Monday 28 November 2016

Idadi ya waliofariki katika ghasia Uganda yafikia 62

Idadi ya waliofariki katika ghasia nchini Ugnada imefikia 62
Maafisa wa polisi nchini Uganda wametawanya watu waliojaribu kuingia katika chumba cha kuhifadhia maiti ili kuchukua miili ya ndugu zao waliouawa katika mji wa magharibi wa Kasese wikendi iliopita kulingana na gazeti la serikali New Vision.
Tayari idadi ya watu waliouawa katika mapigano hayo imefika 62 kulingana na maafisa wa polisi.
Maafisa wa polisi walikabiliana na wapiganaji wanaotaka kujitenga magharibi mwa taifa hilo.
Mfalme wa Rwenzururu, Charles Wesley Mumbere, amekamatwa na kupelekwa katika mji mkuu wa Kampala, akituhumiwa kwa kuchochea ghasia ,mashtaka ambayo amekana.
Mfalme huyo amekana kumiliki wapiganaji na kuchochea ghasia.
''Tunataka miili ya watu wetu ili kuwapatia maziko ya heshima. Baadhi ya miili ipo katika lango la jumba la mfalme huyo na haturuhusiwi kuingia'',alisema Joy Biira.
Biira ambaye ni mwanahabari wa kituo cha runinga ya KTN nchini Kenya alikamatwa na kuzuiliwa na maafisa wa usalama nchini Uganda usiku wa Jumapili.
Vyombo vya habari vinasema bi Biira alikamatwa pamoja na wengine watano kwa tuhuma za kupiga picha na video kuhusu operesheni ya maafisa wa usalama katika kasri la mfalme wa Rwenzururu na kuzichapisha kwenye mitandao ya kijamii.
Wanahabari na mashirika ya kutetea haki za kibinadamu wametoa wito kwa serikali kumwachilia huru.

Kitambulisha mada #FreeJoyDoreen (Mwachilie huru Doreen) kinavuma katika mtandao wa Twitter nchini Kenya.

No comments:

Post a Comment