Sunday 31 January 2016

WAZIRI MAKAMBA ATOA MSAADA MABATI 300 KWA WAHANGA AMBAO NYUMBA ZAO ZILIZOEZULIWA NA UPEPO JIMBONI KWAKE.

93
Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshugulikia Muungano na
Mazingira,January Makamba ametoa msada wa mabati 300 kwa wananchi
ambao nyumba zao zimeezuliwa na upepo uliosababishwa na mvua kubwa
iliyonyesha maeneo mbalimbali jimboni humo.
Nyumba hizo zilikuwa 40 ikiwemo  Kanisa  na Msikiti zimeezuliwa mapaa
katika kijiji cha Msamaka kilichopo wilayani Bumbuli kufuatia Mvua
kubwa iliyoambatana na upepo kunyesha.
Mvua hiyo imesabisha  kaya  hizo  kukosa  mahali pa kuishi , huku
wengi wa  waathirika  wakipewa hifadhi  kwenye  nyumba  za majirani
zao.
Akizungumza  na waandishi wa habari hapo Jana Afisa Mtendaji wa kijiji
cha Msamaka Mbazi Shemhando alisema kuwa tukio hilo lilitokea mnamo
January 27 mwaka huku saa kumi jioni.
Alitaja sehemu zilizo athirika zaidi  kuwa  ni Vitongoji vya Kwemchaa,
Nazareti,CCM, Kwakorosi pamoja na kitongoji cha Kwamingojo ndio
vimeweza kuathirika na maafa hayo.
Hata hivyo aliongeza kuwa waathirika watukio hilo Kwa sasa
wamehifadhiwa kwenye nyumba za Jirani wakati utaratibu mwingine wa
kuwasaidia ukiendelea kuwekwa.
Akikabidhi msaada huo Makamba alisema kuwa kutokana na tukio hilo
anatanguliza msaada huo kwanza wakati akiendelea kutafuta msaada
zaidi.
“Nimejikusanya Kwa hiki kidogo ili kiweze kusaidia pale penye uhitaji
Kwa haraka wakati tukiendelea na utaratibu  mwingine” alisema Makamba
Makamba   aliwataka  wananchi  wote  kupanda  miti ili kuepuka  upepo
mkali  unaosababishwa  na  mvua  zinazoendelea kunyesha  katika
maeneo tofauti

Suala LaAda Elekezi Kuhusisha Wadau Wote – Waziri Mkuu

3
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizunguza katika ibada ya kumuingiza kazini Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Frederick Shoo iliyofanyika kwenye kanisa Kuu la KKKT mjini Moshi Januari 31, 2016.
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema suala la ada elekezi linaendelea kufanyiwa kazi na Serikali na likifika hatua nzuri litahusisha wadau wote ili kupata maoni yao.

Ametoa ahadi hiyo leo mchana (Jumapili, Januari 31, 2016) wakati akizungumza na mamia ya waumini walioshiriki ibada ya kumuingiza kazini Mkuu Mpya wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk. Fredrick Onaeli Shoo iliyofanyika kwenye usharika wa Moshi Mjini, Dayosisi ya Kaskazini.

Waziri Mkuu Majaliwa ambaye alihudhuria ibada hiyo kwa niaba ya Rais Dk. John Pombe Magufuli alikuwa akijibu baadhi ya hoja zilizotolewa na Dk. Shoo ambaye alisema kama Serikali inataka kuondoa ada elekezi haina budi kuziimarisha shule zake ili ziwe kama zilivyokuwa zamani.
Akijibu hoja kuhusu miundombinu ya reli, Waziri Mkuu alisema Serikali imeamua kufufua Miundombinu hiyo na kwamba hivi sasa inafanya mapitio ili kujua gharama halisi kwa maeneo husika. Alisema Serikali imepanga kuanza na maeneo manne ambapo la kwanza alilitaja kuwa ni reli ya kutoka Dar es Salaam – Mwanza – Tabora – Kaliua – Mpanda hadi Karema.

“Eneo la pili ni reli ya ukanda wa Kaskazini ambayo itatoka Dar es Salaam – Tanga – Arusha hadi Musoma. Ya tatu ni ya kutoka Tabora – Kahama – Kigali (Rwanda) na kuishia nchini Burundi Ambayo tunataka isaidie kusafirisha mizigo kutoka bandari ya Dar es Salaam. Reli ya nne ni ile ya kutoka Mtwara kupitia Tunduru kwenda Songea hadi Mbamba Bay,” alisema.

Kuhusu ulinzi wa demokrasia ndani ya Bunge, Waziri Mkuu alisema anakubaliana na Askofu Dk. Shoo juu ya mihimili yote mitatu kuheshimiana na kwamba ameshukuru kwamba ameonya juu ya lugha zinazotumika ndani ya Bunge.

“Bunge ni eneo linaloweza kujenga jamii mpya kwa sababu Bunge ni kioo na jamii ya Watanzania inatuangalia sisi tuliomo mle. Ni vema tuwe na lugha nzuri, tabia njema na hata jinsi tunavyovaa ili wanaotuona wapate hamu ya kuiga,” alisema.

Kuhusu ombi la kuibuliwa upya mchakato wa Katiba mpya, Waziri Mkuu alisema suala hilo amelichukua na anaenda kulifanyia kazi. “Nakuhakikishia Baba Askofu ushauri ulioutoa kwa Serikali tumeupokea,” alisisitiza.

Mapema, akitoa hotuba yake, Askofu Mkuu Dk. Shoo alisema Bunge ni nyumba ya demokrasia kwa hiyo jamii inatarajia kuona hoja zikijadiliwa kwa haki na amani badala kutumia ubabe na mabavu au nguvu ya dola.

“Nimewaona baadhi ya wabunge mko hapa… hili ninalolisema ni lenu na linawahusu ninyi na spika wenu. Wabunge tunzeni heshima yenu na Mungu awasaidie kulitimiza hilo. Wewe Waziri Mkuu ni Msimamizi wa shughuli za Serikali bungeni kwa hiyo una kazi ya kusimamia. Kila mhimili unapaswa utunze heshima yake…,” alisisitiza.

Kuhusu Katiba mpya, Askofu Dk. Shoo alisema Watanzania wengi wana kiu ya kuona mchakato huo ukiibuliwa upya na kukamilishwa ili nchi ipate Katiba mpya yenye kukidhi kiu ya watu wake na inayoheshimu matakwa ya wengi.

“Mchakato huo ukianza utumike kuganga majeraha yote yaliyopita. Tukifanya hivyo tutakuwa tumeisaidia Serikali ya Awamu ya Tano kuipelekea nchi yetu kule ambako imedhamiria. Yote yanawezekana tukitaka na tukipenda,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Askofu ambaye amemaliza muda wake wa kuliongoza kanisa hilo, Dk. Alex Malasusa alisema anamshukuru Mungu kwa kupata kibali cha kushuhudia Mkuu mpya wa kanisa hilo akipokea kijiti cha uongozi kutoka kwake.

“Si kwa akili na uwezo wangu bali ni kwa uweza wa Mungu kwamba nimeweza kuishuhudia siku ya leo. Ninamuomba Mungu akusaidie kuongoza kanisa hili, akusaidie kukemea na kuonya kwa upole. Najua Mungu atakupunguzia hata marafiki kwa sababu ya matamshi utakayokuwa ukiyatoa, lakini si wewe bali ni uweza wa Bwana na roho mtakatifu anayekuongoza,” alisema.
Aliahidi kuendelea kuwaombea Rais Magufuli pamoja na Waziri Mkuu Majaliwa katika majukumu waliyonayo. “Msiogope kwa ajili ya majukumu mliyopewa, msihofu tunaendelea kuwaombea kwa sababu tuko pamoja na sisi ni sehemu ya utumishi wa Taifa,” alisema.

Rais Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Rais Mstaafu Mkapa

2Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana Na Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Mheshimiwa Benjamin Wiliam Mkapa. Rais Dkt. Magufuli Alikwenda kumsalimia Rais mstaafu Mkapa nyumbani kwake Masaki jijini Dar es Salaam Mwishoni mwa wiki

No comments:

Post a Comment