Tuesday 26 July 2016

Yanga kununa tena kwa Medeama leo?

Klabu ya Yanga inashuka dimbani hii leo dhidi ya Medeama Uwanja wa Essipong Sports katika mchezo wa marudiano wa kombe la shirikisho Afrika.
Yanga itahitaji ushindi katika mchezo huo utakaopigwa majira ya jioni na baada ya hapo iiombee Mazembe iifunge Bejaia ili kuweka hai matumaini ya Nusu Fainali.
Mchezo wa Yanga dhidi ya Medeama utachezeshwa na marefa wa Morocco, ambao ni Redouane Jiyed, atakayepuliza filimbi akisaidiwa na washika vibendera Mohamed Lahmidi na Hicham Ait Abbou.

Mazembe itaikaribisha MO Bejaia hapo kesho Uwanja wa Mazembe mjini Lubumbashi ikihitaji ushindi ili kujihakikishia nafasi ya Nusu Fainali.

Katika mchezo wa awali uliopigwa Julai 16 mwaka huu Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, Yanga ililazimishwa sare ya bao 1-1 na kubaki mkiani mwa Kundi A baada ya kufungwa katika michezo mingine miwili ya awali huku Medeama ikiwa nafasi ya tatu kwa kufungwa mechi moja na kutoa sare mbili.

MO Bejaia ya Algeria inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi tano huku vinara TP Mazembe ya DR Congo wakiwa wamejikusanyia pointi saba mpaka sasa.

No comments:

Post a Comment