Waziri wa Nishati na Madini
Profesa Sospeter Muhongo (mbele) akiongoza kikao kati yake na kampuni
inayojishughulisha na usambazaji wa vifaa na teknolojia katika utafutaji
wa mafuta na gesi ya Schlumberger. Pia kikao hicho kilihusisha
watendaji kutoka Wizara hiyo pamoja na taasisi zake likiwemo Shirika
la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC), Shirika la Madini la
Taifa(STAMICO), Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Mamlaka ya
Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA).
Waziri wa Nishati na Madini
Profesa Sospeter Muhongo akifuatilia kwa makini maelezo yaliyokuwa
yanatolewa na Meneja Masoko kutoka kampuni ya Schlumberger, Abdul
Adeshina (hayupo pichani) katika kikao hicho.
Meneja Masoko kutoka kampuni ya
Schlumberger, Abdul Adeshina akielezea shughuli zinazofanywa na kampuni
hiyo ikiwa ni pamoja na kusambaza vifaa na teknolojia kwa ajili ya
utafiti wa mafuta na gesi nchini.
Na Tabu Mullah
Waziri wa Nishati na Madini
Profesa Sospeter Muhongo ametaka makampuni yanayojishughulisha na
shughuli za utafutaji na uchimbaji wa gesi na mafuta nchini kuongeza
kasi ya utafiti kwa kutumia teknolojia ya kisasa ili sekta ya gesi na
mafuta iweze kukua na kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi.
Profesa Muhongo alitoa kauli hiyo
alipokutana na kampuni inayojishughulisha na usambazaji wa vifaa na
teknolojia katika utafutaji wa mafuta na gesi ya Schlumberger yenye
makazi yake jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kujadili utendaji kazi
wa kampuni hiyo.
Kikao hicho kilichofanyika jijini
Dar es Salaam kilihusisha watendaji kutoka Wizara hiyo pamoja na
taasisi zake likiwemo Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC),
Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Wakala wa Nishati Vijijini (REA)
na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA).
Alisema Tanzania kwa sasa ina
utajiri mkubwa wa rasilimali ya gesi ambayo itachochea katika ukuaji
wa uchumi wa nchi kupitia umeme wa uhakika utakaotumika katika viwanda
na kuongeza ajira kwa vijana wa kitanzania.
Aliendelea kusema kuwa ili sekta
ya gesi na mafuta iweze kuwa na mchango katika ukuaji wa uchumi wa
nchi, Tanzania inahitaji wawekezaji watakaowekeza kwa kasi kwa kutumia
teknolojia ya kisasa.
Alisisitiza kuwa serikali ipo
tayari kushirikiana na mwekezaji yeyote mwenye nia ya kuwekeza kwenye
sekta ya gesi na mafuta kwa kutumia teknolojia ya kisasa.
“ Kama serikali tumedhamiria
kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa miongoni mwa nchi zenye utajiri
unaotokana na rasilimali za gesi na mafuta, hivyo tunapenda
kushirikiana na wawekezaji kutoka sehemu mbalimbali ndani na nje ya
nchi kwa kutumia teknolojia ya kisasa,” alisema Profesa Muhongo
Profesa Muhongo aliihakikishia
kampuni ya Schlumberger kuwa serikali itafanya kazi kwa karibu nayo na
kutoa ushirikiano wowote utakaohitajika ili sekta ya gesi na mafuta
iweze kukua kwa kasi na kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi.
Awali akizungumza katika kikao
hicho Meneja Masoko kutoka kampuni ya Schlumberger, Abdul Adeshina
alisema kampuni yake imekuwa imekuwa ikitoa mafunzo kwa wafanyakazi
wa kitanzania asilimia 80 wanaofanya kazi katika kampuni hiyo.
Aliongeza kuwa kampuni hiyo
imekuwa ikishirikiana kwa karibu na Shirika la Maendeleo ya Petroli
Nchini (TPDC) katika shughuli za utafiti wa mafuta na gesi nchini na
kusisitiza kuwa kampuni hiyo ipo tayari kutumia teknolojia na vifaa
vyake katika kuboresha shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi nchini.
No comments:
Post a Comment