
Na Mwamvita Mtanda
Pwani. Mkoa wa Pwani una migogoro ya ardhi ipatayo 47 inayohusisha uvamizi wa mashamba yanayomilikiwa kisheria, maeneo ya Serikali pamoja na ya wakulima na wafugaji.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo alisema hayo wakati akitoa maagizo 11 kwa wakuu wa wilaya wa mkoa huo aliowaapisha mjini Kibaha juzi.
Mhandisi Ndikilo alisema changamoto hiyo ya ardhi na nyingine zinatakiwa kusimamiwa ipasavyo ili kufikia lengo la Hapa Kazi Tu.
Alisema hakuna sababu ya viongozi hao kukaa ofisini, badala yake wawafuate wananchi vijijini wakazungumze nao na kusikiliza kero zinazowakabili.
Mhandisi Ndikilo alisema haipendezi watu wakatafute suluhu mkoani ilhali Serikali za vijiji, kata, tarafa na halmashauri zipo katika maeneo yao.
Pia, aliwataka wakuu hao kulinda amani na utulivu ili wananchi wapate fursa ya kujishughulisha na kazi za maendeleo na kujiongezea kipato.
“Kapambaneni na uhalifu wa aina zote ikiwamo dawa za kulevya, ujambazi wa kutumia silaha na mauaji ya albino. Changamoto za uhalifu zilizotokea Dar es Salaam, Tanga na Lindi zinaweza kutokea na hapa, kwa hiyo mkajipange kuzidhibiti katika wilaya zenu,” alisema Mhandisi Ndikilo.
Wakuu wa wilaya walioapishwa ni Majid Mwanga wa Bagamoyo, Gulamhussein Kifu (Kibiti), Assumpter Mshama (Kibaha), Juma Abdallah (Rufiji), Gilberto Sanga (Mkuranga) na Shaib Nnunduma (Mafia).
Akizungumza baada ya kuapishwa Mwanga alisema ana kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa kuteuliwa kuiongoza Bagamoyo na kwamba ataitumia fursa hiyo kwa uadilifu kutatua changamoto zilizopo.
Abdallah aliwataka wakazi wa Rufiji wampokee kwa kumpa ushirikiano.
Alisema ataanza kwa kupita kila mahali vijijini kusikiliza kero zao ili ajue pa kuanza.
No comments:
Post a Comment