Gingrich alikuwa miongoni mwa waliopigiwa upatu kuwa mgombea mwenza wa Trump
Mwanasiasa huyo wa chama cha Republican amesema wote wanaoamini katika Sharia wanafaa kutimuliwa kutoka Marekani.
Sharia ni sheria ya dini ya Kiislamu inayofuata Koran, maisha ya Muhammad na mafundisho ya wasomi wa Kiislamu.
Bw Gingrich amesema hayo kufuatia shambulio lililotekelezwa mjini Nice, kusini mwa Ufaransa ambapo watu 84 walifariki na wengine zaidi ya 50 kujeruhiwa vibaya.
Matamshi yake yanaonekana kukaribiana sana na ya mgombea urais wa chama cha Republican Donald Trump, ambaye mwaka uliopita alipendekeza Waislamu wazuiwe kuingia Marekani.
"Ustaarabu wa nchi za Magharibi umo vitani. Tunafaa kusema kweli, tumtahini kila aliye hapa ambaye ana asili ya Kiislamu na iwapo anaamini katika Sharia basi aondolewe nchini,” Bw Gingrich aliambia shirika la habari la Fox News.
Trump amtangaza Pence kuwa mgombea mwenza
"Sharia haiwezi kuendana na ustaarabu wa magharibi. Waislamu wa kisasa ambao wameachana na Sharia, tuna furaha kuwa nao kama raia wenzetu. Ninaweza kufurahia hata wakiwa majirani zangu,” akaongeza.
Rais Barack Obama ameshutumu vikali maneno ya Bw Gingrich na kusema yanaenda kinyume na maadili ya Wamarekani.
“Baada ya mashambulio ya jana usiku, tumesikia mapendekezo kwamba Waislamu wote nchini Marekani waandamwe, kupimwa kuhusu imani yao, na baadhi watimuliwe au kufungwa jea,” alisema Bw Obama.
“Kimsingi, wazo hilo lenyewe linakosea heshima maadili ambayo sisi huwatetea kama Wamarekani.
Hatuwezi kukubali kutekwa na woga au tuanze kukosana wenyewe kwa wenyewe au kubadili mtindo wetu wa maisha.”
No comments:
Post a Comment