Hakuna ambaye angejihisi alikuwa na bahati ya pekee kushuhudia tukio ambalo limebakia katika kumbukumbu za Dunia kama safari ndefu zaidi na yenye mafanikio makubwa mno. Lakini kwa raia wazalendo wa kireno, safari hii ilikuwa baada haijahitimishwa…
Mnamo 10 July, 2016 majira yaleyale ya kiangazi hatimaye wareno waliikamilisha safari yao chini ya kapteni Cristiano Ronaldo dos Santos Aveiro!
Toka michuano ya Euro2004 walivyopoteza mchezo wa fainali kwa goli 1-0 dhidi ya Ugiriki mbele ya mashabiki wao mjini Lisbon, wareno waliamini wana laana na kamwe hawataukimbia mkosi. Ni mkosi si kingine walichokitupia lawama kila wakifikiria mafanikio na heshima kubwa waliyowahi kujijengea kama taifa la kwanza kuupeleka utamaduni wake mabara yote ulimwenguni.
Kushuhudia wakoloni wenzao wa Ujerumani wakijizolea kombe la Dunia mara 4, Italy mara 4, Ufaransa wakinyanyua Euro2000 baada ya kuifunga Portugal 2-1 katika nusu fainali, Uingereza wakinyanyua kombe la Dunia 1966 tena katika nusu fainali wakishinda 2-1 mbele ya Portugal ya kapteni Eusébio. Portugal walihitaji taji la kimataifa kuikamilisha heshima yao.
Wengi hawakuipa nafasi Portugal hii ya kukanyaga hata nusu fainali za Euro2016, kutokana na uwezo mdogo wa mchezaji mmoja mmoja kulinganisha na vikosi vingine kama vya Germany, Spain na France. Hata wakati wa kufuzu ni wazi Portugal haikupita kwa rekodi ya kuvutia kabisa licha ya kuongoza ikiwa katika kundi lenye timu zenye uwezo mdogo kama Armenia na Albania lakini walihitimisha michezo minane wakiwa na magoli 11 tu.
Wakitambua madhaifu yao mengi katika kikosi chao na kebehi za miamba mingine ya Ulaya hasa majirani zao wa Spain, Portugal waliamua kuja na msimamo mmoja tu safari hii, matokeo kwanza takwimu waachie wachambuzi wa habari.
Mbinu za Kocha Mzalendo Fernando Santos
Akitoka kufundisha soka katika nchi ya Ugiriki ambako kwa miaka 11 alikuwa akivinoa vilabu vya ligi kuu nchini humo kabla ya kukabidhiwa timu ya taifa ya Ugiriki na kuivusha kushiriki michuano yao ya kwanza ya kombe la Dunia 2014 pale Brazil. Ni wazi kuwa soka la kigiriki lilishamjenga katika falsafa ya kuamini matokeo ya mchezo ni jambo la kwanza kabla ya kuangalia njia zilizofanikisha ushindi huo.
Mara baada ya kushinda 2-0 mchezo dhidi ya Wales katika nusu fainali alipondwa kwa mara ya nne kwa mchezo wao usiovutia, “kama baada ya mchezo wa fainali nitapondwa tena kwa kucheza vibaya na kupata ushindi, basi nitarejea Lisbon (Portugal) nikiwa mtu mwenye furaha zaidi duniani!,” kwa uso wa tabasamu alijibu waandishi.
Anatambua umuhimu wa kuzichanga vema karata katika michuano mikubwa, ni michezo saba pekee inayomuweka mtu mfalme kwa miaka minne.
Portugal haitakuwa na midfielders wenye uwezo wa juu wa kuibeba team kwa possession pindi wanapoyatafuta matokeo na mbele wakiwa na tatizo lao la kitaifa la kukosa foward kwa miaka mingi. Mbinu za Santos kuwachezesha Ronaldo na Nani kama pair ya strikers iliwalipa mno, timu inakaba chini kwa muda mwingi na pindi inapopata mpira inauhamisha haraka kwenye wings kwa ajili ya counter-attacks.
Ni mbinu hizi za kuucheza mpira wakati wanapouhitaji kuufanyia kazi uliowawezesha kushinda mchezo mmoja tu kati ya saba ndani ya dakika 90, lakini wakitoa wachezaji bora wa mchezo katika mechi zao zote.
Uongozi Shupavu Wa Cristiano Ronaldo
Wengi wa wapinzani wake walikuwa wakimuandama sana Ronaldo kabla hata hajakanyaga ardhi ya France. Wakati wachezaji wengi wakiwa katika kambi za maandalizi na vikosi vyao, Ronaldo alikuwa mapumzikoni katika fukwe za Ibiza akituliza akili baada ya msimu mwingine mrefu aliouhitimisha kwa taji la Uefa Champions League. Akitokea kucheza mechi zaidi ya 50 za msimu na Real Madrid, Ronaldo hakuwa na utimamu kamili wa kimwili wakati wakuanza michuano hii, watu walisahau Ronaldo alikosa mechi tatu za mwishoni mwa laliga na nusu fainali ya Uefa dhidi Manchester City sababu ya majeraha.
Mzigo wa matumaini ya Taifa mabegani mwake, mafanikio ya mpinzani wake wa damu Messi akiipeleka Argentina katika fainali za Copa America na maswali ya kebehi kutoka kwa wanahabari juu kusuasua kwa kikosi chake katika hatua ya makundi vilimmaliza uvumilivu, anakamata microphone aliyoelekezewa na kuitosa ndani ya bwawa….. sio muda wa stori. Kesho yake jioni anapasia nyavuni magoli mawili na kuweka rekodi ya kufunga katika michuano minne ya Euro….. ni muda wa kazi.
Hakutaka kujiangusha yeye mwenyewe, kila mechi iliyokuwa mbele yake tayari kulikuwa kuna vita binafsi ya Balon d’ Or ikitajwa dhidi ya Ronaldo. Nusu fainali dhidi ya Wales ya Gareth Bale ilitajwa kama vita ya wachezaji wawili ghali zaidi duniani kabla ya stori zote kukatizwa dakika ya 53 alipompa Luis Nani pasi ya goli muda mfupi baada ya yeye mwenyewe kupaa angani na kukita kichwa kizito nyavuni mwa Wales. Fainali dhidi ya wenyeji France ulikuwa wakati muafaka wa wapinzani wake kujiweka nyuma ya kivuli cha Antoine Griezmann aliyekuwa katika kiwango bora cha michuano ili kuipoteza heshima ya Ronaldo. Lakini hata kuumia kwake kabla ya half-time na kutolewa nje bado havikuwa sababu ya kusalimu amri.
Mara nyingi tunaaminishwa kuwa Ronaldo ni mchezaji bishoo tu na mwenye kujali umaarufu wake kuliko mafanikio ya timu nzima. Lakini katika mwezi huu mmoja amejionesha wazi yeye ni mpiganaji, mzalendo, na mhamasishaji mkuu wa kikosi kuliko mtu yeyote anavyoweza kufanya ndani ya Portugal.
Katika mchezo wa robo fainali kulikuwa na woga miongoni mwa wachezaji wa Portugal kupiga penalti, mmojawapo alikuwa Joao Moutinho (alikosa penalti katika nusu fainali ya 2012 vs Spain), kama kapteni wa timu alimjaza ujasiri “huu ni mchezo tu, piga kwa ujuzi wako kama kawaida. Ukifunga tunasonga mbele, ukikosa poa tu…. Mungu naye ana mahesabu yake!”. Hapo unapokea ushauri kutoka kwa mtu aliyepiga zaidi ya penati 100 katika maisha yake katika michuano ya ngazi ya juu kabisa, Moutinho anaweka mpira vizuri anamwangalia golikipa Lukasz Fabianski anavyorukaruka na kupasia penati nyavuni.
Éderzito António (Éder) mfungaji wa goli pekee la ushindi katika mchezo wa fainali alitoa ushuhuda mbele ya jopo la waandishi “Ronaldo aliniambia nitaingia kufunga goli jioni hii, nilifikiri mzaha!”. Hadi jioni ya fainali, Eder alikuwa ameichezea Portugal mechi 28 na kufunga goli moja tu (katika mchezo wa kirafiki miezi 12 iliyopita), yataka moyo mgumu zaidi ya Farao kumwaminisha ‘mjaluo’ huyu atafunga goli katika usiku wa fainali ya Europe.
Lakini alipoulizwa aliwezaje kumbashiri mfungaji kwa usahihi, “Nipo kwenye huu mchezo kwa muda mrefu kidogo, nimecheza takribani fainali 10 kubwa hivyo ni rahisi kupata hisia (machale) ya mwenendo wa mchezo utakavyokuwa.”
Anawapa kisogo waandishi anaenda kumkumbatia Luis Nani na kumpongeza kwa kulifikisha salama jahazi la Portugal, kisha Ronaldo anachukua zawadi yake ya mfungaji namba mbili na kumkabidhi Luis Nani kiatu cha silver “chukua hiki, mchango wako umekuwa mkubwa sana comrade!”
Mwishowe jemedari Cristiano Ronaldo akichechemea na bandeji gotini anawaongoza wenzake kupanda jukwaani kunyanyua kombe lao la kwanza la kimataifa. Hatimaye wameukamilisha muamala wa mafanikio ya Portugual miaka 597 baada ya kapteni Vasco da Gama kuianza safari!
No comments:
Post a Comment