Saturday 20 February 2016

Uchaguzi Uganda Waangalizi Wamesema Unahitaji Mabadiliko Makubwa


 Tume

Waangalizi wa uchaguzi kutoka Umoja wa Ulaya wamekosoa jinsi uchaguzi mkuu wa Uganda Uliendeshwa na kusema mabadiliko makubwa yanahitajika.
Wakihutubia wanahabari, viongozi wa ujumbe kutoka Muungano wa Ulaya wamesema kulitokea kasoro nyingi.

Mwangalizi mkuu wa Umoja wa Ulaya Eduard Kukan amewaambia wanahabari kwamba ni dhahiri Tume ya Uchaguzi ya Uganda haikujifunza kutokana na mapendekezo yaliyotolewa baada ya Uchaguzi mkuu wa 2011.

Aidha, amesema haikuwa haki kufunga usajili wa wapiga kura Mei mwaka jana akisema hatua hiyo iliwafungia watu waliotimiza umri wa miaka 18 baada ya tarehe hiyo.

"Tume haina uwazi na wadau hawana imani nayo. Tume haina uwazi katika kufanya maamuzi na katika kuwafahamisha wapiga kura kwa wakati na kwa ufasaha,” amesema.

Bw Kukan amesema kucheleweshwa kwa karatasi na vifaa vya kupigia kura pamoja na kuchelewa kuanza kwa upigaji kura siku ya uchaguzi kuliathiri imani ya watu katika zoezi hilo.
Ameshutumu pia kukamatwa na kuzuiliwa kwa kiongozi wa upinzani Dkt Kizza Besigye pamoja na kufungwa kwa mitandao ya kijamii.

Mwangalizi mkuu wa Bunge la Ulaya Jo Leinen kwa upande wake amesema wagombea wote hawakupewa nafasi sawa katika vyombo vya habari na wanasiasa pamoja na raia waliounga mkono upinzani walihangaishwa.

Amesema pia kwamba fedha za serikali na chama lazima kutenganishwa.
"Kuna mengi sana ambayo yanafaa kurekebishwa,” amesema.
Waangalizi wa Jumuiya ya Madola, wanaoongozwa na rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo, pia wameeleza kutoridhishwa kwao na baadhi ya mambo yaliyotokea wakati wa uchaguzi.
Ameshutumu kukamatwa na kuzuiliwa kwa Dkt Besigye akisema hatua hiyo iliongeza tu wasiwasi.
Matokeo kamili ya uchaguzi wa urais yanatarajiwa kutangazwa kabla ya saa kumi alasiri leo.
Matokeo yaliyotangazwa kufikia sasa yanaonyesha Rais Yoweri Museveni anaongoza akiwa na zaidi ya asilimia 60 ya kura Dhidi ya Dkt Kizza Besigye aliye na asilimia 34 ya kura zilizohesabiwa.

No comments:

Post a Comment