Sunday 28 February 2016

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amekuta ufisadi Bandari ya Mtwara

kasl4
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua bandari ya Mtwara na kunusa harufu ya ufisadi katika utoaji wa zabuni  ya ujenzi wa gati mpya tatu.
 
Wazi Mkuu ambaye alikagua eneo la ujenzi wa gati hizo jana (Jumamosi, Februari 27, 2016), alisema anazo taarifa juu ya utolewaji wa zabuni hiyo na mzabuni ameshashinda lakini kuna madai kwamba watu wa manunuzi kupitia PPRA  ndiyo wanakwamisha zabuni hiyo.
 
Aliwaomba wabunge wa mkoa wa Mtwara washirikiane kusimamia suala hilo ili ujenzi wake uweze kuanza mara moja na kuleta ajira kwa wana Mtwara. “Ujenzi ukikamilika siyo tu ajira zitaongezeka bali hata meli nyingi zitaleta mizigo katika bandari hii na mapato ya mkoa yataongezeka”, alisema.
 
“Natambua kwamba kuna mpango wa kujenga gati nne ambapo moja kati ya hizo itajengwa na TPA (Mamlaka ya Bandari) lakini hizi tatu zilitangazwa na kupata mzabuni ambaye ni kampuni ya Hyundai kutoka Japan. Lakini hii kampuni imekuwa ikizungushwa bila sababu. Tutafuatilia kubaini tatizo liko wapi,” aliongeza.

“Sasa hivi tuna uwezo wa kupaki meli moja tu, lakini gati zikikamilika tutaweza kuwa na meli tatu kwa mpigo, cha msingi tusimamie maamuzi yetu kwamba lazima wafanyabiashara wa korosho watumie bandari hii kusafirisha mizigo yao na si kuipeleka kwingine.”

“Kwenye Bodi ya Korosho nako kuna majipu yanahitaji kutumbuliwa. RCC ilishakaa na kupitisha uamuzi kuwa mizigo yote ipitie bandari ya Mtwara lakini kuna watu ndani ya Bosi hiyo wanatoa vibali vya kusafirisha mizigo kupitia bandari ya Dar es Salaam. “
Alimtaka mkuu wa bandari ya Mtwara (Port Master) Bw. Prosper Kimaro awe makini na watu wa kitengo cha manunuzi katika bandari hiyo kwani kimekuwa chanzo  cha upotevu wa fedha za Serikali kutokana na ujanja wa watu wachache.
“Hapa si kuna mtu alitaka kuiba sh. milioni 300 kwa kufoji saini za wakubwa wake? alihoji Waziri Mkuu swali ambalo lilijibiwa na Bw. Kimaro kwamba ni kweli lakini uongozi uliingilia kati kabla wizi huo haujakamilishwa.
Kuhusu fidia kwa wakazi wa vijiji vya Kisiwa na Mgao ambao wamekubali kuhama ili kupisha upanuzi wa bandari hiyo,  Waziri Mkuu aliwahakikishia wabunge hao pamoja na uongozi wa bandari kwamba kiasi cha sh. bilioni 13.8/- kimekwishatengwa na Wizara na kitatolewa mapema mwezi ujao.
Alitumia fursa hiyo kusisitiza udhibiti wa bandari bubu ambazo zinatumiwa kuingiza sukari na  mchele mchezo ambao unaikosesha Serikali mapato.  “Mkuu wa Mkoa, nilikwishatoa agizo kama hilo wakati nimeenda kukagua bandari ya Tanga. Kaa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa nanyi pia muweke mbinu za kudhibiti upenyo huu wa kuingiza bidhaa za magendo kwa sababu hawa ndiyo wanaokwepa kulipa kodi ya Serikali,” alisisitiza.
Naye, Mkuu wa bandari hiyo, Bw. Kimaro wakati akitoa taarifa ya utendaji wa bandari mbele ya Waziri Mkuu, alisema bandari hiyo ilianzishwa mwaka 1950 na imekuwa inakabiliwa na ufinyu wa gati ya kuegesha meli, vifaa vya kupakulia na kupakia mizigo na kwamba hivi sasa wamekwishapata winchi ya bandarini (harbour crane) yenye uwezo wa kubeba tani 100 na tayari wako kwenye mpango wa kujenga gati moja.

‘SERIKALI YATENGA SH. BILIONI 1.6/- VYUO VYA UALIMU”

JILWAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imetenga kiasi cha sh. bilioni 1.65/- kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo kwenye vyuo vya walimu hapa nchini.
Alitoa kauli hiyo jana (Jumamosi, Februari 27, 2016), wakati akizungumza na walimu na watumishi Wa sekta ya elimu kutoka wilaya zote za Mkoa wa Mtwara uliofanyika kwenye ukumbi wa Chuo cha Ualimu Mtwara

“Serikali inatambua uhumimu wa mafunzo kwa vitendo katika vyuo vya ualimu ni kwa sababu hiyo Mwezi huu wa Februari tumetoa sh. bilioni 1.65/- kwa vyuo vya ualimu 35 vya umma nchini ili kuwezesha wakufunzi na walimu wanafunzi kushiriki kikamilifu mafunzo kwa vitendo (Block Teaching Practice),” alisema huku akishangiliwa.
Alisema fedha hizo zinapaswa zitumike kulipia posho za kujikimu, nauli na ununuzi wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia.

Mapema, akizungumza na mamia ya wakazi wa Mtwara kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa mashujaa, Waziri Mkuu alisema Serikali imedhamiria kuimarisha elimu na akawaonya wote wanaowaharibia elimu watoto wa kike.

“Tunataka watoto wa kike wasome wa Kitanzania wasome hadi elimu ya juu waje wawe watumishi Wa umma hapo baadaye. Kila mmoja awe mlinzi wa mwenzake tukikumbuka kaulimbiu ya Mama Salma Kikwete ya kwamba ‘Mtoto wa Mwenzio ni wako’,” alisema.
“Yeyote atakayemharibia mtoto wa kike masomo kwa kumrubuni na chips au pipi ajiandae kwenda Lilungu, (gereza la mkoa wa Mtwara)”, alisema.

No comments:

Post a Comment