Saturday, 10 December 2016

Yanga, Azam kujipima uwezo leo

Dar es Salaam. Katika kujiweka fiti na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara utakaoanza Desemba 17, Yanga na Azam zinaingia viwanjani leo kwa michezo ya kirafiki.
  Pia, michezo hiyo itakuwa maalumu kwa timu hizo kuwapima wachezaji wao wapya iliowasajili wakati huu wa dirisha dogo litakalofungwa Desemba 15.
Mabingwa watetezi Yanga pia watatumia mchezo huo kumuaga kiungo Mbuyu Twite ambaye ametemwa na klabu hiyo baada ya kuitumikia kwa miaka minne.
Twite ametemwa kikosini Yanga kumpisha kiungo mwingine Mzambia Justine Zullu ambaye ataonekana kwa mara ya kwanza leo akiwa ndani ya jezi ya timu hiyo huku mashabiki wakiwa na hamu kubwa ya kuona uwezo wake.
Kocha msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi alisema mchezo huo utatumika kwa ajili ya kocha mpya George Lwandamina kukiangalia kikosi chake kama kiko tayari kwa ajili ya mzunguko wa pili wa ligi utakaoanza Desemba 17 kwa timu hiyo kucheza na JKT Ruvu.
Yanga itacheza na JKU ya Zanzibar kwenye Uwanja wa Uhuru wakati Azam itaikabili Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi.
Azam itatumia mchezo huo kuwapima baadhi ya wachezaji kutoka nchi mbalimbali waliofika kwa ajili ya majaribio.
Wachezaji hao ni washambuliaji Yahaya Mohammed na Samuel Afful pamoja na beki wa kati, Yakubu Mohammed wote kutoka Ghana.
Wengine ni Batetakang Flavius ambaye pia ni beki wa kati na kiungo mkabaji,  Stephane Kingue.
Azam itaanza kampeni yake mzunguko wa pili kucheza na Lyon kwenye Uwanja wa Uhuru.

No comments:

Post a Comment