Friday, 12 February 2016

Waziri wa Maji na Umwagiliaji Atembelea Wilaya Za Wanging ombe na Makambako

ms1      Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe, Assumpter Mshama akizungumza mbele ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Inj. Gerson Lwenge na Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Wanging’ombe (WINGISA), Philemon Luhanjo.
ms2
  Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Inj. Gerson Lwenge akiwa na Mwenyekiti wa Bodi wa Mwenyekiti wa Bodi ya WINGISA, Philemon Luhanjo, Meneja WINGISA, Inj. Najib Asumbwile (mwisho kulia) na Mkurugenzi Msaidizi wa Maji Vijijini, Inj. Jackson Mutazamba (mwisho kushoto) pamoja na wafanyakazi wa WINGISA.
ms3
  Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Inj. Gerson Lwenge akitembelea chanzo cha maji cha Fukulwa, Wilaya ya Makambako.
ms4
   Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Inj. Gerson Lwenge akiwa na Mbunge wa Jimbo la Makambako, Deo Sanga na Mkuu wa Wilaya ya Makambako, Sarah Dumba wakiwa kwenye eneo la ujenzi la Bwawa la Tagamenda, Wilaya ya Makambako.
ms5
 Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Inj. Gerson Lwenge akizungumza na wananchi wa Manga, Wilaya ya Makambako.
Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Inj. Gerson Lwenge leo ametembelea Wilaya za Wanging’ombe na Makambako mkoani Njombe na kujionea hali ya utekelezaji wa miradi ya maji kulingana na ahadi ya Mhe. Rais, John Magufuli katika kampeni zake za urais.
Aidha, ziara yake hiyo imelenga kuhakikisha kuwa miradi inayosuasua inatekelezwa na kuisha kwa wakati ili kutatua kero ya maji kwa wananchi kulingana na Sera ya Maji ya Mwaka 2002, kutimiza lengo la ifikapo mwaka 2025 wananchi wote mijini na vijijini wawe wanapata maji kwa asilimia mia.
Vilevile, Inj. Lwenge alifika kwenye Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira ya Wanging’ombe (WINGISA) kujionea utendaji wa mamlaka hiyo na kuzungumza na wafanyakazi wake kwa nia ya kuboresha utendaji wake.

PROF. MBARAWA AKAGUA CHUO CHA MABAHARIA (DMI)

mb1
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akitoa maelekezo kwa Mkuu wa Chuo cha Mabaharia cha Dar es Salaam (DMI) Eng. Yassin Songoro katika ziara yake ya kukagua Chuo hicho jijini Dar es Salaam.
mb2
Mkuu wa Chuo cha Mabaharia cha Dar es Salaam (DMI) Eng. Yassin Songoro (katikati) akimuongoza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa kukagua madarasa ya Chuo hicho.
mb3
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akikagua dira ya kuongozea meli (compass) katika moja ya darasa la Chuo hicho. Kulia ni Mkuu wa Chuo cha DMI Eng. Yassin Songoro.
mb4
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (mwenye tai) akikagua mitambo ya kuongozea meli katika moja ya madarasa ya chuo cha DMI wakati wa ziara yake chuoni hapo.

TRA yakamata shehena kubwa ya bidhaa za magendo

kay
Na Kalonga Kasati
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imefanikiwa kukamata bidhaa za magendo kwenye maeneo mbalimbali ya Ukanda  wa Bahari ya Hindi, Ziwa Victoria na mipakani.
Taarifa hiyo imetolewa leo na Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi (TRA) Bw. Richard Kayombo wakati akifanya mahojiano na Mwandishi wa Idara ya Habari (MAELEZO) ofisini kwake Jijini Dar es Salaam kuhusu juhudi za operesheni ya kutokomeza bidhaa za magendo nchini.
Bw. Kayombo ameeleza kuwa, mkoani Lindi TRA imefanikiwa kukamata mashua katika bandari ya Lindi ambayo ilisheheni bidhaa za magendo zenye thamani ya shilingi 159,361,046.
Ameongeza kuwa katika operesheni hiyo, TRA imefanikiwa kukusanya kodi ya jumla ya shilingi 10,500,678 kutoka katika bidhaa zilizokuwa katika nyaraka za forodha (manifest) ambapo pia inategemea kukusanya kodi ya shilingi 19,529,500 kutoka katika bidhaa ambazo zilikuwa katika nyaraka za forodha lakini thamani yake ilikuwa chini ya bei halisi.
 
Akitaja bidhaa hizo za magendo zilizokamatwa katika mashua hiyo ni mifuko 3,725 ya sukari yenye thamani ya shilingi 127,070,562, betri katoni 50, mchele mifuko 3,087, mafuta ya kula madumu 80, majokofu manne ya mtumba, baiskeli 4 za mitumba pamoja na katoni 20 za hamira.
“Mashua hiyo ilikamatwa katika bandari ya Lindi tarehe1 Februari, 2016 baada ya wasamaria wema kutoa taarifa ya kuwepo bidhaa za magendo ndani ya mashua hiyo ambapo upakuaji wa shehena hiyo ulianza mara moja.’’Alisema Kayombo.
 
Ameongeza kuwa,  Jijini Dar es Salaam, TRA kwa kushirikiana na kikosi cha doria cha Jeshi la Wanamaji wameweza kukamata Jahazi lenye jina la ‘Takbiri’ lenye usajili wa namba Z-875 likiwa limesheheni lita 19,700 za dizeli ambapo thamani yake bado haijapatikana kwakuwa imepelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya Uchunguzi zaidi.
Aidha, majahazi mengine matatu yamekamatwa katika eneo la Kigombe mkoani Tanga ambayo yalikuwa na bidhaa za magendo yenye thamani ya shilingi 99, 682, 273, 48 ambapo ndani kulikuwa na magunia ya sukari, mchele, mafuta ya kula, matairi ya magari, nyavu za kuzuia mbu, jokofu, jiko la umeme, rangi za kupuliza, betri na biskuti.  
 
Majahazi hayo yalitaifishwa baada ya wahusika kujitosa ndani ya maji na kutoroka.
TRA kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi inafanya doria saa 24 kila siku katika maeneo yote yaliyoshamiri upitishaji wa bidhaa za magendo pia imeunda Kanda Maalum katika maeneo ya Mbweni, Msasani, Kunduchi pamoja na Kigamboni.

No comments:

Post a Comment