
Kocha Mingange aliliambia gazeti hili jana asubuhi baada ya kumalizika mazoezi na vijana wake kwenye Uwanja wao wa nyumbani uliopo ndani ya Gereza Kuu la Ruanda-Mbeya, kwamba wanatambua fika Yanga wana hasira za kuchapwa na City Mbeya.
“Kesho (leo) wataisoma namba tena, tutawaongezea maumivu zaidi kwani lazima wake, vijana wangu wako sawasawa...Ninatambua na hata wachezaji wangu wanatambua, Yanga wana hasira na maumivu ya kichapo na ninawatumia salamu kwamba wasifikirie watapata mteremko kutoka kwangu.
“Wachezaji wangu wote wameshajengwa kisaikolojia kuelekea mechi ya kesho (leo) na wapo ‘Fiti, lazima tuwakalishe tu,” alijinoma Mingange.
Alisema wanatambua fika nguvu wanazotaka kuzitumia kuhakikisha wanapata ushindi kwenye mechi ya kesho hivyo na wao wamejiandaa vyema kuona Yanga haondoki Mbeya na pointi hata moja huku akivunia wachezaji wake wa kutegemewa kuwapo dimbani leo.
“Yanga tunawajua, kuna maeneo ukiyabana sawasawa, hawafurukuti, Donald Ngoma, Msuva (Simon) na Tambwe (Amiss) hawa ukiwakamata, kisha ukambana Niyonzima katikati kuhakikisha achezeshi timu, utakuwa umemaliza kazi, mbona Yanga wepesi tu hawa...,” alisema Mingange aliyesema kazi kubwa aliyonayo ni kuanzisha wachezaji wakali.
No comments:
Post a Comment