Muonekano wa Uwanja wa Ndege wa
kimataifa wa KIA mkoani Kilimanjaro unaojengwa njia za kutua na kuruka
ndege na kukarabatiwa jengo la abiria. Ujenzi huo unafanywa na kampuni
ya NACO kutoka Uholanzi.
Mafundi wakiendelea na ujenzi wa njia ya kuruka na kutua ndege katika Uwanja wa Ndege wa kimataifa wa KIA mkoani Kilimanjaro.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akielekea kukagua ujenzi wa njia za
kuruka na kutua ndege mara baada ya kukagua hanga la uwanja huo.
Katikati ni Mkurugenzi wa Via Avaiation Bi. Susan Mashibe ambaye ni
Muwekezaji wa Hanga hilo.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akijadiliana jambo na Mkurugenzi wa Via
Avaiation Bi. Susan Mashibe ambaye ni Muwekezaji wa Hanga katika Uwanja
wa Ndege wa KIA.
Meneja wa Wakala wa Barabara
(TANROADS) mkoa wa Arusha, Eng. John Kalupale (wa pili kulia) akifafanua
jambo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame
Mbarawa (kushoto) kuhusu ujenzi wa barabara ya Kia-Mererani yenye urefu
wa Km 26 unavyoendelea.
Muonekano wa moja ya makalvati makubwa yaliyojengwa katika barabara ya Kia-Mererani yenye urefu wa Km 26.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akifafanua jambo kwa Mhandisi Mshauri
anayesimamia mradi wa ujenzi wa barabara ya Kia-Mererani Km 26.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (kushoto) akikagua karakana ya Wakala
wa Ufundi na Umeme TEMESA mkoani Manyara.
Serikali imeitaka kampuni ya
KADCO inayoendesha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA),
kuongeza mapato na kuimarisha ulinzi ili kulinda hadhi ya uwanja huo,
kuchangia pato la serikali na kudhibiti hujuma dhidi ya watu wasio
waaminifu.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amesema hayo wakati akikagua utendaji
wa uwanja huo na mradi wa ujenzi wa njia za kurukia ndege na jengo la
abiria unaondelea katika uwanja huo.
Prof. Mbarawa amemtaka Kaimu
Mkurugenzi wa KADCO Bw. Bakari Mururusi, kuhakikisha kuwa uwanja huo
kuanzia mwaka huu wa fedha unazalisha mapato yanayowiana na hadhi yake
na kuchangia kikamilifu mapato ya Serikali na kuachana na utamaduni wa
kufanya kazi kwa mazoea.
“Siridhiki na kiasi cha bilioni
18 mnazozalisha kwa mwaka, nawataka kuanzia sasa mkusanye mapato ya
kutosha na kudhibiti vitendo vya hujuma ili kuupa hadhi inayostahili
uwanja huu”, amesisitiza Prof. Mbarawa.
Amemtaka Muwekezaji wa Hanga
(garage) la Uwanja huo kujiandaa kuondoka kutokana na kutowekeza
kikamilifu katika kipindi cha miaka 10 alichokodishiwa na kusisitiza
kuwa nia ya Serikali ni kukabidhi hanga hilo kwa Shirika la Ndege nchini
(ATCL), ifikapo Julai mwaka huu ili lifanye kazi kwa faida na madhumuni
yaliyokusudiwa.
“Nia ya Rais ni kufufua ATCL liwe
na hadhi inayoshatahili hivyo hanga hili tutawapa ATCL na kuwasimamia
ili wafanye kazi kikamilifu na kuleta mapato kwa Serikali”, amefafanua
Waziri Prof. Mbarawa.
Waziri Prof. Mbarawa amemweleza Mkurugenzi wa Kampuni ya Via Aviation
inayomiliki hanga Hilo kwa miaka 10 kuwa Serikali hairidhishwi na
mapato yanayotokana na hanga hilo hivyo imejipanga kuitumia kuleta faida
zaidi kwa Serikali katika mkakati wake wa kukuza uchumi.
Katika hatua nyingine, Prof.
Mbarawa amekagua ujenzi wa barabara ya Kia-Mererani yenye Urefu wa Km 26
inayojengwa na Kampuni ya Chicco kwa gharama ya shilingi bilioni 32.2
na kumtaka mkandarasi huyo kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa
wakati.
Kwa upande wake Meneja wa Wakala
wa Barabara (TANROADS) mkoa wa Manyara, Eng. Yohani Kasaini
amemhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kuwa licha ya barabara hiyo kupita
katika Ukanda wa tambarare jumla ya makalavati makubwa 6 na madogo 85
yanajengwa ili kukabiliana Na changamoto ya mafuriko na hivyo kuiwezesha
barabara hiyo kupitika wakati wote wa mwaka.
Barabara ya Kia-Mererani ina
umuhimu wa kipekee kiuchumi kwani inapita katika ukanda wenye Rasilimali
zenye madini ya Tanzanite, eneo zuri la kilimo, ufugaji, utalii na
misitu hivyo kukamilika kwake kutapunguza gharama za usafiri na kuvutia
watalii wengi kuja nchini.
Serikali iko katika mkakati wa
kuimarisha uwanja wa ndege wa KIA kwa kukarabati jengo la Abiria na njia
za kutulia na kurukia ndege ambapo kampuni ya NACO kutoka Uholanzi
inajenga Uwanja huo ili kuuwezesha kufanya kazi kisasa, kuruhusu ndege
nyingi kutua na kuongeza mapato ya uwanja huo na Serikali kwa ujumla.
Katika hatua nyingine Prof.
Mbarawa amewataka watendaji wa taasisi zilizo chini ya wizara hiyo Mkoani Manyara kufanyakaz kwa umoja, uwazi, uadilifu ili kuiwezesha
lengo la wizara hiyo la kujenga miundombinu itakayoliwezesha taifa
kufikia uchumi wa kati 2025 kutimia kwa wakati.
No comments:
Post a Comment