Mkurugenzi wa Idara ya Habari,
MAELEZO Bw. Hassan Abbas akizungumza na waandishi wa habari (hawapo
pichani) kuhusu taasisi za Serikali kutekeleza agizo la kuhuisha taarifa
na huduma katika Tovuti zao mapema kabla ya mwisho wa mwezi huu katika
mkutano uliofanyika Ofisi za Wakala ya Serikali Mtandao (EGA) hivi
karibuni Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Meneja wa Habari, Elimu na
Mawasiliano wa Wakala ya Serikali Mtandao Bibi. Susan Mshakangoto.
Meneja wa Habari, Elimu na
Mawasiliano wa Wakala ya Serikali Mtandao Bibi. Susan Mshakangoto
akifafanua jambo kwa waandishi wa habari wakati wa mkutano na waandishi
hao hivi karibuni jijini Dar es Salaam, kuhusu taasisi za umma kuhuisha
taarifa katika Tovuti zao. Kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari,
MAELEZO Bw. Hassan Abbas.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari,
MAELEZO Bw. Hassan Abbas akiwaonyesha waandishi wa habari mwongozo wa
utengenezaji wa Tovuti za Serikali wakati wa mkutano wake na waandishi
hao hivi karibuni Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Meneja wa Habari, Elimu
na Mawasiliano wa Wakala ya Serikali Mtandao Bibi. Susan Mshakangoto.
Picha na MAELEZO
Na Ismail Ngayonga MAELEZO
SERA ya Taifa ya Teknolojia ya
Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ya mwaka 2003, pamoja na mambo mengine
inasisitiza umuhimu wa Serikali kutumia fursa za TEHAMA katika utendaji
kazi wa kila siku na utoaji huduma kwa wananchi.
Katika kutekeleza sera hiyo, mwaka
2004 Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma (OR-MUU) ilianza
kuchukua hatua mbalimbali kuongeza matumizi ya TEHAMA katika kuimarisha
mifumo ya utoaji habari na huduma kwa wananchi.
Moja ya maeneo ya TEHAMA ambayo
Serikali imewekeza na kupata mafanikio makubwa ni pamoja na eneo la
tovuti ambapo hadi kufikia mwaka 2010 takribani Taasisi zote za Serikali
zilikuwa na tovuti.
Katika kipindi cha mwaka mmoja wa
Serikali ya Awamu ya Tano, kumekuwepo na mapinduzi makubwa katika
mfumo wa upashanaji wa habari na utoaji wa huduma kwa umma kupitia
tovuti.
Mtendaji Mkuu wa Serikali Mtandao,
Dkt. Jabiri Bakari anasema taasisi za umma zinapaswa kuwa na tovuti
zitakazosaidia wananchi kupata kwa urahisi taarifa zinazohusu shughuli
na huduma mbalimbali zinazotolewa na taasisi hizo.
“Tovuti za Serikali zinatakiwa
kuwa kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza na mwananchi anapofungua
tovuti hizo lugha itakayoonekana kwanza iwe ni Kiswahili na muda wowote
mwananchi huyo anaweza kubadili kwenda kwenye lugha ya Kiingereza”.
Dkt. Bakari amesema kuwa Wakala imetoa miongozo ya kusimamia na kuendesha tovuti hizo na unapatikana kwenye tovuti ya Wakala www.ega.go.tz sehemu ya Miongozo na Viwango.
Akizungumzia mafanikio ya Wakala
hiyo, Dkt. Jabiri anasema Wakala imetengeneza mifumo mbalimbali na
kuweka miundombinu ya kuwezesha taasisi za umma kutumia Tehama katika
utoaji wa huduma kwa wananchi.
“Tovuti Kuu ya Serikali ni zao la
kwanza la Wakala na ilibuniwa na kusanifiwa na wataalam wa ndani. Katika
tovuti hiyo ambayo pia ni mfumo, ina taarifa za baadhi ya taasisi za
umma, sekta mbalimbali na huduma zake pamoja na balozi zilizoko nchini
na zile za kwetu zilizoko nje ya nchi”, anasema Dkt. Bakari.
Anaongeza kuwa mfumo mwingine
uliotengenezwa na Wakala hiyo ni Tovuti Kuu ya Ajira ambayo humwezesha
mwananchi kuona ajira mbalimbali zinazotangazwa na Serikali ambapo
muombaji wa ajira anaweza kutuma wasifu wake kwa njia ya mtandao na
nafasi zinapotangazwa zenye kuhitaji mtu mwenye sifa hizo.
Kwa mujibu wa Dkt Jabiri anasema
jitihada mbalimbali zinatekelezwa na Wakala ili kuwezesha taasisi za
umma kutoa huduma zao kwa njia ya mtandao kwa kuongeza uwezo wa wataalam
wa Tehama kwa kuwapa maarifa na ustadi wa kubuni.
Dkt. Jabiri anasema Wakala imetoa
mafunzo kuhusu usimamizi na Ujenzi wa Mtandao wa Mawasiliano Serikalini
kwa taasisi za umma 149 wakiwemo Maofisa TEHAMA 226, Mafunzo ya
uendeshaji wa Vituo vya data kwa Taasisi za umma 91 wakiwemo Maofisa
TEHAMA 162.
Aidha Mafunzo ya Usimamizi wa
Mfumo wa Barua Pepe Serikalini yametolewa kwa taasisi 157 pamoja na
Mafunzo ya usimamizi wa taarifa tovuti za serikali yametolewa kwa
taasisi 71.
“Mafunzo ya uwekaji taarifa katika
tovuti kuu yametolewa kwa taasisi 86 na Mafunzo hayo yanaendelea
kutolewa kwa kila taasisi ambayo inatengenezewa Tovuti na Wakala”
anasema Dkt. Jabiri.
Kwa upande wake Meneja Habari,
Elimu na Mawasiliano wa Wakala wa Serikali Mtandao, Suzan Mshakangoto
anasema mbali na kuanzisha mtandao huo Serikali imeziagiza taasisi zote
za umma kuhuisha taarifa katika tovuti zake na Tovuti Kuu ya Serikali (www.tanzania.go.tz).
Anaongeza kuwa tangu kuanzishwa
kwa tovuti hizo kumesaidia kuongeza kasi ya utendaji, uwazi, ufanisi,
uwajibikaji na tija katika utoaji wa taarifa na huduma kwa wananchi,
pamoja na changamoto kadhaa zilizojitokeza katika usimamizi wa tovuti
hizo.
Akifafanua zaidi anasema miongoni
mwa changamoto hizo ni pamoja na tovuti za taasisi za umma kutokuwa na
taarifa mpya na za mara kwa mara, na kutofuatwa kwa mwongozo uliowekwa
unaosisitiza usanifu wa tovuti hizo.
Naye Mkurugenzi wa Habari, Hassan
Abbas anasema ofisi yake kwa kushirikiana na e-GA tayari imezisaidia
Halmashauri 93 kuhuisha taarifa zilizopo katika tovuti zao ili
kuwawezesha wananchi kufahamu huduma mbalimbali zinazotolewa na Serikali
katika maeneo yao.
Abbas anasema tovuti ni mojawapo
ya nyenzo na njia rahisi na ya haraka ya kutoa taarifa na kufikisha
huduma kwa umma kwani miaka ya nyuma taarifa na huduma za Serikali
zilitolewa kwa njia ya kutembelea ofisi husika au kwa kupitia vyombo vya
habari.
Anasema Serikali imetoa mafunzo
kwa Maafisa Habari katika Wizara, Idara, Wakala na Taasisi mbalimbali
jinsi ya kuboresha taarifa katika tovuti zao, na kuanzia sasa ofisi
yake itaanza kufanya tathimini ili kufahamu Wizara ambazo hazijaanza
kuhuisha taarifa zake.
Kwa mujibu wa Abbas anasema
Serikali imekusudia kupanua wigo wa mawasiliano katika Wizara, Idara, na
Taasisi zake kwa kuwahimiza Maafisa Habari kutumia zaidi mitandao ya
kijamii kwa ajili ya kujibu na kutoa ufafanuzi wa hoja mbalimbali
zinazoelekezwa kwa Serikali.
Katika kuboresha mfumo wa
mawasiliano Serikalini, ofisi yake imeanzisha akaunti ya twitter ya;
msemaji wa Serikali@TZ_Msemaji Mkuu ambayo mwananchi anaweza kuifuata
akaunti hiyo kwa kutafuta Msemaji Mkuu wa Serikali on Twitter.
Anasema wananchi wengi kwa sasa
wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii kwa ajili ya kuendesha mijadala
mbalimbali ambayo baadhi yao imekuwa ikipotosha ukweli kuhusu
utelekezaji wa sera mbalimbali za Serikali.
Abbas anasema jukumu la kuboresha
mawasiliano kati ya Serikali na Wananchi ni suala mtambuka, na hivyo ni
wajibu wa Maafisa Habari wa Wizara, Idara, Taasisi, Wakala za Serikali
kutoogopa kutoa taarifa muhimu kwa waandishi wa habari.
“Waandishi wa habari wasitoe
taarifa zisizofanyiwa utafiti wa kutosha kwa wananchi, ni vyema sote
tushirikiane katika kutoa taarifa sahihi kwa wananchi kuhusu sera na
mikakati ya serikali ili kuleta maisha bora kwa watanzania wote” anasema
Abbas.
Kwa kutambua umuhimu wa tovuti
kama nyenzo kuu ya mawasiliano, Serikali kupitia Mradi wa Uimarishaji wa
Mifumo ya Umma (PS3) unaofadhiliwa na shirika la misaada la Marekani
iliunda kikosi kazi kwa ajili ya uhuishaji wa tovuti za Mamlaka ya
Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Kikosi kazi hicho kinahusisha
Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Ofisi ya Rais- Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), na Wakala wa Serikali Mtandao
(E-GA).
Msimamizi wa Mifumo ya Taarifa wa
PS3, Bunto Mbozi anasema tovuti nyingi za TAMISEMI zimetengenezwa,
zinasimamiwa na kuendeshwa bila kuwepo na utaratibu unaofanana, hali
hiyo inasababisha uwepo wa tovuti zisizokidhi viwango na ubora
kufuatana na mahitaji ya watumiaji.
Anaongeza kupitia mradi, PSE3
imekusudia kuhuisha taarifa zote za tovuti za Serikali, ambapo kwa sasa
wataanza na Halmashauri 93 nchini na baadae katika Wizara, Idara,
Taasisi nyingine za Umma.
Bunto anasema mradi huo
ulizinduliwa mapema mwaka huu mkoani Iringa ambapo hadi kufikia mwezi
Agosti mwaka huu, jumla ya mikoa 13 ilifikiwa na taasisi hiyo na
kuendesha mahojiano na Watendaji Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Idara na
vitengo mbalimbali.
Anaitaja mikoa hiyo kuwa ni Iringa, Shinyanga, Dodoma, Mbeya, Mwanza, Kagera, Mara, Rukwa, Kigoma, Lindi, Mtwara na Morogoro.
Akifafanua zaidi anasema katika
utafiti uliofanyika ulibaini kuwa mikoa mingi ilianza kutengezeza tovuti
zao lakini hazikikuwa na taarifa muhimu zinazohitajika na wananchi wa
kawaida.
“Tovuti ya Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) inatembelewa na watu zaidi ya 500,000 kwa siku, hii
inatokana na mahitaji ya huduma inazotoa TRA kwa wananchi, hivyo mradi
huu pia umekusudia kuzifanya tovuti za Mikoa na Halmashauri kutembelewa
na wananchi wengi zaidi” anasema Bunto.
Kwa mujibu wa Bunto anasema, mradi
huo uliichagua TAMISEMI kutokana na Ofisi hiyo kutoa huduma muhimu
zinazomgusa wananchi wa kawaida ikiwemo afya, maji, elimu, mazingira,
uvuvi, ufugaji na kadhalika, ambapo wananchi wengi wanapenda kufuatilia
taarifa na huduma hizo katika ofisi za umma.
Anaongeza uhuishaji wa taarifa za
tovuti utasaidia kutangaza fursa na rasilimali za kiuchumi zilizopo
katika mikoa, hatua itayoziwezesha halmashauri nyingi kuibua vivutio vya
uwekezaji sambamba na kuboresha utoaji huduma kwa wananchi.
No comments:
Post a Comment