Friday 26 February 2016

Basata Wamlilia Mapili

mapi
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limepokea kwa masikitiko na majonzi makubwa kifo cha Msanii Mkongwe wa muziki wa dansi Kassim Mapili kilichotokea katikati ya wiki hii nyumbani kwake Tabata jijini Dar es Salaam.

Na Tabu Mullah
 
Kassim Mapili ni msanii na mdau wa muda mrefu wa sekta ya Sanaa nchini. Amekuwa ni taa na nuru ambayo katika kipindi chote cha uhai wake imeangaza na kutoa mwanga angavu kwenye sekta ya Sanaa.

Mchango wake katika muziki wa dansi na ule wa kiweledi katika kuandaa na kukuza bendi na wasanii mbalimbali wa muziki wa dansi nchini hautasahaulika kamwe. Ni Msanii aliyeacha alama kuu katika muziki wa bendi na amejitolea kwa kiasi kikubwa katika kuufikisha muziki wa dansi ulipo leo.

Aidha, pamoja na kuwa mwimbaji na mpigaji gitaa katika Bendi mbalimbali zikiwemo za Kilwa Jazz, Polisi Jazz, Vijana Jazz na nyingine nyingi Mzee Kassim Mapili alikuwa mstari wa mbele kujenga mfumo wa Utawala kwenye sekta ya Sanaa na kuhakikisha wasanii wa muziki wa dansi wanakuwa na chombo cha kuwawakilisha na kutetea maslahi yao.

Mwaka 1982 alikuwa miongoni mwa wasanii waliokutana Mjini Bagamoyo na kuunda Chama cha Muziki wa Dansi Tanzania (CHAMUDATA) ambacho hadi leo kinatetea na kuwawakilisha wasanii wa muziki wa dansi.

Aidha, Mzee Mapili amekuwa bega kwa bega na Baraza la Sanaa la Taifa katika programu zake mbalimbali na utendaji kazi wa kila siku. Kwa mfano; amekuwa mmoja wa wadau ambao wamekuwa wakishiriki kikamilifu kwenye Programu ya Jukwaa la Sanaa inayoandaliwa na BASATA kwa kushirikiana na chama cha waandishi wa habari za Sanaa na Utamaduni.

Baraza, wasanii na wadau wote wa Sanaa hatuna budi kuendelea kuenzi mema yote aliyotuachia marehemu Kassim Mapili hasa katika kutunga nyimbo za hamasa na ujumbe makini na wenye mashiko kwa jamii yote ya Watanzania
.
Hakika pengo lililoachwa na Marehemu haliwezi kuzibika, kwani imekuwa ni kama mshumaa uliyozimika ghafla wakati tukiingia kwenye giza.

Baraza linatoa pole kwa familia ya Marehemu, chama cha muziki wa dansi, shirikisho la muziki na wasanii wote kwa ujumla. Ni matumaini ya Baraza kwamba, tutaendelea kuenzi mema yote yaliyotendwa na Marehemu, hasa kudumisha upendo na amani katika tasnia yetu ya Sanaa na taifa kwa ujumla.
Bwana ametoa na Bwana ametwaa, Amen
Godfrey Mngereza
KATIBU MTENDAJI

No comments:

Post a Comment