Tuesday 28 February 2017

Serikali imesema itaendelea kuwajengea uwezo wanawake ili kuweza kushiriki katika shughuli za matengenezo na ukarabati wa miundombinu ya barabara

1
Meneja wa Wakala wa Barabara Mkoa wa Mwanza (Tanroads) Eng. Marwa Rubirya (wa pili kushoto) akizungumza na wawakilishi wa vikundi vya wanawake wanaoshiriki mafunzo ya ukarabati na matengenezo ya barabara kwa kutumia teknolojia stahiki ya nguvu kazi, Jijini Mwanza.
2
Mratibu Kitengo cha ushirikishaji wa wanawake katika kazi za barabara kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Ujenzi) Eng. Rehema Myeya (wa pili kulia) akifafanua jambo kwa washiriki wa mafunzo ya ukarabati na matengenezo ya barabara kwa kutumia teknolojia stahiki ya nguvu kazi, Jijini Mwanza kushoto ni Eng. Liberata Alphonce kutoka sekta ya ujenzi na wapili kushoto ni Meneja wa Tanroads mkoa wa Mwanza Eng. Marwa Rubirya.
3
Eng. Liberata Alphonce kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano sekta ya (Ujenzi) wa pili kulia akitoa maelezo kwa washiriki wa mafunzo ya ukarabati na matengenezo ya barabara kwa kutumia teknolojia stahiki ya nguvu kazi, Jijini Mwanza.
4
Mkufunzi wa mafunzo ya kutumia teknolojia stahiki ya nguvu kazi kutoka Chuo cha Teknolojia stahiki ya nguvu kazi Mbeya (ATTI) Eng. Richard Kansimba akifafanua jambo kwa washiriki wa mafunzo ya ukarabati na matengenezo ya barabara kwa kutumia teknolojia stahiki ya nguvu kazi, Jijini Mwanza.
5
Mmoja wa washiriki wa mafunzo ya ukarabati na matengenezo ya barabara kwa kutumia teknolojia stahiki ya nguvu kazi akichangia mada juu ya teknolojia hiyo.
6
Washiriki wa mafunzo ya ukarabati na matengenezo ya barabara kwa kutumia teknolojia stahiki ya nguvu kazi wakifuatilia mada hiyo Jijini Mwanza.

Serikali imesema itaendelea kuwajengea uwezo wanawake ili kuweza kushiriki katika shughuli za matengenezo na ukarabati wa  miundombinu ya barabara kwa kutumia teknolojia stahiki ya nguvu kazi.
Hayo yamesemwa na Meneja wa Wakala wa Barabara Mkoa wa Mwanza (Tanroads) Eng. Marwa  Rubirya wakati akifungua mafunzo ya kozi kwa wanawake wa vikundi vya mikoa ya Kanda ya ziwa jijini Mwanza.
“Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano sekta ya (Ujenzi) imekuwa ikitekekeza sera mbalimbali ikiwemo shughuli za matengenezo yenye kuongeza ushiriki wa wanawake katika kazi za barabara ili waweze kujikwamua kiuchumi”. amesema Eng.Rubirya.
Eng. Rubirya amewataka  wanawake kusijili vikundi vyao kupitia bodi ya usajilibwa Makandarasi nchini (CRB)  ili zabuni za kazi za ukaraba na matengenezo ya barabara zinapotangazwa waweze kukidhi vigezo vya kupata kazi hizo.
Aidha, Eng. Rubirya amewahimiza wakinamama hao kufanya kazi hizo kwa ubora unaotakiwa pindi wapatapo kazi hizo ili barabara hizo ziweze kudumu kwa muda mrefu na kuleta faida kwa wananchi.
Naye  muwezeshaji katika mafunzo hayo Eng. Liberata Alphonce amesema Serikali imelenga kuinua uchumi wa wanawake wenye nia ya kufanya kazi za barabara  kwa vile uchumi wa mwanamke ukiimarika na taifa pia litaimarika.
“Kwa muda mrefu kazi za barabara zimekuwa zikionekana za kiume sasa umefika wakati wa wanawake kushiriki katika kazi hizo kwa vile uwezo tunao.” amesisitiza Eng.Alphonce.
Kwa upande wake Mratibu wa kitengo cha ushirikishaji wanawake katika kazi za barabara Eng. Rehema Myeya amesema Wizara imeona umuhimu wa kutoa mafunzo yatakayowasaidia wanawake kuwa na uwezo wa kufanya kazi za ukandarasi hasa wa barabara hususan matengenezo na ukarabati.
 
“Tumekuwa tukitoa mafunzo haya kwa wanawake katika sehemu mbalimbali  nchini na sasa tupo Mwanza lengo ni kuwafundisha namna ya kufanya kazi hizi za ukandarasi kwa weledi unaotakiwa”. amesema Eng.Myeya.
Teknolojia stahiki ya nguvu kazi inahusisha utumiaji wa rasilimali zilizopo pamoja na kutumia vitendea kazi rahisi na mitambo midogo midogo midogo katika ujenzi na ukarabati wa barabara.
Imetolewa na Kitengo cha habari na Mawasiliano, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

No comments:

Post a Comment