Na Kalonga Kasati
HALMASHAURI Wilaya ya Kinondoni
Jijini Dar es Salaam katika mwaka kipindi cha 2016/17 imepanga kununua
magari 40 yatakayotumika kwa ajili ya zoezi la ukusanyaji wa taka ngumu
katika Kata na Mitaa ya Halmashauri hiyo.
Hatua inaelezwa itasaidia kuondoa
kero ya mlindukano wa taka ngumu ambazo huzagaa ovyo, kutokana na
hushindwa kukusanywa kwa wakati na makampuni ya wakandarasi wa usafi
katika Kata na Mitaa wa Halmashauri hiyo.
Akizungumza na MAELEZO leo
(Jumanne Februari 23, 2016), Afisa Habari wa Halmashauri hiyo Sebastian
Mhowera alisema tayari ofisi hiyo pamoja na Halmashauri za Wilaya ya
Ilala na Temeke zimewasilisha ombi maalum la kuomba kibali cha ununuzi
wa magari hayo katika Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
Kwa mujibu wa Mhowera alisema
Halmashauri hiyo huzalisha jumla tani 2020 za taka ngumu ambapo uwezo
uliopo ni kuteketeza tani 1300 kwa siku, na hivyo kiasi kinachobaki
huibua changamoto katika namna ya kukabiliana na ongezeko hilo.
“Kiasi kikubwa cha taka
zinazozalishwa nyingi hubakia mitaani na hazifiki barabarani ambapo
ndipo hukusanywa kwa ajili ya kupelekwa dampo, kwani vitendea kazi
katika maeneo hayo ni changamoto” alisema Mhowera.
Alisema kwa mujibu wa Sera ya
Usafi, Makampuni ya Wakandarasi wa Usafi yaliyopo katika Mitaa yana
wajibu wa kukusanya taka zote kwani husimamiwa na wananchi wenyewe,
ambapo hata hivyo makandarasi mengi yamekuwa hayana uwezo wa kufanya
kazi hiyo.
Aidha Mhowera alisema katika
kufanikisha zoezi la usafi wa mazingira linalofanyika kila mwisho wa
mwezi nchini, Halamshauri hiyo imetoa maelezo mbalimbali ya kiutendaji
kwa Maaafisa Watendaji wa Mitaa na Kata.
No comments:
Post a Comment