnauye ameyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati wa uchaguzi wa viongozi wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF) ambapo ameahidi kushirikiana na Shirikisho hilo katika nyanja mbalimbali na kuwataka wanachama kuchagua viongozi wawajibikaji watakaoweza kusimamia Katiba kwa maslahi ya wote.

“Chagueni viongozi wenye weledi, wawajibikaji na wachapakazi ili mshirikiane nao katika kuleta maendeleo  kutokana na kazi zenu kitaifa na kimataifa”, alisema Mhe. Nnauye.
Aidha, Mhe. Nnauye ameahidi kutatua tatizo la usambazaji wa kazi feki za filamu ulioenea kwa kasi  nchini  ambapo amesema kwa kushirikiana na wadau wa filamu nchini yaani Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bodi ya Filamu pamoja na COSOTA  watahakikisha kuwa, kazi ambayo haina ubora haingii sokoni.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu, Bi. Joyce Fissoo  ameeleza kuwa, Serikali  itasimamia kwa umakini filamu za nchini kwa kutoa mafunzo kwa vijana na Shirikisho ili waelewe majukumu yao na jinsi ya kufanya kazi kwa weledi.

Bi. Fissoo ameongeza kuwa nidhamu katika kazi ni muhimu kwa wasanii kwa kuwa inaleta heshima kwao na kwa Taifa, hivyo ni wajibu wa kila msanii kufuata maadili ili kuzalisha kazi nzuri zitakazopata soko ndani na nje ya nchi.

“Kuwepo katika Vyama ni msingi mkubwa wa mafanikio, fuateni Katiba,  tafuteni vipaumbele katika kazi zenu na pia zingatieni muda kwa kila mtakalofanya, naamini  mtafanikiwa’’, alisema Bi. Fissoo.

Shirikisho la Filamu Tanzania lilifanya uchaguzi wa Rais, Makamu wa Rais na wajumbe kumi wa Bodi Februari 25 mwaka huu,  ambapo Bw. Simon Mwakifwamba alitetea nafasi yake ya kiti cha Urais wa Shirikisho hilo kwa muhula wa miaka mine (2016-2020) na Bw. Deo Sanga kuwa makamu wa Rais.

No comments:

Post a Comment