Thursday 28 January 2016

Elimu ya sheria Dar kuanza Januari 31

katanga
 
Na Kalonga Kasati

Uongozi wa Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na wadau wa sheria wanatarajia kutoa elimu ya sheria katika viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es salaam.
Hayo yamesemwa na Mtendaji Mkuu wa Mahakama Hussein Kattanga alipokuwa akisisitiza wananchi kujitokeza kwa wingi kupata elimu hiyo.
‘’Natoa wito kwa wananchi kuhudhuria maadhimisho ya siku ya sheria nchini yanayoashiria kuanza mwaka mpya wa shughuli za mahakama”Alisema Kattanga.
Kauli mbiu katika maadhimisho hayo ya mwaka huu ni “huduma za haki kumlenga mwananchi:wajibu wa mahakama na wadau”
Ameongeza kuwa,miongoni mwa wadau watakaoshiriki katika kutoa elimu ya sheria ni pamoja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,Taasisi ya Sheria kwa Vitendo Tanzania (Law School), Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Chama cha Wanasheria Wanawake (TAWLA),Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora,Takukuru pamoja na Polisi.
Aidha Kattanga amesema kwamba wadau hao watatoa huduma za kisheria na kimahakama kwahiyo wananchi wenye mashauri ya muda mrefu,malalamiko yoyote na mapendekezo ya uboreshaji wa utendaji kazi wa mahakama wafike na kuonana na waheshimiwa Majaji, Mahakimu,Wasajili na Watendaji wa Mahakama.
Maadhimisho hayo hufanyika nchini kila mwaka katika wiki ya kwanza ya mwezi wa pili ambapo kwa Jiji la Dar es salaam inatarajia kufanyika tarehe 31 Januari hadi Februari 3.

Serikali kuendelea kujenga barabara zaidi kwa kiwango cha lami

UJ1
Naibu Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano  Mhe. Mhe Eng Godwin Ngonyani akijibu maswali ya wabunge katika kikao cha Bunge la 11linaloendelea Mjini Dodoma.

Na Kalonga Kasati
Serikali imeahidi kuendelea na ujenzi wa barabara katika maeneo tofauti nchini kwa kiwango cha
lami ili kutatua adha kubwa ya Ubovu wa barabara ulipo katika maeneo mengi nchini.
 
Hayo yamesemwa leo Mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano  Mhe. Eng Godwin Ngonyani akijibu maswali ya wabunge waliouliza kuhusu mpango wa serikali kuboresha barabara zilizopo na kujenga mpya ili kukabiliana na adha ya ubovu wa barabara nchini.
 
Akijibu swali la Mhe Richard Mganga Ndassa Mbunge wa Sumve (CCM) lililohitaji  ufafanuzi wa serikali ni lini ujenzi wa barabara ya Magu-Bukwimba –Ngudu-Hungumalwa itajengwa kwa kiwango cha lami, Mhe Eng Godwin Ngonyani amesema katika  mwaka wa fedha 2014/15 na 2015/16 serikali ilitenga jumla ya shilling millioni 200 kwa ajili ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 70 na taratibu za kumtafuta Mhandisi Mshauri zinaendelea na baada ya kukamilika kwa usanifu na kupata gharama za Mradi huo, Serikali itatafuta fedha za kuanza ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami.
 
Aidha akijibu pia swali la Mhe Fredy Atupele Mwakibete  Mbunge wa Busokelo (CCM) Aliyehitaji kujua ni lini barabara ya Katumba-Mbambo-Tukuyu yenye urefu wa Kilometa 82 inayoanzia Katumba(RDC) kupitia Mpombo,Kandete,Isange,Lwanga, Mbambo (BDC) hadi Tukuyu (RDC) itajengwa kwa kiwango cha lami.
 
Akijibu swali hilo, Mhe. Eng Godwin Ngonyani amesema kuwa Serikali kupitia  Wakala wa Barabara (TANROADS) kwa kutambua umuhimu wa barabara hii, katika mwaka wa fedha 2009//10 Serikali ilianza maandalizi ya ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami na Ambapo upembuzi yakinifu na sanifu wa kina ulikamilika na baadae Serikali iliamua kujenga kilometa 10 ambapo mwezi April,2014 Wakala wa Barabara na kampuni ya CICO ilijenga barabara hiyo kuanzia Lupaso hadi Buseji,Wilayani Busokelo.
 
Serikali kupiti Wakala wa Barabara (TANROADS) inaendelea na ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami katika Kata, Wilaya na Mikoa mbalimbali nchini  ili kukabiliana na adha ya Ubovu wa barabara ambao umesababisha watu kukosa mawasiliano baina ya maeneo.

No comments:

Post a Comment