Wana wawili wa mgombea urais wa
chama cha Republican nchini Marekani Donald Trump ni miongoni mwa watu
waliohutubu katika kongamano la kitaifa la chama hicho mjini Cleveland,
Ohio.
Kinyume na mkewe Trump, Melania, ambaye alishutumiwa sana
alipotoa hotuba siku ya kwanza baada ya kubainika kwamba baadhi ya
maneno kwenye hotuba yake yalitoka kwenye hotuba iliyotolewa na mke wa
Rais Barack Obama, Michelle, mwaka 2008, wawili hao walisifiwa sana.Mwanawe wa kiume, ndiye aliyetangaza kwamba babake alikuwa amepata wajumbe wa kutosha na kuidhinishwa kuwa mgombea rasmi wa chama hicho.
- Donald Trump aidhinishwa kugombea urais Marekani
“Kwa babangu, lisilowezekana huwa ni mwanzo tu … hivyo ndivyo anavyotazama maisha,” Donald Trump Jr amesema.
Mwanawe huyo ana wadhifa mkuu katika shirika la Trump Organization na amekuwa mshauri wa karibu wa babake wakati wote wa kampeni.
Bintiye Donald Trump, Tiffany, pia alimsifu sana babake.
Tiffany alifuzu hivi majuzi kutoka kwenye Chuo Kikuu cha Pennsylvania na ana wafuasi wengi sana kwenye Instagram.
“Amenisaidia sana kuwa mtu bora,” amesema.
Wengi walimsifu sana kwa kuonekana kutulia, licha ya kwamba alikuwa anahutubia kikao kikuu cha chama.
Tiffany, 22, ana wafuasi zaidi ya 165,000 kwenye Instagram na ndiye mwana wa pekee wa Donald Trump na mkewe wa pili Marla Maples. Alilelewa Los Angeles, mbali na familia ya Trump.
Alifanya kazi ya uanamitindo kwa muda na mwaka 2011, alichomoa wimbo kwa jina Like A Bird.
Donald Trump ana watoto watano, Donald Trump Jr, Ivanka Trump na Eric Trump kutoka kwa mke wa kwanza Ivana Marie Trump, Tiffany Trump kutoka kwa mke wa pili Marla Maples na Barron Trump kutoka kwa mke wa tatu na wa sasa Melania Knauss.
No comments:
Post a Comment