Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Charles Kitwanga (kushoto meza kuu) akizungumza na Watendaji Wakuu wa
Idara ya Uhamiaji nchini (kushoto) pamoja na Wakuu wa Idara wa Wizara ya
Mambo ya Ndani ya Nchi (kulia), kuhusu masuala mbalimbali ya utendaji
wa kazi ndani ya Idara hiyo na Wizara kiujumla. Kikao hicho kilifanyika
katika Ukumbi wa Mikutano wa Wizara hiyo, jijini Dar es Salaam leo.
Kulia meza kuu ni Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Injinia Hamad Masauni.
Wakwanza upande wa kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Balozi
Simba Yahya, na wakwanza upande wa kushoto ni Kaimu Kamishna wa
Uhamiaji, Victoria Lembeli. Picha zote na Wizara ya Mambo ya Ndani ya
Nchi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Mhe. Charles Kitwanga ameagiza yafanywe mabadiliko makubwa katika
Vitengo mbalimbali vya Idara ya Uhamiaji ili kuboresha huduma na
kuimarisha uadilifu katika Vitengo hivyo.
Mheshimiwa Kitwanga ametoa
maagizo hayo leo wakati alipofanya kikao na Viongozi wa Idara ya
Uhamiaji ambapo pia kilihudhuriwa na Viongozi wa Wizara ya Mambo ya
Ndani ya Nchi, wakiwemo Wakuu wa Idara na Vitengo vya Wizara. Kikao
hicho kilifanyika katika Makao Makuu ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya
Nchi.
Katika kikao hicho, Mheshimiwa
Kitwanga ameagiza watumishi wote wa Idara ya Uhamiaji Walioko Uwanja wa
Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam na Uwanja wa Ndege
wa Kimataifa wa Kilimanjaro, wahamishwe na kupelekwa maeneo mengine
nchini, wakiwemo wale wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.
Wengine watakaohamishwa ni kutoka
Kitengo cha Pasipoti, Uhasibu, Hati za Ukaazi na Kitengo cha Upelelezi,
vyote vya Makao Makuu ya Uhamiaji jijini Dar es Salaam.
Aidha ameagiza pia kuwa Wakuu
wote wa Vitengo vya Upelelezi vya wilaya zilizopo jijini Dar es Salaam,
na pia wale wa Vituo vya Tunduma, Mtukula, Holili na Kasumulo,
wahamishiwe maeneo mengine, na pia watumishi wote waliokaa kwa zaidi ya
miaka mitatu katika Vituo hivyo.
Amesema hatua hii inayochukuliwa
sasa ni mwanzo tu wa mabadiliko makubwa yatakayofanywa katika Idara ya
Uhamiaji ili kuboresha huduma zinazotolewa na Idara hii ambayo ni moja
ya Idara muhimu za Serikali.
Amesema katika kuisafisha Idara
hii, uangalifu mkubwa utachukuliwa ili kuhakikisha kuwa Hakuna mtumishi
anayeonewa wala kupendelewa, lakini lengo kubwa ni kuvunja mtandao wa
wapokea rushwa na wale wasiowajibika.
Amesema kufuatana na utafiti
uliofanywa hivi karibuni umeonyesha kuwa matatizo ya rushwa katika Idara
ya Uhamiaji yanashika nafasi ya kwanza kwa kuwa na asilimia 30,
asilimia 20 ni Uongozi mbovu na asilimia 20 ni matumizi mabaya ya
madaraka. Asilimia 15 inahusisha vitendea kazi wa mifumo hafifu ya
kufanya kazi, asilimia 10 huduma mbovu na asilimia 5 ukabila na
upendeleo.
Amewataka Viongozi na watumishi
wote wa Idara ya Uhamiaji kufanya kazi zao kwa kuzingatia sheria, kanuni
na maadili ya kazi na waepuke vitendo vya kupokea rushwa na kusaidia
wahamiaji haramu na wauza madawa ya kulevya.
No comments:
Post a Comment