Friday 24 February 2017

Azam FC na Mtibwa waingia vitani leo


Michuano ya Kombe la Shirikisho inatarajia kuendelea leo kwa mabingwa watetezi wa Kombe la Kagame, Azam FC kuwakaribisha Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Azam Complex ulioko Chamazi jijini, Dar es Salaam.
Mechi hiyo ya hatua ya 16 bora inatarajiwa kufanyika kuanzia saa 1:00 usiku.
Kaimu Kocha Mkuu wa Azam FC, Idd Cheche, amesema kuwa kikosi chake kiko imara na amefurahishwa kurejea kwa nahodha John Bocco.
Cheche alisema kuwa baada ya kufanya mazoezi ya zaidi ya wiki moja, kikosi chake kimeiva na kinahitaji kupata ushindi katika mchezo huo ambaye atakayefungwa atakuwa ameondolewa kwenye michuano.
"Tunajua mechi zote dhidi ya Mtibwa si mechi rahisi, tumejiandaa vizuri kupata ushindi na vile vile mchezo huo utatusaidia kuendelea na maandalizi ya kuwavaa Mbabane Swallows ya Swaziland," amesema kiongozi huyo.
Aliongeza kuwa bado nafasi ya kumtumia Bocco katika mechi ya leo ni ndogo kwa sababu ameanza mazoezi mepesi juzi na bado anaendelea na matibabu.

Vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba yenyewe imeshatinga hatua ya nane bora baada ya kuifunga African Lyon bao 1-0 wakati Yanga yenyewe itaikaribisha Kiluvya United na mshindi ataendelea mbele kwenye michuano hiyo.

No comments:

Post a Comment