Sunday 31 July 2016

Jinsi ya kulima Vanila

 

Vanilla (Vanilla fragrans) asili yake ni Amerika ya kati huko Mexico, Guatemala na Costa Rica ambako ilianza kutumika tangu karne ya 15.
 Zao la vanilla lilifika barani Ulaya karne ya 16, kisha likapelekwa visiwa vya Reunion, hatimaye kusambazwa Mauritius, Madagasca, Shelisheli, Tahiti na Comoro kati ya karne ya 18 na 19. Zao hili kwa sasa linazalishwa kwa wingi sehemu za Madagasca, Comoro na Reunion. Hapa Tanzania zao hili liliingizwa mkoani Kagera mwaka 1962 kutokea nchini Uganda.
Hata sasa Mkoa wa Kagera ndio unaozalisha zao hili katika wilaya za Bukoba na Muleba, na pia huko Zanzibar. Zao hili linaleta fedha za kigeni kwa nchi na kuleta ajira kwa wananchi. Vanilla ni zao ambalo hutumika kuongeza ladha katika vyakula na vinywaji vya aina mbalimbali. Matumizi makubwa ya zao hili ni kuongeza harufu nzuri na ladha ya vyakula na vinywaji mbalimbali.


 Baadhi ya vyakula ambavyo vanilla huwekwa ni pamoja na chocolate, keki, maandazi, biskuti, uji, barafu (ice cream), n.k.

Vinywaji baridi kama vile soda na juisi. Mbali na vyakula na vinywaji vanilla pia hutumika kutengenezea bidhaa nyingine mbali mbali kama vile manukato, mafuta ya kulainisha ngozi, sabuni, vipodozi n.k

2.0 TABIA YA MMEA
Vanilla ni mmea ambao hutambaa kwenye mti wa mhimili na huzaa matunda yanayofanana na maharage. Mmea wake hukua kufikia urefu wa mita 10 hadi 15. Maua yake ni makubwa, manene na yananukia, yana rangi ya kijani isiyokolea na njano. Ukubwa wa harage ni kiasi cha sentimita 10-25cm na unene wa sentimita 1.5.


3.0 MAENEO YANAYOFAA KWA UZALISHAJI
Zao hili kama yalivyo mazao mengine mengi hustawi vizuri kwenye udongo wenye kupitisha maji, na wenye rutuba na mboji ya kutosha. Kivuli kiasi huhitajika, kwani mimea hii haipendi jua kali.

4.0 HALI YA HEWA INAYOFAA
 Zao la vanilla huhitaji hali ya hewa yenye wastani wa nyuzi joto za sentigrade 28 inaweza pia kuhimili katika nyuzi joto za sentigrade 21 hadi 30). Huhitaji mvua zenye mtawanyiko mzuri wa milimita kati ya 1,500 na 3,000, lakini pia inaweza kustawi vizuri katika mvua za wastani wa milimita 2,000. Vanilla ya porini inamea zaidi maeneo yenye unyevunyevu yaliyo usawa wa bahari hadi mita 600. Kinahitajika kipindi cha kati ya miezi 2 hadi 4 cha ukavu ili kuwezesha mmea kuchanua maua.

5.0 UZALISHAJI
5.1 UTAYARISHAJI WA SHAMBA
Tayarisha shamba lako wakati wa kiangazi, yaani kabla ya mvua za masika hazijaanza.
1. Chimba mashimo yenye urefu wa sentimita 60 (futi 2), upana wa sentimeta 60 (futi 2) na kina cha sentimita 30 (futi 1).
2. Nafasi kati ya mstari hadi mstari ni mita 2.7 hadi 3 na kati ya shimo hadi shimo katika mstari ni mita 1.8 hadi 2.5.
3. Baada ya kuchimba mashimo, yaachwe wazi kwa muda wa kati ya mwezi mmoja hadi miwili hivi.
4. Weka mbolea ya samadi mwezi mmoja kabla ya kupanda, kiasi cha debe moja hadi mbili kwa kila
shimo, changanya vizuri na udongo kisha fukia shimo.

5.2 UPANDAJI
1. Kata mihimili yenye urefu wa sentimita 120 mpaka 150 kila mmoja. Miti inayofaa zaidi kwa mihimili ni aina ya Jatropha (Jatropha curcas) na Casuarina (Casuarina equisetifolia). Baada ya kuikata iache inyauke kwa siku kati ya 1 mpaka 10 hivi kisha ipandwe pembeni mwa kila shimo kiasi cha kina cha sentimita 15 hadi 30.
2. Tayarisha marando yenye urefu wa sentimita 90 (futi 3) mpaka sentimita 120 (futi 4), yaache yanyauke kidogo (kwa silu 7 hadi
10). Toa majani 3 au 5 kutoka sehemu ya chini ya rando. Marando marefu huchanua baada ya mwaka 1.5 au 2, marando mafupi (sentimit30) huchelewa kuchanua (miaka 3 hadi 4).
3. Panda marando hayo kwenye mashimo yaliyotayarishwa kwa kina cha sentimita 10 mpaka 15 funika na udongo na gandamiza.
4. Upandaji ufanyike mwanzoni mwa msimu wa mvua za masika.
5. Tandaza nyasi kavu shambani ili kuzuia magugu na kuhifadhi unyevunyevu shambani.
6. Funga sehemu iliyobakia katik mhimili

6.0 KUHUDUMIA SHAMBA
Shamba liwe safi wakati wote. Tandaza nyasi kavu shambani ili kuzuia magugu na kuhifadhi unyevunyevu. Punguzia mihimili kwa kuikata kila inaporefuka zaidi ya sentimita 180, ili itoe machipukizi yatakayoongeza kivuli shambani. Chavusha maua kila yanapochanua kwa wakati, muda wa kuchavusha ni kuanzia saa 3.00 asubuhi hadi saa 7.00 mchana.

Kifaa chenye ncha kali (mwiba, sindano, pini, n.k.) hutumika kuchavusha ua. Ua lililochavushwa hubaki kwenye kikonyo kwa siku tatu wakati lile ambalo halikuchavushwa huanguka katika kipindi cha siku moja hadi 2.

7.0 MAGONJWA NA WADUDU
Wadudu Wadudu mbali mbali hushambulia zao hili, lakini hawasababishi madhara. Konokono kwa mfano, hula kiasi kidogo sana cha majani. Kuku pia hushambulia mizizi.

Magonjwa
Zao hili hushambuliwa kwa kiasi kidogo sana na magonjwa yafuatayo: -
• Kuoza kwa mizizi
• Kunyauka kwa ncha ya tawi
Mnyauko unaosababishwa na ukungu.
Magonjwa na wadudu hawa huweza kudhibitiwa kwa kupanda mbegu bora na kuweka shamba katika hali ya usafi wakati wote.


8.0 UVUNAJI
Uvunaji hufanyika kati ya miezi 6-9 tangu ua lilipochanua. Maharage ya vanilla huvunwa yanapokuwa yamekomaa sehemu ya ncha ya tunda inaanza kuwa ya rangi ya njano. Tunda likikomaa sana hupasuka. Uvunaji hufanyika kwa kukata maharag yaliyokomaa kwa kutumia kisu kikali au mikono. Vanilla huvunwa kabla haijaiva na kisha huvundikwa ili kutengeneza kemikali inayoitwa vanillin, ambayo ndiyo hutoa harufu nzuri na ladha inapotumiwa kwenye vyakula, vinywaji na bidhaa mbalimbali.
Mavuno ya vanilla mbichi kwa hekta moja ni zaidi ya Tani 2.5.

9.0 USINDIKAJI
 Baada ya kuvunwa, maharage ya vanilla hutumbukizwa ndani ya maji moto (nyuzi joto la sentigredi 63), kwa dakka moja hadi tatu kisha opoa kwa haraka. Maharage yakiwa bado moto hufungwa ndani ya kitambaa cha pamba chenye rangi nzito (kama blanketi), siku ya pili yataanikwa juani kwa saa moja. Kisha kwa kipindi cha wiki moja maharage hayo yataaanikwa kwa saa mbili kila siku, na hubaki yamefungwa wakati yameanuliwa.

Kazi hii huendele kwa kipindi cha miezi miwili au mitatu kisha vanilla huanikwa kwenye kivuli au kwenye chumba chenye hewa ya kutosha. Kwa tendo hili kiasi cha asilimia 70 hadi 80 cha maji huondolewa na rangi ya maharage ya vanilla hubadilika na kuwa ya kahawia. Kazi ya kukausha na kuvundika inaweza kuchukua miezi 5 mpaka 6 kukamilika ili
kuipata harufu nzuri inayohitajika.

Njia nyingine ya uvundikaji huchukua siku 4 baada ya kukatakata maharage na kuya vundika katika joto kali. Njia hii huharakisha usindikaji, ingawa inaathiri ubora wa zao.
Kilo 5.5 hadi 6.0 za vanilla mbichi hutoa kilo 1.0 ya vanilla iliyokaushwa.

10.0 SOKO LA VANILLA
Vanilla mbichi huuzwa hapa nchini (Wilaya ya Bukoba) kuanzia bei ya shilingi 20,000/= kwa kilo. Wakati vanilla iliyokaushwa, huuzwa nchini Uganda kwa kiasi cha shilingi 300,000/= kwa kilo.

11.0 GHARAMA ZA UZALISHAJI NA MAPATO GHARAMA YA HEKTA MOJA:
Mbegu Tshs. 480,000/-
Vibarua 3,600,000/-
Mbolea(mboji/samadi) 240,000/-

Jumla 4,320,000/-

MAPATO YA VANILLA MBICHI:
Kilo 2,500X20,000/- 50,000,000/-

No comments:

Post a Comment