Sunday 26 February 2017

Malaysia yatangaza uwanja wa ndege kuwa salama baada ya kuuwawa Kim Jong-nam

Maafisa wa usalama wa Malaysia wametangaza kuwa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kuala Lumpur ni salama baada ya kuuawa kwa Kim Jong-nam.
Kim Jong-nam, kaka wa kambo wa kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un aliuawa katika uwanja huo siku 12 zilizopita.
Awali, polisi walipekua jengo husika wakichunguza iwapo kulikuwa na sumu kali iliyotumiwa katika mauaji hayo aina ya VX, au sumu nyingine yo yote.
Mwanamke kutoka Indonesia, aliyekamatwa kwa kuhusika na mauaji ya ndugu wa kambo wa kiongozi wa Korea Kaskazini, anasema alilipwa dola 90, kushiriki katika kile alichofikiri, ni kitendo cha mzaha.
Wanabalozi wa Indonesia waliokutana na Siti Aisyah, wanasema aliwaambia kuwa wanaume wawili, walionekana kama Wakorea au Wajapani, walimpa mafuta yaliyofanana na yale ya mtoto kumpaka usoni mwanamme mmoja.
Mafuta hayo sasa yanafikiriwa yalikuwa na kemikali VX, moja kati ya sumu kali kabisa. Hadi sasa watu watatu wametiwa mbaroni kutokana na mauaji hayo.

No comments:

Post a Comment