Saturday 16 July 2016

figisu za ligi ya Tanzania


  Na Golden Mwakatobe
 
Shirikisho la soka hapa nchini, TFF, linakaribia kutoa ratiba ya msimu wa 20 wa ligi kuu Tanzania Bara.
Huu utakuwa msimu wa 20 tangu kuanza kwake mwa 1997 baada ya kubadilika mfumo na muundo kutoka ligi daraja la kwanza kama ligi ya juu zaidi.
Lakini pia huu utakuwa msimu wa 53 tangu kuanza kwa ligi ya Tanzania mwaka 1995 ikiitwa ligi ya taifa.
Siku za mwisho za msimu uliopita  zilishuhudia matukio yanayoweza kuitwa ‘figisufigisu’, kwa mfano kupokwa pointi tatu kwa Azam FC dhidi ya Mbeya City kutokana na kujichanganya kwenye kadi za Erasto Nyoni na mkasa wa mechi ya Ndanda na Yanga iliyohama kimazabe kutoka  Mtwara mpaka Dar Es Salaam.



Lakini matukio ya figisufigisu kwenye ligi ya Tanzania yalianza tangu ligi hiyo ilipoanza mwaka 1965. Kupitia ukurasa huu, tutakuletea mikasa ya kila msimu tangu kuanza kwa ligi hiyo mpaka msimu uliopita.

Leo tunaanza na mkasa wa 1965.

Mwaka 1965 ndiyo ligi ya Tanzania ilianza, wakati huo ikiitwa ligi ya taifa.

Ligi ilianza na timu sita pekee

Tanganyika Planting Company (TPC) ya Moshi Kilimanjaro

Tobacco (Sigara) ya Pwani.

Young Africans (Yanga) ya Pwani.

Sunderland (Simba) ya Pwani

Coastal Union ya Tanga

Manchester United ya Tanga

NB: Wakati huo Dar Es Salaam ilikuwa sehemu ya mkoa wa Pwani.

Yanga ilianza ligi hiyo kwa kishindo na kuongoza.

Kama ilivyokuwa kawaida tangu 1935 wakati wa ligi ya Dar es Salaam ambayo ndiyo ligi ya kwanza kabisa Tanzania kabla ya ligi ya taifa, msimu ulikuwa haukamiliki kabla Yanga na Sunderland hazijakutana.

Kwenye ligi ya taifa 1965, watani hawa walipangwa kukutana 7/6/1965. Huu ndiyo mchezo wa kwanza kabisa baina ya timu hizi kwenye ligi ya taifa.

Mchezo huo ulitawaliwa na mizengwe hata kabla haujaanza. Yanga walipinga mchezaji mmoja wa Sunderland kucheza, Sunderland nao wakawakataa wachezaji wawili wa Yanga.

Ukazuka mvutano mkubwa lakini baadaye mwenyekiti wa ligi, Abdu Hussein akaingilia kati na kusuluhisha na wachezaji wote wakakubaliwa kucheza.

Wakati mpira unataka kuanza, Yanga wakagoma tena wakimkataa mwamuzi.

Rais wa FAT (wakati huo kiongozi mkuu wa FAT aliitwa Rais kabla ya kubadilishwa kuwa Mwenyekiti na siku hizi kuwa tena Rais) Balozi J. Maggid akamteua kocha wa timu ya taifa (mzungu wa kwanza kufundisha timu ya taifa, Myugoslavia Milan Celebic achezeshe mechi hiyo akisaidiwa na washika vibendera wa kuunga unga).

Mpira ulichelewa sana kuanza lakini hatimaye ulifanyika na dakika 15, Yanga wakapata bao kupitia Mawazo Shomvi. Dakika 10 kabla mchezo haujamalizika, giza likatanda na ‘refa’ akapiga filimbi ya kumaliza mchezo.

Sunderland wakakata rufaa wakitaka mchezo urudiwe, FAT wakakubali wakisema Yanga ndiyo walisanabisha mchezo kuchelewa kuanza. Yanga nao wakagoma wakidai Sunderland ndiyo chanzo cha kuchelewa. Pande zote zikashindwa kupata suluhusho na Yanga wakajitoa kwenye ligi. FAT wakaipa ushindi  Sunderland na hapo ndipo Sunderland wakatawazwa kuwa mabingwa wa kwanza wa ligi ya Tanzania.

No comments:

Post a Comment