Sunday 26 February 2017

Rais wa FIFA azindua ujenzi wa Hoteli Rwanda

Rais wa FIFA Gianni Infantino amezindua ujenzi wa Hoteli ya chama cha soka cha Rwanda kwa gharama za FIFA.
Bwana Infantino ameweka jiwe la msingi katika ujenzi wa Hoteli hiyo inayojengwa mjini Kigali karibu na uwanja wa taifa Amahoro.
FIFA tayari imeshatoa kitita cha dolla za Marekani milioni 4,1 kwa ajili ya ujenzi wa Hoteli hiyo huku zikiwa zimesalia dolla milioni 2.
Mwenyekiti wa chama cha soka cha Rwanda FERWAFA Bwana Nzamwita De Gaule, amesema Hoteli hiyo itatumiwa kupokea timu mbali mbali kutoka ng'ambo zinazokwenda kucheza nchini Rwanda.
"Hii Hoteli itakuwa na vyumba 48 vikiwemo vyumba 4 vitakavyojengwa kwa ajili ya walemavu.itakuwa na uwezo wa kupokea timu mbili za taifa kwa wakati mmoja au vilabu 3 kwa wakati mmoja".Amesema mkuu wa chama cha soka cha Rwanda.
Amesisitiza mradi wa Hoteli hiyo ulilenga kukiwezesha chama cha soka cha Rwanda kuwa na uwezo wa kupata pesa za kuendeleza soka nchini Rwanda.
"Tumekuwa tukigharamia kulipia hoteli timu zinazokuja kucheza hapa Rwanda katika mashindano mbali mbali ,hata timu yetu ya taifa kuipeleka katika hoteli nyingine ilikuwa gharama kubwa.Sasa mradi huu utatusaidia na kuturuhusu kuingiza pesa za kuendeleza soka letu."
Rais wa FIFA Gianni Infantino amesema aliidhinisha kugharamia mradi wa ujenzi wa Hoteli hii kwa sababu aliutambua kama mradi mzuri wa kusaidia chama cha soka cha Rwanda kwa sababu una malengo mazuri ya kuendeleza soka ambayo pia ndiyo malengo yake.
FIFA itakuwa na mkutano wa kamati tendaji mwezi wa 10 mwaka huu nje ya makao yake mjini Zurich,na Rwanda tayari imekwishaomba kuwa mwenyeji wa mkutano huo.Kuhusu hilo Rais wa FIFA amesema uwezekano upo:
"Mpango ndio huo,lakini bado tunalijadili hilo.Tunaitambua Rwanda kutakuwa na mazungumzo zaidi kuhusu hilo" amesema Infantino.


Akiwa ziarani nchini Rwanda Rais huyo wa FIFA amechukua fursa ya kuangalia mechi ya ligi kuu ya soka ya Rwanda baina ya Rayon Sports na Police FC iliyoshuhudia sare ya kufungana magoli 2-2 kwenye uwanja wa taifa Amahoro.

No comments:

Post a Comment