Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA)
limepokea kwa masikitiko na majonzi makubwa kifo cha Msanii Mkongwe wa
muziki wa dansi Kassim Mapili kilichotokea katikati ya wiki hii nyumbani
kwake Tabata jijini Dar es Salaam.
Na Tabu Mullah
Kassim Mapili ni msanii na mdau
wa muda mrefu wa sekta ya Sanaa nchini. Amekuwa ni taa na nuru ambayo
katika kipindi chote cha uhai wake imeangaza na kutoa mwanga angavu
kwenye sekta ya Sanaa.
Mchango wake katika muziki wa
dansi na ule wa kiweledi katika kuandaa na kukuza bendi na wasanii
mbalimbali wa muziki wa dansi nchini hautasahaulika kamwe. Ni Msanii
aliyeacha alama kuu katika muziki wa bendi na amejitolea kwa kiasi
kikubwa katika kuufikisha muziki wa dansi ulipo leo.
Aidha, pamoja na kuwa mwimbaji na
mpigaji gitaa katika Bendi mbalimbali zikiwemo za Kilwa Jazz, Polisi
Jazz, Vijana Jazz na nyingine nyingi Mzee Kassim Mapili alikuwa mstari
wa mbele kujenga mfumo wa Utawala kwenye sekta ya Sanaa na kuhakikisha
wasanii wa muziki wa dansi wanakuwa na chombo cha kuwawakilisha na
kutetea maslahi yao.
Mwaka 1982 alikuwa miongoni mwa
wasanii waliokutana Mjini Bagamoyo na kuunda Chama cha Muziki wa Dansi
Tanzania (CHAMUDATA) ambacho hadi leo kinatetea na kuwawakilisha wasanii
wa muziki wa dansi.
Aidha, Mzee Mapili amekuwa bega
kwa bega na Baraza la Sanaa la Taifa katika programu zake mbalimbali na
utendaji kazi wa kila siku. Kwa mfano; amekuwa mmoja wa wadau ambao
wamekuwa wakishiriki kikamilifu kwenye Programu ya Jukwaa la Sanaa
inayoandaliwa na BASATA kwa kushirikiana na chama cha waandishi wa
habari za Sanaa na Utamaduni.
Baraza, wasanii na wadau wote wa
Sanaa hatuna budi kuendelea kuenzi mema yote aliyotuachia marehemu
Kassim Mapili hasa katika kutunga nyimbo za hamasa na ujumbe makini na
wenye mashiko kwa jamii yote ya Watanzania
.
Hakika pengo lililoachwa na
Marehemu haliwezi kuzibika, kwani imekuwa ni kama mshumaa uliyozimika
ghafla wakati tukiingia kwenye giza.
Baraza linatoa pole kwa familia
ya Marehemu, chama cha muziki wa dansi, shirikisho la muziki na wasanii
wote kwa ujumla. Ni matumaini ya Baraza kwamba, tutaendelea kuenzi mema
yote yaliyotendwa na Marehemu, hasa kudumisha upendo na amani katika
tasnia yetu ya Sanaa na taifa kwa ujumla.
Bwana ametoa na Bwana ametwaa, Amen
Godfrey Mngereza
KATIBU MTENDAJI
No comments:
Post a Comment