Sunday 17 January 2016

mwenyekiti
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Nnauye (mwenye suti ya kijivu) akimpongeza mwenyekiti mpya wa FK aliyeteuliwa hivi karibuni Bw. Ahmed Michuzi ambaye pia ni Mmiliki  wa Blogu ya Jiachie na Mkurugenzi Mwandamzi  wa Michuzi  Michuzi Media alikuwa mwanachama mwaminifu wa FK, tukio hilo limetokea leo Wakati alipokutana naye kwenye ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo  jijini Dar es salaam
bona





Mbunge wa Jimbo la Segerea kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) Mh. Bonna Kalua amesema kuwa hakuna nyumba ya mwananchi itakayobomolewa ambayo imejengwa katika umbali unaohitaji 
kisheria wa mita 60 kutoka mtoni.
Mh.Kalua alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es salaam wakati akizungumza na wananchi wa Karakata kwenye mkutano wa hadhara.
Aidha alitoa wito kwa wale ambao wamejenga ndani ya mita 60 na nyumba zao zimewekewa X kujiorodhesha majina yao kwa Wenyeviti wa mitaa ili wamfikishiea Ofisi kwake kwa ajili ya kulifuatilia jambo hilo kwa ukaribu na hatimaye wapate haki zao.
Mh.Bonna aliwatahadharisha wananchi kutodanganywa na watu wanaowachangisha fedha kwa kigezo cha kufungua kesi mahakamani kuwa ni uongo na hawana nia nzuri kwa wananchi kwa sababu kesi ya bomoa bomoa tayari ilishafunguliwa kwa niaba ya nchi nzima.
Aliwataka wananchi kuwa wavumilivu mpaka hapo shauri lilipo mahakamani litakapotolewa tamko .

SERIKALI YALIFUTA GAZETI LA MAWIO

nape1
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Nnauye (mwenye suti ya kijivu) akiwaeleza Waandishi wa Habari (hawapo pichani) juu ya Uamuzi wa Serikali wa kulifuta Gazeti la MAWIO katika Daftari la Msajili wa Magazeti mara alipokutana na waandishi hao 17 Januari 2016 katika Ukumbi wa Idara ya Habari uliopo jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari, Bw. Assah Mwambene, wa pili kulia ni Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia usajili wa Magazeti, Bw. Raphael Hokororo na anayemfuatia ni Mwanasheria wa Wizara Bw. Patrick Kipangula
nape2
Baadhi ya Waandishi wa Habari wakifuatilia taarifa ya Serikali toka kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Nnauye (hayupo pichani) juu ya Uamuzi wa Serikali wa kulifuta Gazeti la MAWIO katika Daftari la Msajili wa Magazeti mara alipokutana na waandishi hao 17 Januari 2016 katika Ukumbi wa Idara ya Habari uliopo jijini Dar es Salaam.
 

Na kalonga kasati
 
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeamua kulifuta kutoka katika Daftari la usajili wa magazeti, gazeti lijulikanalo kama “MAWIO”.
 
Amri ya kulifuta Gazeti hilo imetolewa leo na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Nnauye wakati alipokutana na Waandishi wa Habari katika Ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) uliopo Jijini Dar es Salaam.
 
Mhe. Nnauye amesema kuwa kupitia Tangazo la Serikali Na. 55 lililotolewa tarehe 15 Januari, 2016 Serikali imelifuta Gazeti hilo ikiwa ni uamuzi uliotolewa kwa mujibu wa Sheria ya Magazeti Sura ya 229, kifungu 25(1).
 
Alieleza kuwa, hatua ya kulifuta gazeti hilo inazuia pia gazeti la Mawio kuchapishwa katika njia nyingine yoyote ikiwa ni pamoja na mitandao (Online publication) kwa mujibu wa Sheria ya Mawasiliano ya Kieletroniki na Posta Sura ya 306.
 
‘’Serikali kwa masikitiko makubwa, imechukua uamuzi huu kutokana na mwenendo wa uandishi wa gazeti hilo usioridhisha wa kuandika na kuchapisha habari zenye mwelekeo wa uchochezi na kuhatarisha amani, utulivu na usalama wa nchi yetu’’, alisema Nnauye.
 
Aidha, alifafanua kuwa hatua hiyo ya kulifuta gazeti hilo imechukuliwa baada ya Msajili wa Magazeti kufanya juhudi kubwa za muda mrefu kuanzia Juni, 2013 hadi Januari,  2016  kumtaka Mhariri wa gazeti hilo kubadili aina ya uandishi wa habari na makala katika gazeti lake, bila mafanikio.
 
‘’Msajili wa magazeti kwa juhudi zake alifanya mawasiliano na Mhariri wa gazeti hilo mara nane kwa lengo la kutaka afanye marekebisho ya  mtindo wa kutoa habari zake lakini mhariri wa gazeti hilo hakuzingatia ushauri mzuri aliopewa na Msajili wa Magazeti,
Ninatoa wito kwa wamiliki, wahariri, waandishi na watangazaji wa habari kuzingatia sheria, Kanuni na taratibu za taaluma ya uandishi wa habari ambazo zikizingatiwa hakutakuwa na migogoro yoyote. Aidha Serikali inasisitiza kwamba inaheshimu uhuru wa vyombo vya habari unaozingatia maadili, weledi na Sheria za nchi na kwamba Serikali itaendelea kushirikiana navyo’’ alisisitiza Mhe. Nnauye.
 
Katika hatua nyingine, Waziri nape alitoa pongezi kwa Vyombo vyote vya habari nchini vinavyozingatia maadili, weledi na Sheria zinazosimamia taaluma ya habari na sheria nyingine za nchi. 
 
‘’Kwa namna ya pekee Serikali inawapongeza wamiliki na wahariri wa vyombo vya habari ambavyo vinapofanya makosa vikielekezwa hujirekebisha na kutoa ushirikiano kwa Serikali na pia kubadili mwenendo wao; hawa ni pamoja  na wahariri wa magazeti ya; Mwananchi Tanzania, Mtanzania, The East African, Magazeti ya Daily News na Habari Leo, Uhuru na mengineyo’’, alisema Mhe. Nnauye.

HATUA AMBAZO ZIMECHUKULIWA DHIDI YA STANBIC BANK TANZANIA LIMITED KUHUSU USHIRIKI WAKE KUWEZESHA MKOPO WA SERIKALI WA DOLA ZA KIMAREKANI MILIONI 600

mpa01
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt Philip Mpango (kushoto) akiongea na waandishi wa habari (hawamo pichani)jijini Dar es Salaam, kuhusu hatua zilizochukuliwa na Serikali dhidi ya Benki ya Stanbic Tanzania kutokana na ushiriki wake katika kuwezesha mkopo wa Serikali wa Dola za Kimarekani Milioni 600 na Kulia kwake ni Naibu Gavana  wa Benki Kuu ya Tanzania(BOT) Bw. Lila Mkila.
mpa1
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt Philip Mpango (katikati)  akitoa tamko kwa waandishi wa habari (hawamo pichani) jijini Dar es Salaam, kuhusiana na kusudio la kuitoza Benki ya Stanbic faini ya shilingi bilioni 3.  Kulia kwake ni Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali Dkt. Servicius Likwelile na Kushoto kwake ni Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) Bw. Lila Mkila.
………………………………………………………………………………………
Utangulizi
Mwezi Julai 2013, Benki Kuu ya Tanzania kupitia ufuatiliaji wa kawaida wa shughuli za mabenki iligundua matatizo yaliyohusiana na hasara itokanayo na mikopo na pia kuacha na kuondolewa kazini kwa viongozi waandamizi wa Stanbic Bank Tanzania Limited (Stanbic) katika muda mfupi. Kutokana na hilo, Benki Kuu iliamua kufanya ukaguzi wa kulenga (Targeted Examination) katika benki hiyo. Ukaguzi huo ni kwa mujibu wa mamlaka iliyopewa Benki Kuu chini ya Kifungu 47 cha Sheria ya Benki Kuu ya mwaka 2006 na Kifungu 31 cha Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006.
Matokeo ya Ukaguzi wa Benki Kuu
 Katika ukaguzi huo, wakaguzi wa Benki Kuu, pamoja na mambo mengine walibaini miamala ya kutia shaka iliyohusu malipo kwa kampuni ya kitanzania ya Enterprise Growth Market Advisors (EGMA). Kampuni ya EGMA ilihusika katika uwezeshaji wa upatikanaji wa Mkopo kwa Serikali ya Tanzania ambapo Standard Bank Plc (ambayo kwa sasa inajulikana kama ICBC Standard Bank) na Stanbic Bank Tanzania Limited kwa pamoja walikuwa “Mwezeshaji Mkuu” (Lead Arranger). Malipo hayo kwa kampuni ya EGMA yalikuwa yamefanyika kinyume na taratibu za kibenki na yalihusisha uongozi wa benki ya Stanbic. Jumla ya malipo yalikuwa ni kiasi cha dola za kimarekani milioni 6, na zililipwa katika akaunti ya EGMA na kutolewa kwa muda mfupi kwa njia ya fedha taslimu (cash) ambayo ni nje ya taratibu za kibenki.
Taarifa ya ukaguzi huo iliwasilishwa kwa benki ya Stanbic kwa mujibu wa taratibu, na Benki Kuu iliiagiza Bodi ya Wakurugenzi ya benki hiyo kuchukua hatua stahiki za kurekebisha kasoro zilizoonekana. Aidha, benki ya Stanbic iliagizwa kutoa taarifa kwa Kitengo cha Financial Intelligence Unit (FIU) kilichopo Wizara ya Fedha na Mipango kuhusiana na miamala hiyo yenye mashaka katika akaunti ya EGMA kama Sheria ya Kuzuia Utakatishaji wa Fedha Haramu ya mwaka 2006 (The Anti-Money Laundering Act, 2006) inavyoelekeza. Benki ya Stanbic ilitekeleza maagizo na kutoa taarifa FIU kuhusu miamala inayotiliwa shaka.
Mnamo 29 Septemba 2015, Benki Kuu ilipokea barua toka Idara ya Serikali ya Uingereza inayohusika na Upelelezi wa Makosa ya Kugushi na Rushwa (Serious Fraud Office – SFO) ikiiomba Benki Kuu ruhusa ya kutumia ripoti yake ya ukaguzi kama ushahidi katika kesi dhidi ya Standard Bank Plc ambayo ilikuwa ni mshirika wa Stanbic Bank Tanzania Limited katika kuwezesha mkopo wa dola za kimarekani milioni 600 kwa Serikali na kwamba ripoti hiyo ingekuwa wazi kwa umma. Benki Kuu iliijibu SFO kuwa kwa mujibu wa Sheria ripoti za Benki Kuu zinatolewa tu kwa benki au taasisi ya fedha inayohusika, hata hivyo, Benki Kuu haikuwa na pingamizi kwa SFO kutumia taarifa za ripoti hiyo kwa kuzingatia chanzo cha ripoti hiyo.
Hatimaye, Standard Bank Plc ilikubali makosa na ilitozwa faini ya jumla ya dola za kimarekani milioni 32.20, ambapo kiasi cha dola za kimarekani milioni 7 zinalipwa kwa Serikali ya Tanzania (dola za kimarekani milioni 6 zilikuwa ni fidia na dola za kimarekani milioni 1 ni riba).
Kwa kuzingatia mapungufu ya kufanya miamala iliyohusisha EGMA na pia kutokuweka taratibu madhubuti za udhibiti wa ndani, na kwa kuzingatia Kifungu 67 cha Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006, Benki Kuu imeiandikia benki ya Stanbic barua ya kusudio la kuitoza faini ya shilingi bilioni 3. Sheria inaitaka benki ya Stanbic kutoa utetezi katika kipindi cha siku ishirini (20) ambacho kitaisha tarehe 30 Januari 2016. Endapo Benki Kuu haitaridhika na utetezi, benki ya Stanbic italazimika kulipa faini hiyo.
Hitimisho
 Benki Kuu imechukua hatua hizo kama onyo kwa benki ya Stanbic na ili iweze kuwa makini katika kuhakikisha kuwa shughuli zake zinaendeshwa kwa mujibu wa taratibu za kibenki na kuzingatia Sheria.
Aidha, hatua hii ni onyo kwa mabenki na taasisi za fedha zisijihusishe na makosa ya aina hii ambayo ni kinyume cha taratibu za kibenki na ni uvunjaji wa Sheria za nchi. Hatua kali zitaendelea kuchukuliwa kwa benki au taasisi ya fedha yoyote itakayobainika kwenda kinyume na taratibu za kibenki na Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006.

No comments:

Post a Comment