Mhandisi Uchenjuaji Madini
kutoka Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST), Priscus Kaspana (katikati)
akionesha kipande cha mwamba na kutoa maelezo kwa wananchi waliotembelea
banda hilo, kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Sabasaba yanayoendelea
katika viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.
Na Golden Mwakatobe
Imeelezwa kuwa Megawati 200 za
umeme unaotokana na jotoardhi nchini zinatarajiwa kuzalishwa ifikapo
mwaka 2025 na kumaliza changamoto ya ukosefu wa umeme nchini.
Hayo yameelezwa na Meneja Katika
Masuala ya Sheria na Ukatibu kutoka Kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi
Nchini (TGDC), Mershil Kivuyo katika maonesho ya kimataifa ya
Sabasaba yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar
es Salaam.
Akielezea mikakati ya kampuni
hiyo, Kivuyo alisema kuwa mpaka sasa maeneo zaidi ya 50 yenye
viashiria vya jotoardhi nchini yamegunduliwa ambayo kwa sasa
yanafanyiwa kazi.
Alisema kuwa kampuni imeweka
kipaumbele katika maeneo ya Ngozi na Songwe mkoani Mbeya, Luhoi mkoani
Pwani, Kisaki mkoani Morogoro na Mount Meru mkoani Arusha.
Aliongeza kuwa utafiti wa kina umefanyika Ziwa Ngozi ambapo inatarajiwa kuchimbwa visima virefu mwaka 2017.
Akielezea manufaa ya Jotoardhi
Kivuyo alieleza kuwa nishati ya jotoardhi itatumika kuzalisha umeme wa
uhakika na hivyo kumaliza changamoto ya ukosefu wa umeme na hivyo
kuongeza uwekezaji kwenye viwanda.
Aliongeza matumizi mengine kuwa ni pamoja na kukaushia mazao, kilimo cha maua na katika utengenezaji wa mabwawa.
Alisisitiza kuwa wawekezaji wanakaribishwa kwenye uwekezaji wa jotoardhi na kuchangia kasi ya ukuaji wa uchumi wa nchi.
No comments:
Post a Comment