Wednesday 17 February 2016

Christopher Mwahangila Joshua Mlelwa nao Watakuwemo Tamasha La Pasaka


mle
Na Mwandishi Wetu
KAMATI ya maandalizi ya Tamasha la Pasaka imewatangaza waimbaji wengine watakaopanda jukwaa la tamasha Hilo linalotarajia kufanyika mikoa ya Geita, Mwanza na Wilaya ya Kahama ikiwa ni muendelezo  wa maandalizi ya kuelekea sikukuu hiyo.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi, Alex Msama wameongeza idadi ya waimbaji katika tamasha hilo ambao ni Christopher Mwahangila na Joshua Mlelwa.
Msama alisema wamepanga tamasha hilo litakaloanza Machi 26 mkoani Geita kwenye ukumbi wa Desire huku Machi 27 litafanyika jijini Mwanza katika uwanja wa CCM Kirumba na Machi 28 litamalizia Uwanja wa Taifa ulioko Wilayani Kahama.
Msama alitumia fursa hiyo kuwaomba wakazi wa mikoa hiyo kujitokeza kwa wingi ili kufanikisha malengo ya Tamasha hilo ambayo ni pamoja na kusaidia wenye uhitaji maalum kama yatima, walemavu  na wajane.
Aidha Msama alisema mwaka huu kamati yake imejipanga kugawa baiskeli zaidi ya 100 kwa walemavu ikiwa ni sehemu ya tamasha hilo.
“Tamasha la Pasaka linawajali wenye uhitaji maalum kama walemavu, yatima na wajane ambao wanapata misaada kupitia mapato ya mlangoni kupitia viingilio,” alisema Msama.
Msama aliwataja waimbaji wengine waliothibitisha kushiriki tamasha hilo ni pamoja na Rose Muhando, Bonny Mwaitege, Upendo Nkone, Jesca BM Honore, Faustine Munishi, Anastazia Mukabwa na Jennifer Mgendi.

No comments:

Post a Comment