Kaimu
Mkurugenzi British Council Tanzania, Bi. Nesia Mahenge (kulia)
akiwaelekeza baadhi ya Viongozi wa Mashirikisho ya Sanaa Tanzania pamoja
na Wadau wa masuala ya Sanaa kuhusu Fursa ya Sanaa inayodhaminiwa na
Taasisi hiyo, 19 Julai, 2016 jjijini Dar es Salaam.
PICHA ZOTE NA BENEDICT LIWENGA-WHUSM.
Kaimu Mkurugenzi, Idara ya Maendeleo ya Sanaa, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bi. Leha Kihimbi (kulia) akiwasisitizia
baadhi ya Viongozi wa Mashirikisho ya Sanaa Tanzania pamoja na Wadau wa
masuala ya Sanaa kuhusu umuhimu wa Fursa ya Sanaa inayodhaminiwa na
Taasisi hiyo, 19 Julai, 2016 jjijini Dar es Salaam.
Kaimu
Mkurugenzi British Council Tanzania, Bi. Nesia Mahenge (wa pili kushoto
waliokaa mbele) akiwaelekeza baadhi ya Viongozi wa Mashirikisho ya
Sanaa Tanzania pamoja na Wadau wa masuala ya Sanaa kuhusu Fursa ya Sanaa
inayodhaminiwa na Taasisi hiyo, 19 Julai, 2016 jjijini Dar es Salaam.
SERIKALI kwa
kushirikiana na British Council Tanzania imekutana na baadhi ya
Viongozi pamoja na Wawakilishi wa Mashirikisho mbalimbali ya Sanaa
nchini na kuwapatia elimu juu ya namna ya kuandika Mapendekezo
(Proposals) za Mradi wa kuwania fursa ya sanaa inayodhaminiwa na British
Council Tanzania.
Elimu hiyo
imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi wa British
Council Tanzania, Bi. Nesia Mahenge pamoja na Kaimu Mkurugenzi Idara ya
Sanaa, Bi. Leah Kihimbi lengo likiwa kuwahamasisha wasanii kote nchini
kuchangamkia fursa hiyo inayodhaminiwa na Taasisi hiyo yenye Makao yake
Makuu nchini Uingereza.
Awali
akieleza kuhusu fursa hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa British Council
Tanzania, Bi. Nesia Mahenge amesema kwamba fursa ya sanaa kwa Wasanii
zinahusisha sehemu tatu ikiwemo fursa ijulikanao kama nAnA (new Arts new Audiences) ambayo ndiyo imefunguliwa kwa sasa na baadaye fursa nyingine mbili za Creative Hustle pamoja na Mobility East Africa zitafuata.
Ameeleza
kuwa kuhusu vigezo vya kujiunga na fursa hiyo ni pamoja Wasanii kuwa na
umri kuanzia miaka 18-35, kuwa na Ushirikiano (Partnership) katika ya
nchi tano zinazohusisha fursa hiyo, kuwa na Kampuni binafsi au ya
Shirikisho, fursa inahusisha fedha ya uandikaji wa Pendekezo (Proposal)
zitakazotolewa ni kuanzia paundi 2,000 hadi paundi 20,000 pamoja na kuwa
na akaunti namba katika benki fulani.
Amefafanua
kuwa, fedha zitakazotolewa na British Council Tanzania sio za mkopo bali
ni kwa ajili ya wasanii wote ambao watafanikiwa kuwania fursa hiyo
ambapo kwa sasa amesema kwamba wanaanza na fursa ya nAnA, hivyo
amewahimiza wasanii nchini kupitia mmoja mmoja pamoja na Mashirikisho
yao kuanza kuandika mapendekezo ya kuomba fursa hiyo kwa kujaza fomu
ambayo inapatikana katika tovuti ya www.britishcouncil.or.tz
“Fedha hizi
sio za mkopo, mtu akifanikiwa kuzipata haimaanishi kuwa anapaswa
kuzirejesha, isipokuwa British Council wao watakuwa wanafuatilia ni kwa
namna gani fedha hizo umeweza kufanikisha wazo lako na lina faida gani
katika jamii ama wengine wamenufaika vipi na wazo lako”, alisema Bi.
Mehenge.
Ameongeza
kuwa, Wasanii pamoja na Mashirikisho hayanabudi kusaidiana katika
kufanikisha suala hilo kwa kuelekezana juu ya namna ya kuwapata watu
wenye ujuzi wa jinsi ya kuandika Mapendekezo (Proposals) na kuziandika
kwa wingi ili Wasanii wa Tanzania wapate nafasi ya kushinda fursa hiyo
kwani kuna nchi nyingine nazo zinahusika na fursa hiyo ambazo ni za
Afrika Mashariki.
Kuhusu
mwisho wa kuwasilisha maombi hayo, amesema kwamba, tarehe ya mwisho ni
31 Julai mwaka huu,lakini wasanii hawanabudi kuwa na hofu kwani bado
wana nafasi kubwa ya kuandika na kuweza kushinda hiyo fursa, kwani
kinachomata ni wazo zuri msanii alilokuwa nalo na sio tu uandishi mzuri.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Sanaa, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo,
Bi. Leah Kihimbi amewasisitizia Wasanii kote nchini kuchangamkia fursa
hiyo bila kuwa na woga kwani ni fursa ya pekee ya kuwanufaisha na kazi
zao na kuiletea sifa Taifa.
“Msiogope
kuandika kuomba hii fursa, kwani kuna wenzenu pia wanaitafuta,
jitahidini kushirikiana ili mwisho wa siku Tanzania iwe na miongoni mwa
wasanii watakaowania fursa hii, na kwa kufanya hivyo mtakuwa mmelejengea
heshima Taifa letu”, alisema Kihimbi.
Fursa ya
Sanaa kwa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla ni fursa
inayodhaminiwa na British Council Tanzania ambapo wasanii wanatakiwa
kuiomba kwa kuandika mapendekezo kuhusu mawazo yao juu ya mambo
wanayotarajia kuyafanya kupitia sanaa na namna gani itanufaisha jamii
huku ikihusisha nchi tano za Afrika Mashariki zikiwemo Tanzania, Kenya,
Uganda, Rwanda na Ethiopia.
No comments:
Post a Comment