Kocha wa Simba, Joseph Omog, amesema mchezo wa leo wa kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) Dhidi ya African Sports ni muhimu kwao kushinda ili kujenga molali kuelekea mchezo wao wa Ligi Kuu dhidi ya Yanga utakaochezwa Februari 25 jijini Dar es Salaam.
Simba leo inavaana na African Sports kwenye raundi ya sita ya michuano hiyo.
mchezo huo awali ulikuwa umepangwa kuchezwa Machi Mosi lakini Shirikisho la soka nchini (TFF) uliurejesha nyuma.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Omog, amesema mchezo wa leo ni muhimu kwao kwa kuwa wamepania kufanya vizuri kwenye kila mashindano wanayoshiriki.
"Utakuwa mchezo mzuri, nafikiri ushindi ndicho tunachotakiwa kukifikiria, ushindi utatuweka kwenye molali kuelekea kwenye mchezo unaofuata mbele yetu, hilo ndio jambo la muhimu," alisema Omog.
Amesema amefanyia maandalizi ya kutosha kuelekea mchezo wa leo utakaochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru.
"Naamini wachezaji wangu wataendeleza kile walichokifanya kwenye michezo iliyopita," aliongezea kusema Omog.
Baada ya mchezo wa leo, michezo ya raundi hiyo ya sita itaendelea tena Februari 24 kwa michezo minne kuchezwa.
Kwa mujibu wa ratiba ya TFF, michezo ya siku hiyo itashushudia Madini FC ya Arusha ikicheza na JKT Ruvu jijini Arusha wakati Kagera Sugar itaumana na Stand United kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Mjini Songea, wenyeji Might Elephant itaumana na Ndanda FC wakati washindi wa pili wa msimu uliopita, Azam FC yenyewe itaumana na Mtibwa Sugar kwenye uwanja wa Azam Complex, mchezo huo umepangwa kuanza saa 1:00 usiku.
Michuano hiyo pia itaendelea Februari 26 wakati 'ndugu' wa mkoa mmoja, Mbeya City na Tanzania Prisons watakapoonyeshana ubabe kwenye Uwanja wa Sokoine.
Mabingwa watetezi, Yanga wenyewe wamepangiwa kucheza Machi 7 dhidi ya Kiluvya United kwenye Uwanja wa Taifa.
No comments:
Post a Comment