Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la
Nyumba la Taifa NHC Bw. Nehemia Mchechu akizungumza na waandishi wa
habari katika makao makuu ya shirika hilo Upanga jijini Dar es salaam
kuhusu uuzwaji mpya wa nyumba za shirika hilo kwa utaratibu wa sera
mpya ya Mnunuzi Mpangaji maarufu kama “Tenant Purchase Scheme” ambayo
ilitumika sana na Shirika lilipoanzishwa hadi mwishoni mwa miaka ya
1970.
Baadhi ya wakuu wa vitengo wa
Shirika la Nyumba NHC kutoka kushoto ni Suzan Omary Mkuu wa Kitengo cha
Mawasiliano, Itandula GambalagiMeneja Mauzo NHC na Meneja Biashara na
Mipango Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu Bw. Arden Kitomari wakiwa katika
mkutano huo.
kulia ni Meneja wa Mauzo wa NHC Bw. Tuntufye Mwambusi akiakiwa pamoja na maofisa wengine wa shirika hilo wakati wa mkutano huo na waandishi wa habari.
Shirika la Nyumba la Taifa
linapenda kuutaarifu Umma wa Watanzania kuwa leo tarehe 07/11/2016
linazindua sera mpya ya Mnunuzi Mpangaji maarufu kama “Tenant Purchase
Scheme” ambayo ilitumika sana Shirika lilipoanzishwa hadi mwishoni mwa
miaka ya 1970.
Katika Sera hii ya Mnunuzi
Mpangaji, mnunuzi atalipa kidogo kidogo kila mwezi (kiwango hutofautiana
kulingana na bei ya nyumba na muda ambao mnunuzi mpangaji atatumia
kulipa) kiwango kilichowekwa na kukubaliwa na Shirika na kiwango
huhesabika kama gharama ya pango kwa mwezi na malipo ya kununulia nyumba
na mnunuzi atahesabika kama mpangaji mpaka kiasi anacholipia kila mwezi
kitakapofikia gharama ya nyumba, nyumba inakuwa yake rasmi na
hukabidhiwa.
Sera hii itawasaidia Watanzania
wengi ambao wana uwezo wa kulipia nyumba zao, lakini hawakidhi vigezo
vya kibenki kuweza kupata Mkopo wa nyumba hizi zilizojengwa kwa ajili ya
makazi katika mikoa ya Geita (Bombambili, Chato), Katavi (Ilembo,
Inyonga), Dodoma (Kongwa), Ruvuma (Mkuzo), Kigoma (Mlole), Babati
(Mrara), Singida (Unyankumi), Kagera (Muleba), Tabora (Uyui, Igunga)
Arusha (Longido), Morogoro (Mvomero), Shinyanga (Bukondamoyo), Njombe
(Makete), Mara (Buhare), Mtwara (Masasi), Mbeya (Mbarali) na Mkinga
Tanga.
Chini ya utaratibu huu mpya
unaoanza kutumika kuanzia Novemba 2016; Muombaji atapaswa kuainisha
kwenye fomu ya maombi aina ya nyumba anayohitaji na Mkoa ilipo.
Sifa kuu ya Mnunuzi Mpangaji ni
kwamba awe na Mshahara au kipato kinachozidi Shilingi 500,000 kwa mwezi.
Mnunuzi Mpangaji atahitajika kulipa malipo ya awali ya asilimia
Ishirini na tano (25%) ya thamani ya nyumba anayotarajia kununua (ikiwa
na kodi ya ongezeko la thamani yaani VAT).
Kiwango cha riba kitakuwa
asilimia (15%) ya kiwango kilichosalia kuwekwa. Mnunuzi atahitajika
kulipa malipo kwa mpango wa mwezi mmoja mmoja kulingana na thamani ya
nyumba. Kiwango cha juu kabisa cha muda wa kulipa ni miezi 120 sawa na
miaka kumi (10), Zaidi ya hayo malipo ya Bima ya Maisha ya asilimia moja
(1%) na Bima ya Moto ya asilimia 0.077 yatalipwa mwanzoni mwa kila
mwaka.
Kulingana na Mpango Mkakati wa
Shirika la Nyumba la Taifa kwa kipindi cha mwaka 2015/2016 hadi mwaka
2024/2025, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), litajenga nyumba kwa ajili
ya kuuza kwa wananchi wa aina zote za vipato; yaani wale wa vipato vya
chini, vya kati na juu. Shirika litajenga nyumba 12,000 za gharama
nafuu, nyumba 13,500 za kipato cha kati, nyumba 2,700 za kipato cha juu
na nyumba 1,800 za bishara kufikia 2025.
Lengo kuu la Mpango Mkakati huu, ni kuliwezesha Shirika kujenga nyumba za makazi na biashara zipatazo 30,000 nchi nzima.
Bei za nyumba ni kati ya
sh.29,000,000/= hadi sh.49,000,000/= (bila VAT). Bei hizi ni kulingana
na ukubwa wa nyumba na mkoa nyumba ilipo. Ukubwa wa nyumba ni kuanzia
vyumba viwili hadi vitatu.
Nyumba hizi za gharama nafuu
zinajengwa nchi nzima zikiwa na lengo la msingi la kuwezesha Watanzania
wengi zaidi kumiliki nyumba za kuishi ambao hawawezi kujijengea nyumba
kutokana na kuwa na kipato cha chini.
Wakati Shirika likijaribu kuweza
kuongeza idadi ya nyumba za gharama nafuu huku Shirika likipata faida
kidogo, Shirika pia lina lengo la kujenga nyumba katika maeneo yote ya
nchi ili kufikia kila sehemu ya nchi, kikubwa zaidi ni kwamba
litasaidia kujenga nyumba katika maeneo mapya na wilaya mpya
zinazoanzishwa na Serikali.
Kwa kuongezea ni kwamba
uendelezaji wa nyumba za gharama nafuu una athari nyingi chanya katika
uchumi wa maeneo husika kwa mfano unachangia sana kukua kwa uchumi wa
maeneo hayo kwa kutengeneza ajira za moja kwa moja na zile zisizo za
moja kwa moja, hivyo kupandisha kiwango cha maisha cha maeneo hayo.
No comments:
Post a Comment