Friday 15 January 2016

k5
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa, akizungumza na Wadau wa Sekta ya Ujenzi kuhusu Kuungana na Kushirikiana katika kuboresha Miundombinu hapa nchini katika Hoteli ya Kilimanjaro jijini Dar es Salaam.
k6
Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Eng.Joseph Nyamhanga akizungumza kuhusu fursa za Uwekezaji katika Sekta ya Miundombinu hapa nchini katika Mkutano huo uliyohusisha sekta binafsi na Serikali kuhusu namna ya kuboresha sekta ya Miundombinu.
k7
Naibu Waziri wa Miundombinu wa Japan Koji Yonetani akizungumza katika Warsha hiyo na kusema nchi yake iko tayari kushirikiana na Tanzania katika kuboresha Miundombinu hapa nchini.
k9
Watendaji na Wadau wa Sekta ya Ujenzi wakifuatilia mada zilizowasilishwa katika Mkutano wa Wadau wa Sekta ya Serikali na Binafsi kuhusu Ubora wa Miundombinu nchini.
k8
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa (Wa kwanza kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na Naibu Waziri wa Miundombinu wa Japan Koji Yonetani(Wa pili kulia) pamoja na Naibu Waziri Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng.Edwin Ngonyani (Wa Pili kushoto).

Na Kalonga Kasati
 
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amewataka wadau wa Sekta ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kushirikiana na wakezaji kutoka nchini Japan katika kuendeleza miradi mbalimbali ya ujenzi, usafirishaji na mawasiliano nchini.
 
Akizungumza jijini Dar es salaam katika mkutano uliowakutanisha wadau wa sekta hiyo kutoka Nchini Japan na Tanzania, Waziri Mkuu Majaliwa amesema ushirikiano huo utaleta tija kwa taifa kwani wadau wa Sekta hiyo wataweza kujifunza masuala mengi kutoka kwa wataalam hao.
“China na Japan ni moja ya nchi zenye Wakandarasi wengi na wazoefu katika sekta ya ujenzi, kushirikiana nao kutaongeza ushindani na kupelekea kupata fursa ya uwekezaji ndani na nje ya nchi, amesema Waziri Mkuu.

 
Waziri Mkuu Majaliwa ameyataka Makampuni yote yenye miradi ya ujenzi nchini kufanya kazi Vizuri na kumaliza kwa wakati katika kipindi hiki ili kuendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano.
Amesema fursa ipo kwa Kampuni kutoka Nje ya nchi kufanya kazi na Kampuni za ndani kwa lengo la kupata Zabuni ndani na nje ya nchi, mara zinapotangazwa.
“Kutokana na uchumi wa Tanzania kukua kwa kasi, hatuna budi Makandarasi wetu kuungana na kufanya kazi kwa ushirikiano na wenzenu kutoka nje ili kupata maendeleo katika Sekta hii”, Alisisitiza Waziri Mkuu.

 
Naye, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani kwa niaba ya Waziri, Prof. Makame Mbarawa amewaomba Wawekezaji, Wakandarasi na wadau wa Sekta ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kutumia fursa hiyo, kuungana na kutengeneza kampuni za ubia baina ya nchi hizo mbili ili kuweza kujenga miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.
“Tumieni fursa hii kupata elimu na uzoefu na hata kuunganisha Makampuni kwani wenzetu wa Japan wana uzoefu mkubwa na maendeleo katika Sekta hii, ukilinganisha na sisi”, alisema Naibu Waziri.

 
Naibu Waziri huyo ameongeza kuwa kupitia mkutano huo Wakandarasi nchini wataweza kujifunza Njia za kisasa ambazo zitasaidia katika kuboresha Sekta ya Miundombinu na Mawasiliano.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Miundombinu kutoka Wizara ya Ardhi, Miundombinu, Usafirishaji na Utalii wa Japan, Bwana Takatoshi Nishiwaki, ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kukubali kushirikiana katika kuendesha mkutano huo na wadau wa sekta ya ujenzi wenye lengo la kubadilishana ujuzi na teknolojia kuhusu Miundombinu bora.

 
Mkutano huo wa siku moja umewashirikisha Wawekezaji, Wakandarasi na na Wafanyabiashara kutoka nchini Japan na Tanzania walio katika Sekta ya Miundombinu na Mawasiliano.

No comments:

Post a Comment