Akizungumza leo na waandishi wa habari, Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako asema kuwa kwa kipindi chote serikali
ilikuwa ikifanya uchambuzi ili kuona ni wanafunzi gani walikuwa na sifa
za kusoma kozi hiyo maalum ambayo ilianzishwa kutokana na tatizo la
walimu wa Sayansi.
Baada ya uchambuzi wa kina serikali imebaini kuwa takriban wanafunzi 290
waliokuwa wakisoma stashahada ya ualimu wa sekodari na wengine 1,181 wa
stashahada ya ualimu wa shule ya msingi, wakiwa hawana sifa kabisa ya
kuendelea na programu hiyo na wameshauriwa kuomba programu nyingine
katika vyuo vingine zinazoendana na sifa zao.
Ifuatayo ni sehemu ya taarifa iliyotolewa na Wazir Ndalichako..
Maamuzi ya Serikali
Kundi la Stashahada Maalumu ya Ualimu wa Elimu ya Sekondari
(i) Kwa kuwa uchambuzi umebainisha kuwa Wanafunzi wenye ufaulu wa Daraja
la I na la II ambao pia wamefaulu masomo mawili ya Sayansi kwa kiwango
cha C-A ni 382 (mwaka wa I -134 na mwaka wa II - 248), wanafunzi hao
ndiyo pekee watakaorudishwa katika Chuo Kikuu cha Dodoma ili wakamalizie
mafunzo yao katika Chuo hicho.
(ii) Wanafunzi 4,586 wa mwaka wa I wa Programu Maalum ya Stashahada ya
Ualimu wa Elimu ya Sekondari waliokidhi vigezo vya ufaulu watahamishiwa
katika Vyuo vya Ualimu vya Morogoro, Butimba, Mpwapwa, Songea na Tukuyu
kuendelea na masomo yao.
(iii) Wanafunzi 1,337 wa Mwaka II watahamishiwa kwenye Vyuo vya Ualimu vya Korogwe na Kasulu kumalizia masomo yao.
(iv) Wanafunzi 290 waliokuwa wamedahiliwa kusoma Programu Maalum ya
Stashahada ya Ualimu wa Elimu ya Sekondari Masomo ya Sayansi na Hisabati
ambao hawana sifa stahiki wanashauriwa kuomba mafunzo yanayolingana na
sifa walizo nazo kwenye chuo chochote wanachotaka wao.
Kundi la Programu ya Ualimu wa Elimu ya Msingi
Wanafunzi katika kundi hili hawakuwa sehemu ya program maalum ya
kupunguza uhaba wa walimu wa Sekondari wa Sayansi na Hisabati. Walikuwa
wanaandaliwa kufundisha shule za msingi wakati lengo la Programu Maalum
ilikuwa ni kukabiliana na tatizo za uhaba wa walimu wa Sekondari.
Maudhui ya program waliyokuwa wanasoma hayakuwa sawasawa na yale ya Programu ya Ualimu wa Sekondari wa Sayansi na Hisabati.
(v) Wanafunzi 29 wa mwaka wa II wenye Cheti cha Daraja IIIA
waliodahiliwa kusoma Stashahada ya Ualimu wa Shule za Msingi
watahamishiwa katika Chuo cha Ualimu Kasulu wamalizie masomo yao kwa
gharama zao wenyewe.
(vi) Wanafunzi 1,181 waliodahiliwa kusoma Stashahada ya Kawaida ya
Ualimu wa Elimu ya Msingi waombe mafunzo yanayolingana na sifa
walizonazo mahali popote watakapotaka wao.
Gharama za Masomo
Serikali itaendelea kuwapatia mikopo wanafunzi watakaorejeshwa UDOM.
Aidha, wanafunzi watakaohamishiwa kwenye Vyuo vya Ualimu vya Serikali
watapewa mkopo wa kiasi cha Sh. 600,000/= kwa mwaka ambayo ni ada ya
Mafunzo ya Ualimu itakayolipwa moja kwa moja Chuoni.
Hitimisho
(i) Wanafunzi wote wanaorejeshwa Chuo Kikuu cha Dodoma wataanza masomo mwezi Oktoba 2016.
(ii) Wanafunzi watakaohamia katika Vyuo vya Ualimu wataendelea na mafunzo yao mwezi Septemba mwaka 2016.
(iii) Wanafunzi wote watatakiwa kuripoti wakiwa na vyeti vyao halisi vya
Kidato cha Nne ambavyo vitahakikiwa kabla hawajapokelewa rasmi kwenye
vyuo walivyopangiwa.
No comments:
Post a Comment