Sunday, 6 November 2016

Dk. Shein: Serikali imedhamiria kuimarisha ujenzi wa dakhalia katika vyuo

mq3
Na Masanja Mabula -Pemba
 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameiagiza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kuangalia upya na kwa mapana yake mahitaji, huduma na maeneo ya kujenga dhakhalia kwa ajili ya skuli za sekondari na vyuo.

Dk. Shein amesema serikali imedhamiria kuimarisha ujenzi wa dakhalia katika vyuo kwa kuwa zina mchango kubwa sio tu katika kuimarisha masomo bali hata kujenga mshikamano miongoni mwa wanafunzi wanaotoka maeneo mbali mbali ya Zanzibar.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa dakhalia ya wasichana katika Chuo cha Ufundi huko Kingeja,Wilaya ya Mkoani Mkoa wa Kusini Pemba jana, Dk. Shein alieleza kuwa mara baada ya Mapinduzi ya mwaka 1964, Serikali iliweka mkakati maalum wa kujenga na kuimarisha dakhalia kwa kuwa ndio lilikuwa suluhisho la haraka la kuwapa fursa watoto wengi kutoka mashamba kupata elimu.  

Dk. Shein alieleza kuwa serikali hivi sasa kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA0 ina mpango wa kujenga dakhalia ya kisasa mithili ya ‘mji wa wanafunzi’ huko Tunguu, wilaya ya Kati,Unguja ambapo wanafunzi wa vyuo jirani na SUZA wataweza kuishi katika dhakhalia hiyo.

“Katika eneo hilo (la dakhalia) tutajenga maduka, viwanja vya michezo na kila kitu muhimu kawa maisha ya wanafunzi” Dk. Shein aleleza.

Katika hotuba yake hiyo, Dk. Shein alieleza kwa kirefu namna dhakhalia miaka ya nyuma zilivyoweza kujenga urafiki, udugu na mshikamano kati ya wanafunzi kutoka sehemu mbali za visiwa vya Unguja na Pemba halikadhalika kuondoa tofauti zilizokuwepo kabla ya Mapinduzi ya mwaka 1964.

“Dakhalia zilikuwa na mchango mkubwa katika kuondoa tofauti na kasumba zilizopandikizwa na wakoloni dhidi ya wananchi…zilikuwa daraja muhimu la kuwakutanisha na kuwaunganisha watu wa mashamba na mijini na baina ya watu wa Unguja na Pemba” Dk. Shein alieleza.

Aliongeza kuwa katika dakhalia hizo wanafunzi waliishi kwa kuheshimiana na kusaidiana wakiwa kitu kimoja na hivyo kuung’oa kabisa ubaguzi na ndio maana kuna uhusiano mkubwa kati ya watu wa Unguja na Pemba kutokana na sera ya elimu iliyotilia mkazo kuchanganya wanafunzi kutoka visiwa hivyo viwili.

Hata hivyo, alibainisha kuwa mafanikio katika ujenzi wa skuli za sekondari na vyuo katika maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba katika miaka ya tisini yalipunguza idadi ya wanafunzi wanaohitaji kukaa dakhalia kwa kuwa wengi walipata fursa za kuendelea na masomo yao katika maeneo wanayotoka.

“Lazima nikiri kuwa mafanikio haya ambayo yamepelekea kupunguza idadi ya wanafunzi katika dakhalia yametunyima fursa muhimu ya kuimarisha uhusiano baina ya wanafunzi wa sehemu mbali mbali za Unguja na Pemba” Dk. Shein alieleza na kusisitiza kuwa serikali italiangalia upya suala hilo.

Wakati huo huo, katika hotuba yake hiyo Dk. Shein ameitaka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kuimarisha mtaala wa mafunzo ya ufundi ili wanafunzi wanaomaliza vyuo hivyo waweze kujiajiri na kuajirika.

Dk. Shein aliueleza uongozi wa Wizara hiyo kuwa amepata taarifa za kuwepo malalamiko kutoka kampuni nyingi kutoka nje zinazofanyakazi za ujenzi Zanzibar kuwa zinapata shida kuajiri mafundi wenye ujuzi, vyeti na uwezo wa kufanya kazi za  useramala.
“Hizi si habari njema. Lazima tushirikiane katika kutatua changamoto hii, hasa tukizingata Zanzibar ilikuwa inasifika kwa kuwa na maseramala wazuri” Dk. Shein alisisitiza.
Dk. Shein aliwahimiza wanafunzi wa vyuo vya ufundi kuongeza bidii katika masomo yao ili watakapomaliza waweze kuamua ama kuajiriwa au kujiari na kufafanua kuwa hivi sasa kuna mahitaji makubwa ya masomo ya ufundi Tanzania nzima.
Katika maelezo yake mafupi kumkaribisha mgeni rasmi, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Mheshimiwa Riziki Pembe Juma alikiri kuwa sekta ya elimu ina changamoto nyingi lakini alieleza kutiwa moyo na jitihada binafsi za Mheshimiwa Rais katika kushughulikia masuala ya elimu.

“Kila unapokwenda na kuiangalia sekta hii ina changamoto nyingi lakini sisi watumishi wa wizara tunapata faraja kuona kila wakati tuko nawe kushughulikia changamoto hizo” alisema Waziri huyo.
Aliwataka wanafunzi wa kike katika skuli hiyo ya ufundi kuongeza bidii baada ya kupata dakhalia hiyo mpya na ya kisasa ambayo ina uwezo wa kuchukua wanafunzi 72.  Dk. Shein yuko kisiwani Pemba kwa ziara ya siku tano kukagua na kuhimiza shughuli za maendeleo.

No comments:

Post a Comment